2016-11-16 09:57:00

Amani inarutubishwa kwa njia ya haki jamii, heshima na maridhiano!


Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mama Chiara Lubich, Muasisi wa Chama cha Wafokolari alipopewa tuzo ya Amani na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO imekuwa ni fursa nyingine tena kwa wadau mbali mbali kujizatiti katika mshikamano na wadau mbali mbali duniani ili kushuhudia umuhimu wa amani katika maisha ya mwanadamu, hasa wakati huu anapokabiliana na changamoto mbali mbali za kihistoria.

Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Rais Sergio Mattarella wa Italia kwenda kwa Dr. Maria Voce, Rais wa chama cha kitume cha Wafokolari katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 20 tangu UNESCO ilipotoa tuzo ya amani kwa Mama Chiara Lubich. Rais Mattarella anakaza kusema, ujenzi wa amani ni kati ya dhamana nyeti inayopaswa kuvaliwa njuga na familia nzima ya binadamu. Amani inatembea kati ya mipaka ya vita, migogoro na kinzani; vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kidini na kiimani!

Amani ni fadhila inayorutubishwa kwa njia haki jamii, heshima na maridhiano ya kijamii; kwa kuthamini na kuheshimu tofauti msingi zilizopo; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kudumisha ushirikiano kati ya mataifa; kwa kukoleza na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene bila kusahau sera na mikakati ya uchumi shirikishi inayopania kukuza na kudumisha ukuaji wa uchumi ili kupambana na umaskini pamoja na utumwa mamboleo. Amani inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko; inahitaji ari na moyo wa majadiliano na udugu kwa kuwasukuma watu wote kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa amani.

Kumbu kumbu hii imefanyika kwenye Makao makuu ya UNESCO mjini Paris, Ufaransa, Jumanne, tarehe 15 Novemba 2016.  Ni matumaini ya Rais Sergio Mattarella kwamba, kongamano hili litasaidia kuchangia mchakato wa ukuaji wa amani, umoja, upendo na mshikamano Barani Ulaya, ili kuweza kuchangia katika kuleta uwiano bora zaidi duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.