2016-11-13 12:05:00

Jiandaeni kwa imani na matumaini kwa ajili ya Siku ya Hukumu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Jubilei ya maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kiini cha Injili, amana na utajiri wa Kanisa, Jumapili, tarehe 13 Novemba 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, amewakumbusha waamini kwamba, Injili ya jumapili ya XXXIII ya Mwaka C wa Kanisa inajikita katika mambo ya nyakati, Siku ya hukumu, mambo yote yatakapotoweka.

Huu ni mwaliko wa kuwa na matumaini kwani hata wakati mwingine, waamini wanakumbwa na wasi wasi kutokana na shida na magumu wanayokabiliana nayo, lakini yote haya kwa neema na baraka za Mungu yanapita na kutoweka kama ndoto ya mchana! Yesu anawaonya wafuasi wake, wasijiaminishe sana na usalama wa ambo ya kidunia, wawe pia macho na wahubiri wa uwongo wanaotaka kuwatisha watu kwa: vita, matetemeko ya ardhi na mapinduzi kwani yote haya ni sehemu ya mambo ya dunia.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, historia na maisha ya Kanisa yamesheheni watu jasiri waliosimama kidete kukabiliana na changamoto za maisha kama vile dhuluma na mahangaiko mbali mbali, lakini imani na matumaini yao, yaliwawezesha kuwa na moyo wa subira. Mwenyezi Mungu ni mwaminifu na mwangalifu na kamwe hawezi kuwaacha watoto wake. Hii ni changamoto ya kujikita kwa Mungu, kutembea katika mwanga wa matumaini na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi licha ya matatizo na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza kwa mtu binafsi au katika ngazi ya jamii katika ujumla wake.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya waamini inajiandaa vyema ili kuiendea “Siku ya Bwana”. Kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ambayo kwa Jumapili, tarehe 13 Novemba 2016 Makanisa makuu na Madhabahu ya huruma ya Mungu yamefunga malango ya huruma ya Mungu, changamoto ni kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu pamoja na kujikita katika Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani tendaji, ili watu wote waweze kupata wokovu.

Waamini wafahamu kwamba, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuiongoza historia na anatambua hatima ya kila jambo na kila tukio. Kwa mwanga wa huruma na upendo wa Mungu, mwamini anaweza kuona historia ya wema na ubaya; mambo ambayo yemehifadhiwa yote ndani mwake na kwamba, hata maisha ya mwanadamu yako mikononi mwake na kamwe hayawezi kupotea na kutoweka kabisa! Bikira Maria, awasaidie waamini kuwa na matumaini ya maisha ya uzima wa milele hata katika matukio ya kusikitisha.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu amewaambia waamini kwamba, baada ya ukarabati mkubwa, Msalaba wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro umerejeshwa tena mahali pake kwa ajili ya ibada kwa waamini na kwamba, huu utakuwa ni kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na utawekwa kwenye Kikanisa cha Sakramenti kuu.

Baba Mtakatifu ameungana pia na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kusherehekea Siku ya Shukrani Kitaifa kwa mazao ya nchi na kazi ya mikono ya wanadamu, changamoto na mwaliko wa kuwa na matumizi endelevu ya ardhi. Kanisa liko sanjari na wakulima na linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka watu wanaoteseka kwa baa la njaa na ukame wa kutisha. Amewashukuru waamini wote waliojisadaka kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wakati wa maadhimisho ya Jubilei yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.