2016-11-18 06:46:00

Kanisa ni kwa ajili ya watu pamoja na watu!


“Tuko upande wa watu, na ni lazima tuwepo kwa ajili yao, pale ambapo serikali haiwezi kuwasaidia”. Ndugu msikilizaji hayo maneno ya kutafakarisha juu ya tabia, wajibu, na utendaji wa Mchungaji mwema, anayatamka Kardinali Mteule John Ribat, Askofu mkuu wa Port Moresby, Papua New Guinea. Akieleza safari yake ya wito wa ukasisi, Kardinali Mteule Ribat anasema, wazazi wake wamekuwa na nafasi kubwa katika kujenga hisia za utumishi ndani yake. Alipokuwa angali mdogo, wazazi wake, hawakuwa watu walioelimika sana, lakini walikuwa na imani thabiti. Walikuwa wakiishi kijijini, na walipaswa kutembea umbali wa kutosha na kuvuka mito kwa mitumbwi, ili kufika shule iliyokuwa mjini, ambapo wamisionari walikuwa wakiadhimisha Misa Takatifu. Mwendo huu wakati mwingine uliwachukua takribani masaa 8.

Wamisionari hao walikuwa Wajerumani, na katika umri wake mdogo, Kardinali mteule Ribat, alivutiwa na utendaji wao, na jinsi watu walivyowaamini. Hivi ndivyo mbegu ya wito wa ukasisi ilivyoanza kumea ndani yake. Akiwa shule ya Sekondari mchanganyiko ya serikali, kati ya walimu walikuwapo watawa wa kike na wa kiume, ambao waliwapenda na kuwajali wanafunzi. Walikuwa wanasali pamoja Rozari, wanaandaa maadhimisho ya Misa Takatifu, huku wakifunzwa jinsi wakubwa zaidi wawasaidie walio wadogo. Hapo ndipo akafanya maauzi ya kuwa padre, akisukumwa na roho ya utumishi na kujali.

Ukristo umewasaidia watu wa Papua New Guinea kuthamini zaidi maisha ya jumuiya na udugu, kwa moyo wazi na ukweli. Kabla, waliishi kadiri ya tamaduni asilia, ambazo pamoja na tunu nzuri walizokuwa nazo, bado walipendelea kuishi kwa mshikamano wa familia na koo chache, wakati familia nyingine wakiwekwa pembeni. Lakini leo, ukristo umewafanya wajisikie wote ni wamoja, wote ni ndugu. Wanajitambua kuwa Kanisa ni lao, nao ni sehemu ya Kanisa, na ndiyo maana maadhimisho ya liturjia yanachangamka sana kwa ushiriki kamilifu wa kila mwamini.

Changamoto hazikosekani, hasa kwenye upande wa Maisha ya ndoa ya kikatoliki na useja. Tamaduni za Papua New Guinea zinatambua ndoa halali na kamili, pale ambapo kuna matunda ya watoto. Wanapokosekana mara nyingi ndoa huyumba, kukosa uaminifu na utengano wakati mwingine. Hivyo baadhi ya vijana wanakwepa kufunga ndoa Kanisani, kwa kuhofia kujifunga, sababu Kanisa Katoliki haliruhusu talaka, bali laweza kuitangaza ndoa batili, iwapo ilikuwa batili tangu awali. Kwa upande wa maisha ya wakfu, utii, ufukara na usafi wa moyo; vijana wengi wanakwepa sababu wanatamani kuwa na watoto na kuishi maisha ya ndoa. Jambo hili ni jema, hata hivyo maisha ya wakfu, useja na usafi wa moyo yana thamani na umuhimu wake. Yanawezekana hasa pale mhusika anapopalilia mahusiano mazuri na familia yake, na waamini kwa ujumla, kasisitiza Kardinali mteule John Ribat.

Papua New Guinea ni kati ya nchi zinazoshuhudia tayari madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Baadhi ya visiwa vimechukuliwa na maji, barabara na nyumba za watu vimeharibiwa vibaya, watu wanalazimika kuhama na hawana pa kwenda. Wakulima hawavuni vizuri sababu ya uhaba wa mvua, na wanapofanikiwa kuvuna mazao au matunda mara nyingi wanashindwa kuvila, sababu vinakuwa na chumvi nyingi, kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Kwa hali kama hii, anahimiza Kardinali mteule Ribat, Kanisa lipo upande wa watu, na serikali inaposhindwa kuwasaidia watu, Kanisa linafanya hivyo kwa kutetea haki zao msingi, utu na heshima yao kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Changamoto nyingine ni vijana wengi kukimbia vijiji na kuhamia mijini kwa matumaini kwamba watapata kazi na maisha mazuri. Lakini wengi wanaishia kukata tamaa na kulewa, sababu mijini maisha sio mepesi na hakuna nafasi za kazi kama wanavyodhani. Jimbo kuu la Port Moresby linaandaa utaratibu wa kuwakusanya na kuwaelimisha vijana hao wanapofika maeneo hayo, ili kuwapa mwanga wa kutafakari vizuri juu ya fursa za uchumi wanazotafuta, na kwamba ni bora zaidi kurudi kijijini ambapo walikuwa wanapata chochote hata kama katika hali ya umaskini. Jambo la msingi zaidi, wajifunze kuridhika na maisha ya vijijini, huku wakishirikiana kuyaboresha.

Suala la dini na imani linapoteza nafasi kwa wakristo wengi wanaokumbatia maisha ya kisasa na kumweka Mungu kando. Hii ni hatari kwa vizazi vijavyo, sababu hakuna maisha ya furaha na amani, iwapo Mungu hapewi nafasi katika maisha na utaratibu wa kila siku. Mahusiano ya kiekumene nchini Papua New Guinea ni mazuri ingawa bado yana changamoto zake. Wakatoliki na makanisa mengine wameungana kushirikiana kwa mambo yanayowagusa kwa pamoja, mfano upande wa ugonjwa wa Ukimwi, ambapo baadhi bado wanawatenga na kuwanyanyapaa wagonjwa. Mahusiano ya kiekumene wanawaelimisha watu kwa pamoja njia za kuepukana na maambukizi, na pia kuwajali na kuwapenda wagonjwa, wakiwahudumia siku zote huku wakijali utu wao.

Askofu mkuu John Ribat alizaliwa mnamo mwaka 1957, huko Volavolo, kwenye kanda ya East New Britain, nchini Papua New Guinea, akiwa mtoto wa 7 kati ya watoto 9. Alijiunga na wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, na mwaka 2007 akawekwa kuwa Askofu mkuu wa Port Moresby. Kabla ya utume huo, aliliongoza Jimbo Katoliki la Bereina, amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Papua New Guinea na Visiwa vya Salomon. Kwa sasa ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Oceania Tarehe 19 Novemba 2016, atapewa hadhi ya ukardinali, katika Kanisa Kuu la Mt. Petro, mjini Vatican, na kuwa Kardinali wa kwanza wa Papua New Guinea.

Kardinali Mteule John Ribat, anaongelea kuhusu heshima hiyo ya ukardinali kwamba: kwa kuwa ni mapenzi ya Mungu, basi Mungu mwenyewe amjalie nguvu za kuumudu wajibu huo. Heshima ya ukardinali ni heshima wanayopewa baadhi ya watumishi wa Mungu katika Kanisa Katoliki ili kuwa washauri wa Baba Mtakatifu, na kumchagua Baba Mtakatifu mpya pale ambapo Kiti hicho cha Khalifa wa Mtume Petro kinapokuwa wazi.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.