2016-11-16 09:13:00

Marekani jengeni madaraja ya watu kukutana na wala si kuta za utengano


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kuanzia tarehe 14-17 Novemba 2016 linafanya mkutano wake wa mwaka ili kujadili sera na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji nchini Marekani. Katika tukio hili, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia Maaskofu wa Marekani ujumbe kwa njia ya video, akikumbuka kwa namna ya pekee hija yake ya kitume nchini Marekani, kwa mwaka 2015. Alishuhudia mwenyewe umoja na utofauti unaofumbatwa katika maisha na utume wa Jumuiya ya Wakatoliki nchini Marekani na kwamba, kwa historia ya Kanisa inaonesha kwamba, kwa miaka mingi Marekani imeonesha ukarimu mkubwa kwa wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Wahamiaji hawa wamekuwa ni sehemu ya utajiri mkubwa wa Marekani kutokana na lugha na tamaduni zao; mambo ambayo yamesaidia kuleta mabadiliko katika uso wa Kanisa nchini Marekani. Kuanzia Januari mwaka 2017 hadi  Septemba, 2018: Majimbo ya Kanisa Katoliki nchini Marekani yataadhimisha Kongamano la Tano la Kitaifa la Shughuli za Kichungaji kwa lugha ya Kihispania. Kongamano hili linalojulikana kama “Encuentro” linapania pamoja na mambo mengine kutambua na kuenzi tunu msingi zinazobubujika kutoka katika maisha na utume wa waamini wa Kanisa Katoliki wenye utamaduni na wanaozungumza lugha ya Kihispania.

Hili ni kundi ambalo limekuwa na mchango mkubwa anasema Baba Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa nchini Marekani. Kongamano hili liwe ni sehemu ya mchakato wa upyaishaji wa ari na moyo wa kimissionari, changamoto kwa Makanisa Mahalia. Baba Mtakatifu anaendelea kukaza kwa kusema, changamoto kubwa mbele ya Mama Kanisa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni kujenga utamaduni wa watu kukutana ili kushirikishana tamaduni na mang’amuzi yao; kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano, ili kujenga madaraja ya watu kukutana.

Baba Mtakatifu analitaka Kanisa nchini Marekani na duniani kote, kutoka kifua mbele ili kuwa chachu ya umoja, kati ya Wakristo, kati ya raia pamoja na wale wote wanaotafuta matumaini ya leo na kesho iliyo bora katika maisha yao!. Kanisa linapaswa kutambua dhamana yake ya kuendelea kuwa ni mitume na wamissionari waliojazwa na upendo wa Kristo Yesu na ari ya kutangaza na kushuhudia Injili. Jumuiya ya Kikristo inapaswa kuwa ni alama na unabii wa mpango wa Mungu kwa familia ya binadamu, daima ikiwa ni chombo na shuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, kwa jamii ambayo inakabiliwa na changamoto mbali mbali katika maisha ya kijamii, kitamaduni na kiroho pamoja na kuongezeka kwa mwingiliano wa watu.

Ni Matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kanisa nchini Marekani katika ngazi mbali mbali litaenzi mchakato huu wa kongamano la kichungaji kwa tafakari na mang’amuzi ya shughuli za kichungaji, ili kuliwezesha Kanisa nchini Marekani kufaidika zaidi na uwepo wa waamini kutoka katika tamaduni za kihispania. Baba Mtakatifu anatumaini kwamba, kongamano hili litaweza kuzaa matunda ya upyaisho wa Jamii ya Wamerekani sanjari na utume na maisha ya Kanisa nchini Marekani. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake. Anawaweka Maaskofu pamoja na waamini wao chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.