2016-11-16 09:44:00

Kumbu kumbu ya miaka 20 ya Tuzo ya Amani kwa Chiara Lubich


Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe Bwana Marco Desalvo Rais wa Chama cha kitume cha Ubinadamu mpya - Wafokolari akiwatakia heri na baraka katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 20 ya Tuzo ya Amani iliyotolewa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO kwa Muasisi wa Chama hiki Hayati Chiara Lubich mintarafu elimu kwa ajili ya amani. Chama hiki kimeendelea kuwa mstari wa mbele kwa kushirikiana na wadau wengine kama UNESCO kujikita katika majiundo makini ya amani, upatanisho; urafiki na maridhiano kati ya watu wa mataifa, lugha, tamaduni na dini mbali mbali.

Baba Mtakatifu anawapongeza Wafokolari kwa kuendelea kujizatiti katika kuwafunda watu tunu ya amani, dhamana ambayo Chiara Lubich aliivalia njuga kwa nguvu zake zote na kuonesha udumifu. Anapenda kuwatia shime washiriki wa tukio hili lililofanyika mjini Paris, Ufaransa, Jumanne tarehe 15 Novemba 2016 kuendelea kupyaisha fadhila ya amani, ili kweli amani iweze kuwa ni matunda ya maendeleo endelevu kwa wote kwa kutambua mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa yanayojikita katika heshima, sanaa ya kusikilizana kwa makini; makini kwa mahitaji na shida za jirani; haki, majadiliano na ushirikiano. Baba Mtakatifu anawakia heri na baraka katika tafakari zao, ili ziweze kuzaa matunda ya amani, mwishoni, amewapatia washiriki wote baraka zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.