2016-11-17 15:35:00

Wakristo wanaalikwa kujisadaka kwa ajili ya umoja na udugu!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 17 Novemba 2016 amekutana na kuzungumza na Patriaki Mar Gewargis III, Katolikos wa Kanisa la Assira ya Mashariki na amemtakia neema na baraka pamoja na kuonesha masikitiko yake kutokana na hali tete huko Mashariki ya kati na kwa namna ya pekee, Iraq na Syria ambako watu wanaendelea kupoteza maisha kutokana na vita ambayo kamwe haiwezi kuhalalishwa. Huko kuna watu wanajaribiwa na kuteseka kila siku ya maisha yao.

Baba Mtakatifu anasema, hawa ni watu wanaoendelea kufuata Njia ya Msalaba, huku wakiunganisha mateso yao na yale ya Kristo Yesu, chemchemi ya upatanisho, changamoto na mwaliko wa kuendelea kushikamana katika Kristo, ili kuumbata Msalaba na kuaminia upendo wake, kwani Yesu ndiye kiini cha imani kwa wafuasi wake. Wakristo wanaalikwa hata katika utofauti wao, kuendelea kujitahidi kuishi ujumbe wa upendo, upatanisho na msamaha, shule tosha kabisa kutoka kwa mashuhuda wa imani, wanaoendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake kwa kushinda ubaya kwa wema. Damu Azizi ya Yesu iliyomwagika ni chemchemi ya upendo, upatanisho na umoja inayoliwezesha Kanisa kusonga mbele kama ilivyo pia damu ya mashuhuda wa imani ambayo imekuwa ni mbegu ya umoja wa Wakristo, mwaliko wa kujisadaka katika udugu na umoja!

Ushirikiano kati ya Makanisa haya mawili unaendelea kuimarishwa tangu wakati ule Patriaki Katolikosi Mar Dinkha IV alipokutana na Mtakatifu Yohane Paulo II na wote kwa pamoja wakaweka sahihi katika Tamko la Pamoja kuhusu Uelewa wa Kristo kwa kuungama imani moja katika Fumbo la Umwilisho. Tukio hili lilifungua hija ya pamoja kuelekea katika umoja kamili wa Kanisa, utashi unaodhihirishwa na Kanisa Katoliki katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ambayo kwa sasa yamefikia hatua kubwa zaidi.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Tume ya pamoja ya majadiliano ya kitaalimungu kati ya Makanisa haya mawili, itayasaidia Makanisa haya siku moja kufikia umoja kamili. Lakini kwa wakati, waamini wa Makanisa haya wanapaswa kuendelea kufahamiana kwa kushuhudia Injili kwa pamoja, ili ukaribu wao iwe ni chachu ya umoja na upendo kwani kiini cha umoja huu kinafumbatwa katika Sakramenti ya Ubatizo na kwamba, wote wanajenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, mwaliko wa kuendelea kutembea pamoja katika sala na upendo. Wamwombe Kristo Yesu, Mganga mahiri agange na kuponya madonda ya nyuma kwa njia ya mafuta ya huruma yake.

Ni vyema ikiwa kama Makanisa haya mawili yataendelea kujikita katika ushuhuda wa Uinjilishaji wa pamoja kama ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo. Huo ukawa ni mwanzo wa Injili na nguzo ya imani iliyoenea sehemu mbali mbali za dunia na hivyo kuchipusha Jumuiya za Kikristo. Wainjilishaji wakuu wa nyakati hizo, watakatifu na mashuhuda wa imani wa nyakati zote wanawasindikize Wakristo ili kujenga umoja na kushuhudia Injili kwa pamoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.