Ifuatayo ni Hotuba ya Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (MB), Waziri mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania wakati wa kuahirisha mkutano wa tano wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa tanzania Tarehe 11 novemba, 2016. Amezungumzia kuhusu shughuli za Bunge,
maazimio, maafa mkoani Kagera, mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya taifa kwa mwaka
2017/2018; uwekezaji pamoja na taarifa kutoka katika sekta mbali mbali. Sasa unaweza
kuendelea kujihabarisha zaidi na hotuba hiyo!
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba kutumia fursa hii kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutufikisha salama siku ya leo tunapohitimisha Mkutano
wa Tano wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 1 Novemba, 2016.
- Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kukupa pole,
kwa msiba mzito uliotokea tarehe 7 Novemba, 2016 ambao Bunge lako tukufu, Serikali
na Taifa tumepata kwa kumpoteza Mheshimiwa Samwel Sitta, mmoja wa Viongozi mahiri
wa Bunge hili katika historia ya nchi yetu. Msiba uliotupata wa aliyekuwa Spika Mstaafu
wa Bunge la Tisa (2005-2010) na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo Mkoani Tabora ni
pigo kwa Taifa letu. Nasi Wabunge kwa kuwawakilisha Watanzania leo hii muda mfupi
ujao tutaaga mwili wa kipenzi chetu Mheshimiwa Samuel Sitta. Tunamwomba Mwenyezi
Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema Peponi. Amina.
- Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa pole
kwa mjane wa marehemu, Mheshimiwa Margareth Simwanza Sitta, Mbunge mwenzetu, watoto
wake na wanafamilia wote na marafiki wote kwa ujumla kutokana na msiba mzito uliowapata.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na siku
zote wamtangulize Mwenyezi Mungu katika kuwaongoza wanafamilia waliobakia.
Sina budi kukiri kuwa Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika
uongozi na maendeleo. Enzi za uhai wake, Marehemu Mheshimiwa Sitta, alibahatika kufanya
kazi na Marais wa awamu zote nne zilizopita tangu ya kwanza ya Hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, akiwa Mbunge kwa miaka 30. Alikuwa ni Spika wa Bunge la Tisa
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja
na Mkuu wa Mikoa ya Iringa na Kilimanjaro, Waziri wa Ujenzi, Waziri aliyesimamia Ustawishaji
Makao Makuu, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Afrika Mashariki, Waziri wa Uchukuzi
na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.
- Mheshimiwa Spika, tarehe 8 Novemba, 2016 tumeondokewa
tena na Kiongozi wa muda mrefu Serikalini Ndugu Joseph Mungai. Kiongozi huyu ameshika
nafasi mbalimbali katika utumishi wa umma ikiwemo Ubunge na Uwaziri.
- Mheshimiwa Spika, tangu tulipokutana mara ya mwisho,
pametokea majanga mbalimbali yakiwemo maradhi, ajali, na matukio mengine ambayo yamesababisha
vifo na majeruhi kwa Watanzania wenzetu. Sote tunakumbuka tukio la kusikitisha la
watumishi wa Serikali waliopoteza maisha wakiwa kazini walipovamiwa na wanakijiji
wa Makang’wa wilayani Chamwino mkoani Dodoma. Nalaani mauaji hayo na kuvitaka vyombo
vya usalama kuwachukulia hatua wote waliohusika. Vilevile, katika miezi ya Oktoba
na Novemba, kumetokea ajali za barabarani katika Mikoa ya Mbeya, Pwani, Singida, Lindi,
Iringa, na ile iliyopoteza ndugu zetu 19 mkoani Shinyanga na kwingineko ambako ndugu
zetu walipoteza maisha. Ninatoa pole kwa wafiwa wote na wale wote waliopatwa na majanga
kutokana na matukio hayo. Tunawaombea afya njema wale waliopata majeraha na waliopo
hospitali. Pia niendelee kuwataka Askari wa usalama barabarani kuhakikisha wanasimamia
madereva na watumiaji wa Barabara kuzingatia Sheria za usalama wa barabarani.
- Mheshimiwa Spika, leo tunahitimisha Mkutano huu wa
Tano tukiwa tumekamilisha shughuli zote zilizopangwa. Naomba nitumie fursa hii kukupongeza
wewe Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge na Waheshimiwa
Wabunge wote kwa kukamilisha kazi zote kwa ufanisi mkubwa. Nawapongeza sana!
SHUGHULI ZA BUNGE
- Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu tumepata fursa
ya kujadili, kupokea na kushauri kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa
unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na muongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti
ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, katika kipindi hiki, tumejadili Hoja
mbalimbali za Serikali ikiwemo Miswada, Taarifa za Kamati, Mkataba wa EPA, Maazimio
na Kauli mbalimbali za Mawaziri. Vilevile, Wabunge walipata majibu ya maswali mbalimbali
ya msingi na ya nyongeza yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wabunge na maswali ya Papo kwa
Papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
- Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumshukuru
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na Wataalam wake, kwa kazi kubwa ya kuandaa miswada
mbalimbali iliyowasilishwa katika Bunge lako Tukufu. Aidha, napenda kutumia fursa
hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri. Serikali itazingatia
ushauri na maoni yenu wakati wa utekelezaji.
-
- Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu, Waheshimiwa
Wabunge wamepata fursa ya kupokea na kujadili Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya yaani East Africa Community –
European Union Economic Partnership Agreement. Napenda kuwashukuru Waheshimiwa
Wabunge wote kwa michango yenu mizuri tuliyoipata wakati wa mjadala wa Mkataba huo.
Serikali itafanyia kazi maoni, ushauri na uamuzi wenu kuhusu Mkataba huo.
JUHUDI ZA SERIKALI ZA KUWAHUDUMIA WAATHIRIKA WA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI
KAGERA
- Mheshimiwa Spika, mtakumbuka kuwa mnamo tarehe 10
Septemba, 2016 lilitokea tetemeko la ardhi katika eneo la Kanda ya Ziwa na
hususan Mkoa wa Kagera. Tetemeko hilo lilisababisha athari mbalimbali zikiwemo vifo,
majeruhi, uharibifu wa makazi na miundombinu ya umma na watu binafsi. Jumla ya Watu
117,721 wameathirika kwa kupoteza makazi yao, mali na athari za kisaikolojia
katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa. Aidha, jumla ya watu
17 walipoteza maisha na 560 walijeruhiwa. Vilevile,
nyumba 2,072 za makazi zilianguka kabisa na nyumba 14,595 za makazi zilibomoka, baadhi
zina kuta au kupata nyufa kubwa na hivyo kuzifanya kuwa hatarishi kwa makazi ya binadamu.
Vilevile, maafa haya yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na majengo
ya Serikali 1,718 yaliyoharibika kwa viwango tofauti.
- Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, Serikali ilianzisha
Kituo cha Operesheni na Kuratibu Maafa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Kagera kwa lengo la kuharakisha huduma. Aidha, Serikali ilitoa matibabu bure kwa
majeruhi wote, kuandaa na kugharamia mazishi ya watu 17 waliofariki
ambapo mimi binafsi nilihudhuria na pia kutoa mkono wa pole wa Shilingi Milioni
17 kwa wafiwa. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali iliwahudumia
wananchi walioathirika na tetemeko kwa kuwapatia misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula,
madawa, nguo, makazi ya muda, vifaa vya ujenzi, vifaa tiba, vifaa vya shule na huduma
ya ushauri wa kisaikolojia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwakilishi
Mkazi wa Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali walifanya Tathmini ya pamoja ya mahitaji
ya haraka katika kukabiliana na Athari za Tetemeko hilo. Ambapo utekelezaji wa masuala
muhimu yaliyoainishwa katika tathmini hiyo unaendelea.
- Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha wadau, taasisi na
wananchi mbalimbali kuchangia maafa hayo, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na
Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Kagera ilifungua Akaunti pekee
Namba 0152225617300 katika Benki ya CRDB Bukoba yenye jina la “KAMATI
MAAFA KAGERA”. Hadi kufikia tarehe 10 Novemba, 2016 kiasi
cha Shilingi 5,427,671,677.32 kilikuwa kimeingizwa kwenye Akaunti hiyo. Hadi
kufikia tarehe 10 Novemba 2016 Salio katika Benki ni Shilingi 4,296,038,711.79 na
matumizi hadi tarehe tajwa yalikuwa ni Shilingi 1,130,428,347.53. Aidha,
Kamati pia ilisajili namba za simu za mkononi za kupokea michango katika Kampuni za
Vodacom (M-Pesa) 0768 196 669, Tigo (Tigopesa) 0718 069 616
na Airtel (Airtel Money) 0682 950 009 kwa jina la “KAMATI
MAAFA KAGERA”. Hadi kufikia tarehe 10 Novemba, 2016, kiasi
cha Shilingi 16,638,747 kilichangwa kupitia mitandao
hiyo ya simu. Hivyo kufanya jumla ya fedha zilizopokelewa kupitia Benki na Mitandao
ya Simu kuwa Shilingi 5,444,310,424.32. Aidha, Serikali imechangia
Shilingi Billioni Moja katika kukabili janga hilo.
- Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupokea
misaada kutoka kwa Washirika wetu wa Maendeleo, Balozi na hata Nchi marafiki. Mathalan,
tumepokea kutoka Serikali ya Uganda Dola za Kimarekani 200,000 sawa
na Shilingi Milioni 419.2, Serikali ya India Shilingi Milioni
547, Serikali ya Kuwait Shilingi Milioni 51 na Serikali
ya Uingereza iliahidi kutoa Shilingi Bilioni Sita zitakazoelekezwa
kwenye ujenzi wa shule.
- Mheshimiwa Spika, tumepokea vifaa mbalimbali vyenye
thamani ya zaidi ya shilingi milioni 357 yakiwemo maturubai, magodoro, ndoo, mashuka,
vifaa tiba, dawa na chakula kutoka Serikali za Japan, China, Kenya, Pakistan, Burundi
na Rwanda.
- Mheshimiwa Spika, taarifa ya Kikosi Kazi cha Wataalam
imeainisha kuwa takribani Shilingi Bilioni 63.2 zitahitajika kurejesha
hali ya kawaida katika Mkoa wa Kagera kufuatia maafa hayo. Gharama hii inajumuisha
ukarabati wa shule za msingi, sekondari, vituo vya afya na taasisi nyingine katika
wilaya zote sita za Mkoa huo, ujenzi mpya wa shule za Ihungo na Nyakato (tayari wafadhili
wamejitolea kujenga shule hizi). Aidha, hadi kufikia tarehe 10 Novemba, 2016
kiasi cha Shilingi 966,898,826 zilitumika katika kufanya ukarabati
mkubwa na mdogo wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Zahanati katika Halmashauri
za Mkoa wa Kagera. Serikali inaendelea na ujenzi wa Zahanati mpya (Ishozi) inayojumuisha
chumba cha Upasuaji na wodi ya kinamama na watoto na usimamizi wa ujenzi wa shule
za Ihungo na Nyakato. Aidha, katika kuongeza nguvu ya urejeshaji hali jumla ya Askari
96 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakiwemo Wahandisi, Mafundi, Wapishi, na Madereva
waliwasili Mkoani Kagera tarehe 19 Oktoba, 2016 kushiriki katika
zoezi la kurejesha hali ya majengo na miundombinu.
- Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kulihakikishia
Bunge lako Tukufu na wananchi kwa jumla kuwa Serikali ipo pamoja na waathirika hawa
katika suala hili na ina mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunarejesha hali bora kwa
kuendelea kurudisha miundombinu, kutoa huduma za kibinadamu na matibabu kwa waathirika.
Aidha, napenda kuwashukuru wale wote waliochangia katika kusaidia wenzetu wa Kagera,
kwani katika kipindi hiki, tumeonesha umoja wetu, upendo wa dhati, hali ya kuthaminiana
na kujaliana. Mungu awabariki sana na kuwaongezea pale walipotoa. Kipekee, niwashukuru
Nchi marafiki, Balozi, Wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya Nchi, Taasisi za Kiserikali
na zisizo za Kiserikali, Taasisi za Fedha, Kampuni, Vikundi mbalimbali, pamoja na
Wananchi wote wakiwemo wale waishio nje ya Nchi.
MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2017/2018
- Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa tano wa Bunge,
Serikali imewasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018.
Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri
iliyotolewa wakati wa kujadili Hoja hiyo. Maoni na ushauri uliotolewa utazingatiwa
wakati wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/2018.
TAARIFA ZA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE ZA PAC NA LAAC KUHUSU HESABU ZILIZOKAGULIWA
KWA MWAKA 2013/2014 NA 2014/2015
- Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Waheshimiwa
Wabunge wamepata fursa ya kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali na Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge za PAC na LAAC kuhusu Hesabu za Serikali
Kuu, Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa zilizokaguliwa kwa mwaka ulioishia tarehe
30 Juni, 2014 na tarehe 30 Juni, 2015. Serikali imepokea michango na Hoja za Waheshimiwa
Wabunge na itazifanyia kazi.
- Mheshimiwa Spika, napenda kuwakumbusha Waheshimiwa
Wabunge kwamba kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2016, Serikali
imetakiwa kuchukua hatua kali na za haraka kwa wale wote watakaobainika kujihusisha
na ubadhirifu
na wizi wa mali ya umma, ukiukaji wa maadili ya Utumishi wa Umma na wale wanaoendeleza
vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za Umma. Kutokana na maelekezo hayo,
Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Serikali na
kuchukua hatua kwa Watumishi wa Umma wasiozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za matumizi
ya Fedha za Umma. Maafisa Masuuli wote wanakumbushwa kuzingatia kikamilifu Sheria
ya Ununuzi wa Umma na Kanuni zake. Aidha, Maafisa Masuuli wote wanatakiwa kuchukua
hatua stahiki za kinidhamu na kisheria kwa Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi za Serikali
wanaofanya malipo yenye mashaka wakati wa kufanya manunuzi ya Umma au kuingia Mikataba
na Zabuni tata za utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hatua hizo zitapunguza na kuondoa
Hoja za ukaguzi na kuimarisha usimamizi wa fedha za walipa kodi.
SEKTA YA KILIMO
Mwenendo wa Uzalishaji wa Mazao Katika Msimu wa Mvua za Vuli
- Mheshimiwa Spika, naomba nitoe taarifa kutoka Mamlaka
ya Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa, kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2016 imeonesha
kuwa katika maeneo mengi ya nchi, mvua zinatarajiwa kuwa chache, kuchelewa kuanza
na mahali pengine kunyesha kwa mtawanyiko usioridhisha. Aidha, kwa maeneo yanayopata
mvua za vuli zikiwemo Wilaya za Kyerwa, Missenyi na Karagwe, mvua zilipoanza kunyesha
zilikuwa chini ya wastani na kusababisha baadhi ya mazao yaliyopandwa kuathirika.
Vile vile, taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA zinaeleza kuwa katika maeneo yanayopata
msimu mmoja wa mvua zinazoanza mwezi Novemba hadi Aprili, mvua zitachelewa na kunyesha
chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi isipokuwa katika baadhi ya maeneo
ya Mtwara Lindi na Ruvuma. Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwataka wataalam
wa kilimo kuhakikisha wananchi katika maeneo yatakayopata mvua kidogo wanawezeshwa
kupata mbegu za mazao yanayostahimili ukame na zinazokomaa haraka.
Aidha, niwashauri wakulima kuandaa mashamba yao mapema na kutumia mbegu hizo zinazokomaa
mapema na kustahimili ukame. Niwasihi wananchi na wakulima kuendelea kutumia kwa uangalifu
na kuhifadhi akiba ya chakula walichovuna au kununua kwa matumizi katika kaya zao.
Nitoe wito kwa Sekta binafsi kuendelea kushiriki katika kutoa masoko ya kununua na
kuuza mazao katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba.
Usambazaji wa Pembejeo za Zao laTumbaku
- Mheshimiwa Spika, ili kuondoa kero ya upatikanaji
wa pembejeo kwa zao la tumbaku kwa msimu wa 2016/2017, Serikali imebadili utaratibu
kutoka ule uliohusisha zabuni kwa wauzaji wa kati (middlemen) na kuweka utaratibu
mpya unaohusisha wazalishaji wa pembejeo kuzisafirisha pembejeo hizo hadi katika Vyama
vya Msingi vya Ushirika moja kwa moja kwa bei ya Dola za Kimarekani 40.45
kwa mfuko wa NPK (ikilinganishwa na Dola za Kimarekani 52.7 za msimu
uliopita), na Dola za Kimarekani 21 pungufu kwa mbolea aina ya Urea
na CAN kwa tani moja ukilinganisha uliopita. Hadi sasa wazalishaji wawili wa mbolea
za tumbaku (Kampuni ya Yara Tanzania na Rosier) wamechukua jukumu hilo. Napenda kuchukua
fursa hii kuvitaka Vyama vya Ushirika kusimamia kikamilifu mpango huu ili wakulima
wazalishe kitaalamu na kuongeza tija katika uzalishaji.
SEKTA YA VIWANDA NA UWEKEZAJI
- Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 17 Oktoba, 2016, Mheshimiwa
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji alizindua rasmi matokeo ya Sensa ya Uzalishaji
Viwandani ya mwaka 2013 iliyofanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Viwanda, Biashara
na Uwekezaji na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Zoezi la sensa hii lilitumia taarifa
za uzalishaji za viwanda za mwaka, 2013, yaani viwanda vilivyokuwepo mwaka 2013 na
vilivyokuwa vinazalisha. Zoezi la ukusanyaji wa taarifa za uzalishaji, za viwanda
lilifanyika mwaka 2014 na mwaka 2015 ilikuwa ni kufanya uchambuzi wa kitalaamu na
kuandika ripoti.
- Mheshimiwa Spika, matokeo ya Sensa hiyo yanaonesha
kuwa, kufikia mwaka 2013 Tanzania ilikuwa na jumla ya viwanda 49,243 ambapo viwanda
vidogo vinavyoajiri mtu 1 – 4 vilikuwa ni Asilimia 85.13, viwanda vidogo vyenye watu
5 - 49 ni Asilimia 14.02, viwanda vya kati vyenye watu 50 - 99 ni Asilimia 0.35 na
viwanda vikubwa vyenye watu kuanzia 100 na kuendelea ni Asilimia 0.5. Hivyo, Asilimia
99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo.
- Mheshimiwa Spika, katika utafiti wa mwaka jana ilionekana
kuwa mpaka mwezi Oktoba, 2015 kulikuwa na viwanda 52,579. Aidha, kwa kipindi cha mwaka
mmoja tu, yaani kuanzia Novemba, 2015 mpaka Oktoba, 2016 jumla ya viwanda vipya 1,843
vimeanzishwa na kufanya jumla ya viwanda vyote nchini kufikia 54,422.
Ni matumaini ya Serikali kuwa kutokana na juhudi za uhamasishaji zinazofanyika, kasi
ya uanzishwaji viwanda na hasa viwanda vidogo na vya kati na vikubwa itaongezeka sana.
- Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara mbalimbali
za Kisekta tayari imebainisha maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchochea uwekezaji
kama vile kuendeleza eneo la Mji wa Kigamboni na kutenga maeneo maalum ya Uwekezaji
katika Mikoa mbalimbali Nchini. Hatua nyingine ni kuboresha miundombinu kama vile
barabara na reli. Mfano mzuri ni ujenzi wa reli yenye urefu wa kilomita 4 katika kiwanda
kipya cha KILUA GROUP cha kutengeneza nondo kilichopo Mlandizi, Pwani. Pia, Serikali
inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika. Kwa viwanda ambavyo vipo karibu
na bomba la gesi watasaidiwa kuunganishwa na gesi. Vilevile, Serikali, imechukua hatua
madhubuti za kuharakisha upatikanaji wa ardhi ambacho ni kivutio muhimu katika kuhamasisha
uwekezaji.
Uongezaji Kasi ya Uwekezaji kwenye Sekta ya Viwanda Nchini
- Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati madhubuti
ya kuhakikisha kasi ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda inaongezeka ili ichangie
Asilimia 15 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2020 Ili kutekeleza adhima hiyo hatua zifuatazo
zinaendelea kuchukuliwa:-
Kwanza: Kutambua sekta za kipaumbele
kwa kuzingatia viwanda vinavyotumia malighafi za ndani, na hususan kwenye sekta za
kilimo na maliasili ili kuchochea uzalishaji vijiini na kuongeza ajira; viwanda vinavyotumia
malighafi za ndani ambazo si za kilimo kama vile madini na kemikali; na kuweka msukumo
kwenye kuanzisha viwanda visivyotumia malighafi za ndani kama vile uunganishaji wa
magari na uzalishaji wa vifungashio.
Pili: Kuandaa Mpango
mahsusi wa uwekezaji kwenye viwanda kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mpaka sasa,
Mifuko ya LAPF, PPF, PSPF, NSSF na GEPF tayari wameainisha miradi ya uzalishaji watakayoanza
nayo.
Tatu: Kuhamasisha Sekta
Binafsi, ya ndani na nje ya Nchi, kuwekeza kwenye viwanda. Kupitia makongamano ya
biashara na uwekezaji nchi mbali mbali zimehamasishwa kuwekeza nchini. Baadhi ya nchi
hizo ni China, Oman, Vietnman, Urusi, Morocco n.k.
Nne: Kuingia makubaliano
ya ushirikiano na Nchi zingine ili kuongeza uwekezaji. Mpaka sasa Nchi ya China imechagua
jimbo la Jiangsu kuleta viwanda nchini na pia kupitia Jukwaa la Ushirkiano la China
na Afrika itawezesha ujenzi wa miundombinu ikiwemo Bandari ya Bagamoyo. Aidha, kwa
utaratibu huu Serikali tayari imeanza utekelezaji wa mradi wa kuunganisha matrekta
2400 pale TAMCO Kibaha kufuatia ushirikiano na Serikali ya Poland, uunganishaji wa
magari wa Kampuni ya Kitanzania ya SIMBA MOTOR kwa ushirikiano na Jeshi (NYUMBU) na
Kampuni ya China. Vile vile, India kupitia mradi wake wa kuimarisha uwekezaji Afrika
(SITA) inasaidia utekelezaji wa mikakati minne ya kukuza na kuendeleza alizeti, pamba,
ngozi na mazao ya jamii ya kunde.
Tano: Kutoa elimu na mwongozo
kwa Serikali ngazi ya Mikoa na Wilaya kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika maeneo
yao. Serikali imegawa Mikoa katika makundi manane ambayo Watendaji Waandamizi wa Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji watakwenda kuzungumza na wadau ili kuhakikisha viwanda
vinasambaa Nchi nzima.
- Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hili mambo
muhimu ambayo Mikoa inatakiwa kuzingatia ni pamoja na Mikoa kuweza kubaini fursa walizonazo
na kuandaa taswira ya mkoa kutegemeana na fursa walizonazo. Aidha, Mikoa inahimizwa
kuhamasisha wananchi juu ya uwekezaji. Vilevile, Viongozi wa Mkoa wanashauriwa kuongeza
kasi ya kuhamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga maeneo na kuhakikisha kuwa
wanazingatia katika mipango ya Halmashauri za wilaya ujenzi wa miundombinu wezeshi
kwenye maeneo watakayotenga kwa ajili ya uwekezaji.
SEKTA YA ELIMU
Matokeo ya Mitihani ya Darasa la Saba 2016
- Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba, 2016 Baraza la Mitihani
la Taifa lilitangaza matokeo ya Mitihani wa Darasa la Saba kwa mwaka 2016. Taarifa
hiyo ilibainisha kuwa katika mtihani huo, kati ya wanafunzi 789,479
waliofanya mtihani, jumla ya wanafunzi 555,291 walifaulu sawa na
Asilimia 70.36. Kati yao wasichana ni 283,751 na
wavulana ni 271,540. Nitumie fursa hii kuwapongeza wanafunzi wote
waliofaulu na Shule zote zilizofanya vizuri na hasa wale kumi bora. Napenda kuwaagiza
Viongozi wa Mikoa na Halmashauri kuendelea kukamilisha miundombinu ya vyumba vya madarasa
na miundo-mbinu mingine ili kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wanaotakiwa kujiunga
na kidato cha kwanza mwezi Januari, 2017. Kila Mkoa uweke lengo la kuhakikisha Wanafunzi
wote watakaochaguliwa wanajiunga na Sekondari. Serikali kwa upande wake itahakikisha
inatoa ruzuku kwa ajili ya mahitaji ya Wanafunzi watakaojiunga na Sekondari.
Mwenendo wa utoaji wa mikopo
- Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 1994
Serikali ilipoanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu, jumla ya kiasi cha
Shilingi Trilioni 2.44 kimekwishatolewa. Jumla ya wanafunzi 324,994
wamenufaika na fedha hizo.
- Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017
jumla ya wanafunzi 64,441 wamedahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu na orodha
yao kuwasilishwa Bodi ya Mikopo ya Elimu Juu. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia tarehe 3 Novemba, 2016, wakati akitoa kauli ya Serikali
Bungeni kuhusu upangaji na utoaji wa Mikopo ya Elimu ya Juu, ni kwamba hadi kufikia
tarehe 2 Novemba, 2016 jumla ya wanafunzi 25,228
wa mwaka wa kwanza walikuwa wamekwishapewa fedha za mikopo. Kati ya wanafunzi hao,
4,787 ni Yatima, 127 wenye Ulemavu na 94
ni waliosoma Sekondari kwa Ufadhili wa Taasisi mbalimbali.
- Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa wanafunzi
wote wanaoendelea na masomo, ambao ni wanufaika wa mikopo na vyuo vyao vimewasilisha
Bodi ya Mikopo taarifa za matokeo wameendelea kupatiwa mikopo kama ilivyokuwa katika
mwaka uliopita wa masomo.
Changamoto Zilizopo za Mkopo na Utatuzi Wake
- Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto zinazojitokeza
katika uratibu wa mikopo ya wanafunzi, Serikali inafanya mapitio ya mfumo wa udahili
wa wanafunzi vyuoni, utaratibu mzima wa utoaji na urejeshwaji mikopo kwa lengo la
kuwa na mfumo bora zaidi na kuondoa adha inayowapata wanafunzi wanapofungua vyuo kutokana
na mfumo uliopo sasa. Nimeagiza kazi hii ikamilike mapema ili mapendekezo ya mfumo
utakaokuwa na tija zaidi yaweze kuzingatiwa wakati wa maandalizi ya Bajeti ya 2017/2018.
SEKTA YA ARDHI
Hali ya Migogoro baina ya Watumiaji wa Ardhi Nchini:
- Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeendelea kukumbwa na
migogoro mbalimbali ya ardhi baina ya watumiaji wa ardhi ikiwemo migogoro mikubwa
baina ya wakulima na wafugaji; migororo baina ya wananchi na wawekezaji; wafugaji
na hifadhi za Taifa na baina ya wakulima na baadhi ya maeneo ya hifadhi za Wilaya
mbalimbali.
Juhudi na Mikakati ya Serikali ya Kuondoa Migogoro Mikubwa ya Wakulima
na Wafugaji
- Mheshimiwa Spika, migogoro ya matumizi ya ardhi baina
ya Wakulima na Wafugaji imeendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la watu na mifugo,
vijiji kutokuwa na Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi inayoainisha
maeneo mahsusi kwa ajili ya Kilimo na Ufugaji. Aidha, uwepo mabadiliko
ya tabia nchi yanayosababisha ukame na ukosefu wa malisho na maji katika maeneo ya
wafugaji kumesababisha uhusiano hafifu baina ya jamii za wafugaji na wakulima kutokana
na mifugo kuingizwa katika mashamba ya wakulima kwa mabavu.
- Mheshimiwa Spika, migogoro hii imesababisha kuwepo
kwa vitendo vingi vya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha ya wananchi, baadhi ya
wananchi kupata vilema vya maisha, uharibifu wa mali, uharibifu wa mazingira, athari
za kijamii kama watoto kushindwa kwenda shule na wananchi kushindwa kushiriki katika
shughuli za maendeleo kutokana na hofu jambo linaloweza kusababisha njaa na umaskini
miongoni mwa jamii na Taifa.
Hatua za kutatua migogoro mikubwa ya wakulima na wafugaji
- Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na migogoro na
kuwawezesha wakulima na wafugaji kuendelea na shughuli zao bila migogoro, Serikali
inaendelea kutekeleza mikakati ya kuainisha, kupima, kutenga na kumilikisha ardhi
kwa ajili ya wafugaji na wakulima; na kanda za malisho kwa wafugaji wakubwa na wadogo
itakayohusisha vijiji, Wilaya na Mikoa. Maeneo haya yatakayotengwa yatalindwa kwa
kuyatangaza kwenye Gazeti la Serikali, na matumizi yake yatasimamiwa ili kuhakikisha
wanafuga kwa kuzingatia uwiano wa malisho na mifugo.
- Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kuzigawanya
Ranchi zilizopo katika vitalu ili wafugaji wenye ng’ombe zaidi ya 200 wahamie huko,
kila kitalu kimoja kulingana na uwezo wa kitaalamu wa kulisha idadi maalum ya ng’ombe.
Wafugaji wenye mifugo chini ya 200 watagawiwa maeneo katika maeneo yaliyotengwa kwa
ajili yao katika vijiji na watakuwa wanauza mifugo yao katika minada ambapo wafugaji
kutoka Ili katika ranchi watafika kununua mifugo hapo. Kwa mikoa ambayo haina Ranchi
za Taifa, watatenga maeneo yaliyo wazi kwa ajili ya wafugaji wakubwa.
- Mheshimiwa Spika, ili kuzuia wafugaji kuhamahama
kutafuta maji na huduma nyingine, Serikali kwa kushirikiana na wafugaji itaweka miundombinu
ya majosho, mabwawa ya kunyweshea maji, huduma za ugani zikiwemo matibabu, elimu ya
kulima malisho, unenepeshaji, uwekaji sahihi wa chapa za ng’ombe n.k.
- Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hizo, jawabu la
kudumu la migogoro hii ni kuhakikisha kuwa tunawawezesha wafugaji kuvuna na kupunguza
mifugo bila kupata hasara, kupitia uwekezaji wa Viwanda vya Kuchakata Nyama na Usindikaji
Maziwa ili kuongeza thamani. Wizara husika zikae pamoja na kubuni Mikakati na Mipango
ya kuvutia wawekezaji katika eneo hili katika miaka mitatu ijayo kuwe na tofauti.
- Mheshimiwa Spika, aidha napenda kuzikumbusha Halmashauri
za Wilaya kote nchini kuendelea kuweka na kutekeleza mipango madhubuti ya matumizi
bora ya ardhi, na wale wenye Benki ya Ardhi wagawe kwa busara kwa wafugaji, wazuie
wafugaji wengine wasiendelee kuingiza mifugo katika maeneo ya kilimo na watumie sheria
ndogo zilizopo na kama hazipo ziandaliwe na kutumiwa; na ikibidi wahalifu wapelekwe
mahakamani. Aidha, niwakumbushe wafugaji wote kufuata sheria na kwamba Serikali haitasita
kuwachukulia hatua wafugaji watakaoingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima kwa
makusudi.
- SEKTA YA NISHATI
Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Pili
- Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa nishati
ya umeme, Serikali imeendelea kutoa mkazo katika kutekeleza na miradi mikubwa ya uzalishaji
na usafirishaji umeme pamoja na miradi ya kusambaza umeme vijijini. Ili kuhakikisha
huduma ya umeme inawafikia wananchi wengi, hususan waishio vijijini, Serikali kupitia
REA imeendelea kutekeleza Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Pili tangu
mwaka 2014. Mradi huu unatekelezwa katika wilaya zote za Tanzania Bara. Hadi kufikia
Oktoba, 2016 ujenzi wa kilometa za njia ya msongo wa Kilovolti (kV) 33 umefikia Asilimia
95.6; ujenzi wa kilometa za njia ya Msongo wa Volti 400
umefikia Asilimia 89.3; na ufungaji wa transfoma umefikia Asilimia
87.2. Aidha, jumla ya wateja 146,311 wa awali sawa na
Asilimia 59 ya lengo la wateja 255,000 wameunganishiwa umeme
kupitia mradi huo.
Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu
- Mheshimiwa Spika, Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi
cha miaka 5 katika vijiji 7,873 vya wilaya zote za Tanzania Bara.
Takriban vijiji 7,697 vitapelekewa umeme wa gridi ya Taifa na vijiji
176 umeme wa nje ya gridi (Off-grid). Mpango huu utaongeza
wigo wa usambazaji umeme katika maeneo ambayo hayakufikiwa na miradi ya REA Turnkey
Phase I na II. Ili kutekeleza miradi hiyo kwa kasi zaidi, Serikali ya
Awamu ya Tano katika bajeti yake ya mwaka 2016/17 iliongeza fedha za kupeleka umeme
Vijijini kutoka Shilingi Bilioni 357.117 zilizotengwa mwaka 2015/16
hadi Shilingi Bilioni 587.61 mwaka 2016/17. Hadi kufikia mwezi Oktoba,
Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 109.8 kwa ajili ya Mfuko
wa Nishati Vijijini kutoka kwenye vyanzo vya fedha za ndani. Kati ya fedha hizo Shilingi
Bilioni 100.4 ni tozo ya mafuta na Shilingi Bilioni 9.4
ni tozo ya umeme.
- Mheshimiwa Spika, zabuni za kupata wakandarasi wa
kutekeleza mradi huu zilitangazwa tarehe 1 Agosti, 2016. Kwa sasa REA inaendelea na
uchambuzi wa zabuni hizo. Taratibu zote za mradi huo zimepangwa kukamilika mwezi Januari,
2017. Natoa rai kwa viongozi mbalimbali wa Serikali wakimemo Waheshimiwa Wabunge kuwahamisha
wananchi katika maeneo yao kutumia fursa ya kuunganishiwa umeme wakati wakandarasi
wakiwa kwenye maeneo ya miradi. Katika kipindi hicho bei ya kuunganisha umeme ni Shilingi
27,000 tu kama ilivyotaarifiwa awali katika Bunge hili.
- Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanzisha
Mradi wa Kupanua Wigo wa Upatikanaji wa Umeme Vijijini (Tanzania Rural Electricity
Expansion Project). Mradi huo utagharamiwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia wa
Dola za Kimarekani milioni 209. Mradi ulizinduliwa tarehe 26 Agosti 2016, katika kijiji
cha Kwedikwazu wilayani Handeni Mkoani Tanga na utawezesha kaya takriban 500,000 kupata
huduma ya umeme nchini.
SEKTA YA MADINI
Migodi Mikubwa Kuendelea Kulipa Mrabaha
- Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kati ya Oktoba,
2015 na Oktoba, 2016 Serikali ilifanya ukaguzi na kuwezesha migodi mikubwa kulipa
mrabaha ambapo: Migodi Mikubwa ya Dhahabu ya Biharamulo, Bulyanhulu, Buzwagi, Geita,
New Luika na North Mara imelipa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 69.4
ikiwa ni Mrabaha, sawa na Shilingi Bilioni 151.4. Vilevile, Mgodi wa Makaa ya Mawe
wa Ngaka umelipa kiasi cha Dola za Kimarekani 309,836 na Shilingi
Milioni 676 ikiwa ni mrabaha. Aidha, Mgodi wa TanzaniteOne umelipa mrabaha
wa Dola za Kimarekani 189,731 sawa na Shilingi Milioni 414.
Kuhamasisha Masoko ya Madini ya Vito Nchini
- Mheshimiwa Spika, Serikali iliandaa mnada wa madini
ya vito, hususan tanzanite uliofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 12 Agosti, 2016 Jijini
Arusha. Katika mnada huo madini yenye thamani ya Dola za Kimarekani 3,448,050,
sawa na Shilingi Bilioni 7.56, yaliuzwa na kuwezesha Serikali kukusanya
Dola za Kimarekani 150,491.06, sawa na Shilingi Milioni 331
ikiwa ni mrabaha kutokana na madini yaliyouzwa.
- Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia Sekta
za Nishati na Madini ili ziweze kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa ajili
ya maendeleo ya Taifa letu.
TAARIFA YA MAKUSANYO YA FEDHA KWENYE HALMASHAURI KWA MWAKA 2016/2017
- Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya mwaka 2016/2017
Halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya mapato ya Shilingi Bilioni
665.4. Hadi kufikia Septemba, 2016 Halmashauri zimekusanya Shilingi
Bilioni 114.46, sawa na Asilimia 17.2 ya makisio.
Kiwango hiki cha ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri bado hakiridhishi. Hivyo,
naomba nitumie fursa hii kuhimiza Halmashauri zote nchini kuongeza jitihada katika
kukusanya mapato ya vyanzo vya ndani. Nazihimiza Halmashauri kutumia mifumo ya kielektroniki
katika ukusanyaji mapato na pia katika maeneo ya kutolea huduma za afya ili kudhibiti
upotevu wa mapato. Aidha, naelekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa waimarishe mifumo
ya udhibiti wa ndani na kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana katika kila huduma
au bidhaa inayonunuliwa na Halmashauri. Halmashauri hazina budi kuepuka matumizi ya
fedha yasiyo na tija katika shughuli za uendeshaji wa Mamlaka hizo.
- Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote zinaagizwa zifuatilie
kwa karibu mapato na matumizi ya fedha zinazopelekwa kwenye shule na kwenye vituo
vinavyotoa huduma za afya ikiwemo Hospitali, vituo vya afya na zahanati. Ili kufikia
azma hiyo, uwekwe utaratibu madhubuti wa ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha hizo
kwa kushirikisha Wakaguzi wa ndani wa Halmashauri.
MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE YA LAAC
- Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ushauri mzuri na
mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya LAAC kuhusu ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na 2014/2015, Serikali imeshatoa
maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa zinatekeleza kwa ukamilifu
maelekezo yote ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati
nyingine ili kuondoa hoja zilizojitokeza katika taarifa ya CAG. Aidha, Halmashauri
zinaelekezwa kuimarisha mifumo ya uthibiti wa ndani na kutumia vizuri ushauri unaotolewa
na Kamati za Ukaguzi ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha
za umma.
- Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kwamba Halmashauri
zote ni lazima zitekeleze vipaumbele vilivyoidhinishwa katika mpango na bajeti kwa
mwaka 2016/17 kwa kupanga vema utekelezaji kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha. Halmashauri
ziendelee kuimarisha usimamizi wa mikataba ili thamani ya fedha za Serikali iweze
kupatikana katika miradi na Kandarasi nyingine zilizoingia Mikataba na Halmashauri.
-
- Mheshimiwa Spika, wakati tunahitimisha mkutano huu
leo, napenda nitumie nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na
Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia vizuri na kwa weledi mkubwa vikao vyote vya
mkutano huu. Niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu. Ninashukuru
pia Watendaji wa Serikali kwa kuwasaidia Mawaziri na Naibu Mawaziri katika kujibu
maswali na hoja mbalimbali za Wabunge. Niwashukuru wanausalama wote kwa kazi yao nzuri.
Niwashukuru madereva wote kwa kuwaendesha Mawaziri, Wabunge na Watendaji wote kwa
usalama kabisa. Niwashukuru pia wanahabari wote kwa kuihabarisha jamii juu ya mkutano
wetu. Kipekee, nimshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah na timu yake kwa
kutuwezesha kukamilisha shughuli zote za mkutano huu kwa mafanikio makubwa.
- Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini si kwa umuhimu,
nitumie muda huu kumwomba Mwenyezi Mungu awalinde na awaongoze Waheshimiwa Wabunge
wote katika safari ya kurejea majumbani kwenu. Aidha, nawatakia kila la kheri na fanaka
katika sikukuu zijazo za mwisho wa mwaka na kuwatakia mwaka mpya wa 2017.
- Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, napenda
kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 31 Januari,
2017, siku ya Jumanne, saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika
ukumbi huu hapa Dodoma.
- Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hojaSEKTA