2016-11-14 08:00:00

Amani ya kudumu ni changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa


Harakati za utunzaji amani, mapatano na bidii katika kujenga amani vimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuzuia machafuko na magomvi yanayosababishwa na tamaa na aina mbalimbali za ubinafsi. Maneno haya ya Askofu Mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, akichangia hoja juu ya harakati za udumishaji amani duniani, ameikumbusha dunia wito wa Baba Mtakatifu Francisko katika mkutano wa kawaida wa Umoja wa Mataifa mwezi September 2015, kwamba urejeshaji amani katika baadhi ya nchi, ni kati ya mafanikio ambayo Jumuiya ya Kimataifa inafaa kujivunia kwa kiasi fulani.

Pamoja na mafanikio yote hayo, juhudi za makusudi bado zinahitajika ili kuhakikisha kwamba suala la utunzaji amani linaweka kipaumbele ulinzi wa raia. Takwimu zinaonesha kwamba, kwa vita vya karne ya 20, ni asilimia tano tu ya vifo na majeruhi walikuwa ni raia wasio na hatia, wakati kwa karne hii ya ishirini na moja, asilimia tisini ya wahanga wa vita ni raia, wala sio wapiganaji. Kwa bahati mbaya zaidi hali ya namna hii inaongezeka siku hadi siku ambapo raia wengi wasio na hatia wanauwawa na kujeruhika, wanalazimika kukimbia makazi yao. Miji, barabara, hospitali, maeneo ya uzalishaji mazao; mashule na huduma zote za msingi vinaharibiwa vibaya, tena kwa makusudi wakati wa vita na machafuko, anasema Askofu mkuu Auza. Raia wasio na hatia, ndiyo wanaotumika kama silaha za vita, badala ya kulindwa.

Kwa namna ya pekee, wanawake na watoto wamekuwa wahanga wakubwa zaidi wa vita. Kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, vita inahusisha uhalifu mwingine mbaya wa ubakaji na unyanyasaji kijinsia, vinavyomuathiri sana mwanamke kimwili, kiroho na kimahusiano katika jamii kwa ujumla. Juhudi za kuwalinda wanawake, ziendelee sambamba na juhudi za kuwapa nafasi kushiriki katika ujenzi wa amani duniani. Wajibu wa kulinda raia wasio na hatia na kuepuka vita na machafuko, kwanza kabisa unawaangukia viongozi wa Mataifa, na ni muhimu Jumuiya ya Kimataifa kuhimiza wajibu huo kutekelezwa., vinginevyo mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa yataporomoka na kuwa kazi bure.

Kanisa Katoliki linapoendelea kuweka juhudi kutetea kanuni ya ulindaji wa raia wasio na hatia, linatambua pia kuwa sio rahisi kwa Mataifa kuzingatia hilo, hasa kwa sababu ya baadhi ya kanuni za Jumuiya ya Kimataifa, zinazoheshimu Mamlaka ya kila Taifa. Hata hivyo palipo na uonevu mkubwa na uvunjaji wa haki za binadamu, kanuni hizo hizo zinaruhusu kuingilia kati ili kulinda haki za binadamu katika Taifa husika. Kufuatia uhalisia huo, Askofu mkuu Auza amealika Jumuiya ya Kimataifa kutafakari na kuchanganua upya kanuni hizo na kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha raia wasio na hatia wanalindwa dhidi ya vita na machafuko, katika harakati za kudumisha amani na haki duniani.

Udhibiti wa silaha ni moja ya nyenzo msingi katika kuepuka migogoro ya machafuko na kulinda raia. Kwa sababu hiyo Kanisa linasisitiza udhibiti mkubwa zaidi wa utengenezaji na biashara holela ya silaha hasa katika maeneo yaliyo dhaifu zaidi kuanguka katika machafuko. Kanisa linaendelea kujiweka mstari wa mbele kushiriki kikamilifu ili kuzuia migogoro, machafuko, na kudumisha amani mahali popote panapokuwa na uhitaji huo.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.