2016-11-17 16:46:00

Tamko la viongozi wa kidini kuhusu mazingira kwa Jumuiya ya Kimataifa!


Yapigwe marufuku matumizi endelevu ya mafuta machafu yasiyokubalika kimaadili. Huu ni wito wa viongozi takribani 220 wa itikadi mbali mbali za kidini na imani, kwa wakuu wa nchi wa mataifa, Cop22, waliokutana mjini Marrakech, Morocco, kwa ajili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Baadhi ya wakuu wa dini waliozungumza ni pamoja na Askofu Marcelo Sanchez Sorondo, Katibu wa taaisisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii, Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Sayyid M. Syeed wa Chama cha Waislamu wa Marekani Kaskazini na Desmond Tutu, Askofu mkuu mstaafu wa Kanisa Anglikani.

Wakuu wa dini wamehimiza Jumuiya ya Mataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti kwa ajili ya kutetea haki kwa hali ya hewa ulimwenguni, hali ambayo kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, inaathiri sana maisha ya jamii na mazingira. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, mazungumzano hayakwepeki, kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake ya Kitume, laudato sì, yaani sifa iwe kwako:juu ya utunzaji wa Nyumba ya wote. Ni wajibu wa mataifa yote kutazama upya na kuweka utaratibu stahiki wa uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya Nishati na bidhaa zote ulimwenguni na kubadili mtindo wa maisha.

Wakuu wa dini wametoa mapendekezo kadhaa ili kuharakisha ubadilishwaji wa taratibu za uzalishaji na usafirishaji wa Nishati kwa ajili ya mazingira na hewa safi kwa siku za usoni, kwani muda ni mfupi katika kukabili hatari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi. Katika hilo wamesisitiza kuhakikisha katika viwanda joto lisizidi nyuzi joto 1.5, ukilinganisha na nyakati za kabla ya uzalishaji viwanda. Zaidi wamependekeza kuzuia kabisa matumizi ya mafuta machafu, badala yake mataifa husika yawekeze kwenye nishati-rafiki na suluhu zingine za uasili wa mimea, pia waongeze misaada ya kifedha kiulimwengu ili kutokomeza umaskini wa Nishati, zilindwe haki za binadamu kwa kuweka nguvu zaidi kuzuia mabadiliko ya tabia nchi, na udhibiti wa uzalishaji na biashara holela zisizojali haki msingi za binadamu.

Katika mji wa Marrakech, Morocco, wamekutana mataifa 192 ili kukubaliana utendaji na hatua za pamoja zitakazoweza kusaidia udhibiti wa uzalishaji katika kila taifa, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.