2016-11-13 09:41:00

Salam na pongezi kutoka kwa Viongozi wa Makanisa kwa Rais Trump!


Kufuatia kuchaguliwa kwa Rais wa Marekani, Bwana Donald Trump, Baraza la Maaskofu nchini humo, wanampokea yeye aliye chaguo la Marekani wengi na kuwaalika wote sasa kujikita katika utendaji kazi kwa ajili ya mafao ya wengi, kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko alivyowakumbusha Wamarekani wote alipowatembelea mwaka jana 2015 akisema: shughuli yeyote ya siasa, lazima ihudumie na kutetea manufaa ya mwanadamu, ikizingatia heshima kwa utu wa kila mmoja. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, linampongeza Rais mteule Donald Trump kwa kuchaguliwa kwake, na linawaalika wahusika wote kuachana na tofauti na mgawanyiko waliokuwa nao wakati wa kampeni za uchaguzi, ili waanze kuiongoza nchi yao kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya raia wote wa Marekani.

Askofu mkuu Joseph Edward Kurtz wa Louisville na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu nchini Marekani anasema: mamilioni ya wamarekani wanaohangaika kutafuta fursa za uchumi kwa ajili ya familia zao, wamemchagua Donald Trump ili wasikilizwe kilio chao. Kwa sababu hiyo, jibu la viongozi wa Marekani linapaswa kuwa jepesi, nalo ni kuwasikiliza wananchi katika mahitaji na mahangaiko yao, ili waweze kuwahudumia vyema. Mchango katika uimarishaji wa familia, ni wajibu wa kila mmoja. Hivyo, Baraza la Maaskofu litakuwa tayari kushirikiana na Rais mteule, Donald Trump, kwanza kabisa kwenye kulinda zawadi ya maisha ya mwanadamu, tangu hali nyonge ya kutungwa mimba mpaka mwihso wake wa asili, amesisitiza Askofu mkuu Joseph Kurtz.

Pamoja na ulinzi na utetezi wa uhai, Maaskofu wataunga mkono siasa na sera zitakazotoa fursa kwa watu wote wa dini na imani mbali mbali, wenye asilia yeyote na wa makundi yote katika jamii. Kwa msimamo huo, Maaskofu nchini Marekani wanaamini kwamba, wahamiaji na wakimbizi watapokelewa kwa utu, bila kuhatarisha usalama wa nchi yao. Maaskofu wamewakumbuka ndugu zao wanaoteswa na kunyanyaswa sababu ya imani zao katika mataifa kadhaa, hasa Mashariki ya kati. Wanaalika kuwekwa kwa mikakati, nguvu ya pamoja na ushirikiano ili kuhakikisha kunapatikana uhuru wa kuabudu kila mahali duniani, na kwamba kila mwanadamu anapewa uhuru wa kuishi ukweli wa maisha na uhalisia wa mwanamke na mwanaume, ikiwa ni pamoja na tunu ya ndoa moja na asilia inayofaa kufungwa maishani.

Kila uchaguzi huwa ni ishara ya mwanzo mpya. Kwa nchi ya Marekani, wengi wanajihoji kama inawezekana kupatana, kuponya majeraha ya wakati wa kampeni, na kuungana tena ili kutenda kazi kwa pamoja kwa manufaa ya wote. Askofu mkuu Joseph Kurtz anasema: Kristo atawatia nguvu ya upatano, uponyaji na kuungana tena kwa lengo moja la kuijenga nchi yao.

Mwaliko kwa Wakristo: kushinda changamoto zinazowakabili na kuendelea kutafuta amani na mshikamano, unatolewa pia na Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa ulimwenguni, Dr. Olav Fykse Tveit, ambaye dakika chache baada ya uchaguzi alitupia ujumbe kwenye ukurasa wa twitter kwamba: kampeni za Urais nchini Marekani zimefikia tamati. Lakini hija ya haki na amani inaendelea, tena sasa hivi ni kwa ari zaidi.

Katika mtandao wa twitter, Justin Welby, Askofu mkuu wa Canterbury na kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani katupia sala akiomba kwamba: wakati Rais mteule Donald Trump anajiandaa kuapishwa, ataendelea kuombea nchi ya Marekani ili ipate kujipatanisha baada ya kampeni za maumivu, na ili Donald Trump apate neema ya hekima na busara kwa kazi iliyo mbele yake. Salamu za pongezi zimetolewa pia na Patriaki Cyril, wa Kanisa la Kiorthodox la  Mosco, aliyesisitiza kutilia maanani nafasi ya Marekani katika kupambana na itikadi kali na ugaidi kimataifa na katika kulinda na kutetea haki na utu wa mwanadamu.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.