2016-11-13 08:59:00

Mshikamano wa Kanisa kwa watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi Italia


Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, Ijumaa tarehe 11 Novemba 2016 ametembelea mji wa Norcia, Italia ambao hivi karibuni umekumbwa na mfululizo wa matetemeko ili kujionea mwenyewe janga lililosababishwa na tetemeko hili katika maisha ya watu, miundo mbinu na majengo ya ibada na huduma za kijamii. Katika ziara hii ya kikazi, Kardinali Tagle alikuwa amefuatana na Askofu mkuu Renato Boccardo wa Jimbo kuu la Norcia pamoja na viongozi wengine wa Shirika la Misaadala Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Norcia.

Kardinali Tagle akiwa katika eneo ambalo limeathirika sana na matetemeko haya, alipata nafasi ya kusali katika ukimya kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu pamoja na Kanisa kuu la Mtakatifu Benedikto. Kardinali Tagle kwa niaba ya Caritas Internationalis ametoa salam zake za rambi rambi, upendo na mshikamano kwa wananchi wote walioguswa na kutikiswa na majanga haya asilia. Majengo, makazi na nyumba nyingi za Ibada zimebomoka kiasi cha kuwakatisha watu moyo wa kusonga mbele.

Katika mazingira kama haya, Kanisa linawahamasisha viongozi wake kujizatiti katika ujenzi wa matumaini, mapendo na mshikamano na waamini wote, ili kuanza tena kwa ari na moyo mkuu ujenzi wa makazi yao kwa imani na matumaini. Kardinali Tagle amekutana na kuzungumza pia na viongozi wa mji wa Norcia pamoja na Askari wa Kikosi cha Zima moto wanaoendelea kutoa huduma makini kwa waathirika wa matetemeko haya pamoja na kulinda usalama wa mali na majengo yaliyobomoka kutokana na tetemeko la ardhi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.