2016-11-17 16:13:00

Wafanyabiashara jihadharini na uchu wa mali na rushwa: Jengeni udugu


Shughuli zozote za uwekezaji, zinazoshirikisha wote na hasa wanyonge kiuchumi na kijamii, zinaweza kuwa ni shughuli za huruma ya Mungu, ambapo wahusika wote wanashiriki upendo wa Mungu kwa wanadamu. Uwekezaji una hatari zake nyingi, zinazoshuhudiwa hata katika Injili, mfano wa hazina iliyofichwa katika shamba au lulu ya thamani inayotafutwa na mfanya bishara (Rej., Mathayo 13: 44-45). Kwa maneno hayo Baba Mtakatifu Francisko, siku ya Alhamisi, tarehe 17 Novemba 2016, amewaalika wanachama wa Umoja wa kimataifa wa wawekezaji wa kikatoliki, kutafakari pamoja naye hatari tatu wanazopambana nazo katika uwekezaji: matumizi ya fedha, uaminifu na udugu.

Akiongelea matumizi ya fedha, Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha jinsi watangulizi wake Leo XIII, Paul VI, na Yohane Paulo II walivyohimiza kwamba tamaa ya fedha imegawanya jamii katika utofauti wa kina kirefu kati ya maskini na tajiri. Utafutaji na matumizi mabaya ya fedha na mamlaka, umepelekea kuingia kwa namna mpya ya utawala wa kidikteta kwa upande wa uchumi, jamii, tamaduni na siasa. Kristo katika mfano wa karani asiye mwaminifu, anafundisha kutumia mali ya dunia kujitengenezea marafiki, ili waweze kuwapokea  katika makao ya milele. (Rej., Luka 16: 9-15). Tangu mababa wa Kanisa wa Karne za kwanza, wameitafsiri sehemu hiyo ya Injili kwamba, fedha na mali ni nzuri na vinafaa, pale ambapo vinatumiwa kwa ajili ya kumhudumia jirani, na sio kwa kujitafutia faida binafsi. Fedha ni nyenzo ya kiteknolojia inayotumika katika kuthaminisha vitu, haki, na wajibu. Iwapo fedha na mali vitapoteza lengo lake la mwisho, basi vinapoteza nguvu yake. Hivyo wawekezaji wasitafute kujilimbikizia mali, bali kuhudumia wahitaji, sababu wawekezaji wapo kwa ajili ya kutoa huduma.

Shughuli za kifedha na mihamala yote vitendeke kwa akili na ujuzi wa kutosha, huku wahusika wakikubali sadaka ya kuachana na baadhi ya mambo mfano faida kubwa kwa migongo ya maskini na wanyonge. Zaidi sana, kila faida inayopatikana itumike kwa ajili ya kuwasaidia wanyonge na maskini, kutoa huduma za elimu na afya, na uboreshaji wa miji ambayo iko nyuma kimaendeleo. Kutojali hayo, ni kuanguka katika ibada ya sanamu ya masoko ya biashara.

Hatari ya pili ni kukosa uaminifu na kukumbatia rushwa. Hili hupelekea unyanyasaji kwa walio wanyonge, kiasi cha kukosa huduma msingi katika jamii. Ni uharibifu wa jamii, ni unyonyaji wa maskini, ni dhihaka kwa demokrasia na ubinafsi ulio kubuhu. Kwa wenye tabia za rushwa na dhuluma huanguka katika mtego wa ibada ya sanamu ya fedha, na wanakuwa wafungwa na watumwa wa ibada hizo za kishetani. Rushwa, dhuluma, na ukosefu wa uaminifu kwenye mali, ndivyo vimepelekea kuzuka na kukua kwa biashara za utumwa, ukahaba, madawa ya kulevya, bishara za silaha an kadhalika, sababu wanamfuata Ibilisi, aliye baba wa uzushi.

Rushwa, udhalimu na ukosefu wa uaminifu kwa ujumla ni hatari kwa siasa, kwa wawekezaji, kwa fani ya mawasiliano, kwa Kanisa na hatari kwa mashirika yote ya kijamii. Iwapo hawatachukua tahadhari, wataangukia katika ibada ya sanamu ya fedha. Baba Mtakatifu Francisko amewaalika wawekezaji hao, kujifunza kutoka kwa mifano ya Mt. Petro na wakristo wengi wa awali, waliogoma kuabudu miungu ya fedha na mali, wakawa tayari kuifia imani yao ndani ya Kristo.

Hatari ya tatu ni kutojali udugu. Katika shughuli zote za uwekezaji na biashara ni muhimu kuzingatia utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na kukabidhiwa kwa pamoja matumizi na utunzaji wa mali hizo, kwa faida ya wote. Kwa sababu hiyo, ni muhimu ukarimu wa kisiasa, kijamii, na kiuchumi unaomwelekea Mungu kupitia kila mwanadamu, hasa kwa wahitaji. Ukarimu huu ufumbatwe katika dhana ya utu na udugu, kwa kutambua kuwa wanadamu wote ni sehemu ya familia pana ya wana wa Mungu. Mahusiano ya haki kati ya waajili na waajiliwa yanapaswa kuheshimiwa kwa pande zote mbili. Heshima hiyo ya kila mmoja kama ndugu, iwekwe pia kwa jamii ambapo wahusika wanawekeza, ili wakazi wa mahali hapo wafaidike pia kwa kiasi kikubwa na uwekezaji wao. Baba Mtakatifu Francisko, kawaasa kuendeleza vyama na mashirika yanayokuza udugu kati yao.

Amegusia suala la wahamiaji na wakimbizi ambalo linaumiza mioyo ya watu wengi leo. Kanisa katika nafasi mbali mbali linaendelea kushughulika ili kuwasaidia wahusika, na zaidi kutatua vyanzo vya migogoro na mahangaiko katika nchi wanamotoka. Hata hivyo Baba Mtakatifu amewaalika wawekezaji kulitazama kwa namna ya pekee na kutumia nafasi zao kutafuta suluhu za vyanzo vya wengi kukimbia maeneo yao. Wawekezaji watoe pia fursa za kutosha kwa ujengaji uchumi kwa makundi ya wahamiaji na wakimbizi. Ikumbukwe kwamba, wengi wa wanadamu sehemu wanazoishi leo, babu na baba zao walikuwa wahamiaji maeneo hayo. Kumbe, suala la uhamiaji sio la kubeza au kukwepa, linawahusu wote.

Amewaalika kujifunza kutoka kwa mfano wa Enrique Shaw, aliyekuwa mwekezaji mzuri na mwenye kujali mahitaji ya wengine. Baba Mtakatifu Francisko, alipokuwa Askofu mkuu wa Buenos Aires, alianzisha mchakato wa Shaw kuwa mtakatifu. Kwa sababu hiyo kawaalika wawekezaji wakatoliki, wamuombe Enrique Shaw awaombee wawe wawekezaji wazuri. Kwa mfano wa Zakayo, aliyekuwa tajiri na muwekezaji wa Yeriko, waongoke ili waifae jamii kwa huduma zao za ukarimu na uungwana.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.