2016-11-14 09:46:00

Endelezeni ari na moyo wa huruma na mapendo kama Wasamaria wema


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanafungwa rasmi kwa Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: hapo tarehe 20 Novemba 2016. Hii itakuwa ni siku ya furaha na shukrani kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwa kulijalia Kanisa kipindi cha neema na baraka. Ni siku ya kumkabidhi Kristo Yesu, maisha na utume wa Kanisa na ulimwengu mzima, ili kila mtu ajitahidi kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Jumapili tarehe 13 Novemba 2016, Malango ya huruma ya Mungu kwenye Makanisa makuu na Madhabahu yamefungwa rasmi. Kardinali Agostino Vallin, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amefunga lango la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano. Katika mahubiri yake, amewataka waamini kutafakari mambo ya nyakati kwa kuwa macho dhidi ya manabii wa uwongo; majanga asilia, vita na kinzani; dhuluma na mauaji; matunda ya dhambi za wanadamu.

Katika mazingira katika haya, waamini wanahimizwa kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hatima na mustakabali wa maisha ya mwanadamu uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma wa Baba, mwaliko kwa kujiaminisha kwake ili kuchota mwanga, utulivu na amani, ili kukutana na Baba mwenye huruma katika maisha. Jubilei ya huruma ya Mungu umekuwa ni muda uliokubalika kwa waamini kushuhudia imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, mwaliko wa kuendelea kumwilisha huruma hii katika uhalisia wa maisha ya watu.

Huruma ya Mungu ni mahali ambapo waamini wanakimbilia kuonja upendo wa Baba wa milele anayeganga na kuponya madonda ya udhaifu wa binadamu; anawasimamisha wale walioteleza na kuanguka, ili kuwategemeza katika kutenda mema. Huruma ya Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa kwani inafumbata; upendo, huruma, rehema na msamaha. Ikiwa kama waamini wanatembea katika jicho la huruma ya Mungu, wataweza kuwa ni chemchemi ya furaha kwani historia nzima ya wokovu inafumbatwa katika huruma ya Mungu.

Yesu mwenyewe aliifunua huruma hii kwa wagonjwa, maskini, wadhambi na wale wote waliokuwa wanatengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Fumbo la Pasaka ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma ya Mungu kwa mwanadamu! Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu umekuwa ni muda muafaka wa kumwilisha imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kuwaonjesha wengine furaha, faraja, huruma ili hatimaye,  kuweza kujichotea msamaha unaobubujika kutoka kwa Mungu.

Kardinali Vallin anawataka waamini kujenga na kuimarisha ndani mwao subira, huruma, upendo na msamaha kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma. Waamini wanapopokea huruma ya Mungu, wawe na ujasiri pia wa kuwaonjesha jirani zao upendo na huruma ya Mungu, kwa kuwarejeshea tena utu wao uliochakaa kutokana na dhambi kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu anayesimuliwa kwenye Injili. Huruma ni fadhila ambayo imewekwa mikononi mwa Wakristo, licha ya udhaifu wao wa kibinadamu,  ili kuwakirimia amani na utulivu wa moyo. Huruma inakuwa ni dira na mwelekeo wa maisha ya waamini kama ushuhuda wa imani tendaji!

Kama hazina ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wanahamaishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba wanaonesha upendo na ukarimu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama alivyofanya Msamaria mwema. Waamini washirikiane na Mashirika ya Misaada ya Kanisa katika kuganga na kuponya majeraha ya binadamu kwa mafuta ya faraja na mshikamano kadiri ya uwezo na nafasi ya kila mwamini, bila kuwageuzia maskini na wale wanaoteseka kisogo. Kardinali Agostino Vallin, mwishoni anawataka waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa urafiki na udugu ili kuvunjilia mbali kuta za ubaguzi na utengano; mambo amabayo kimsingi ni kichaka cha unafiki kinachoficha ubinafsi. Watu wajenge utamaduni wa upendo na kuishi katika misingi ya haki katika mahusiano ya kijamii, ili kujenga na kudumisha mafungamano kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.