2016-11-17 15:59:00

Uekumene: Fumbo la Umwilisho na Maisha ya Kisakramenti!


Patriaki Katolikos Mar Gewargis III, wa Kanisa la Assira ya Mashariki kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuliongoza Kanisa, amekutana na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 17 Novemba 2016 mjini Vatican. Amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, damu ya Wakristo inayoendelea kumwagika huko Mashariki ya Kati, itakuwa ni chemchemi ya furaha ya maisha ya kiroho na faraja kutoka kwa Kristo Yesu. Hawa ni watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao, mahali ambapo kumekuwa ni mwanzo wa ustaarabu wa maisha ya mwanadamu na kukua pamoja na kupanuka kwa Kanisa la Mwanzo. Wakristo huko Mashariki ya Kati wanaendelea kumshuhudia Kristo na Kanisa lake kwa kumwaga damu.

Kwa mara ya kwanza Patriaki Katolikos Mar Gewargis III, alikutana na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1991 ili kumshirikisha wasi wasi wake kutokana na mashambulizi yaliyokuwa yanahatarisha amani huko Mashariki ya Kati, lakini haikuwezekana kutokana na kiburi cha wanasiasa kutoguswa na mahangaiko ya wananchi wa kawaida. Wakristo nchini Iraq wanaendelea kukimbia nchi yao, hali inayowasababishia mateso na mahangaiko makubwa kama wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Wengi wao ni wale wanaoteseka kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Kutokana na changamoto hii, Wakristo wanapaswa kuimarisha umoja na mshikamano, kwa kujizatiti kikamilifu ili kuwasaidia watu wanaoteseka huko Mashariki ya kati. Kutokana na changamoto hii, viongozi wakuu wa Makanisa huko Mashariki wanataka kuitisha mkutano wa kimataifa ili kupembua kwa kina na mapana mateso na mahangaiko ya wananchi wengi huko Mashariki ya Kati, kwani wananchi hawa kutoka Mashariki wamezamisha matumaini ya usalama wa maisha yao kwa viongozi wa Makanisa.

Patriaki Katolikos Mar Gewargis III, ametumia fursa hii, kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho kati ya watu wa mataifa wanaoendelea kuogelea katika dimbwi la vita, kinzani na  mipasuko ya kijamii. Anasema, kuna haja ya kusitisha vita, nyanyaso na dhuluma za kidini duniani. Safari hii ya kikazi ni sehemu ya utekelezaji wa majadiliano ya kiekumene pamoja na matunda ya mkutano wa kiekumene kati ya Papa Yohane Paulo II na Patriaki Mar Dhinka IV. Sasa wanaangalia uwezekano wa kuwa na Tamko la Pamoja kuhusu Maisha ya Kisakramenti kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.