2016-11-12 08:54:00

Ijumaa ya Huruma: Papa akutana na Mapadre walioacha Upadre


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa “Uso wa huruma” “Misericordiae vultus” anasema, ukweli wa kwanza kabisa wa Kanisa ni upendo wa Kristo. Kanisa linapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha upendo huu kwa watu wote. Huu ni upendo unaojionesha kwa kusamehe na kujisadaka kwa ajili ya wengine. Na matokeo yake, popote pale ambapo kuna Kanisa, huruma na upendo wa Baba wa milele unapaswa kuonekana. Huruma hii ionekane katika: Familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Parokia, Jimbo, Vyama vya kitume, kwa neno moja, popote walipo Wakristo, kila mmoja anapaswa kuwa ni chombo, shuhuda na chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu! Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu alijiwekea utaratibu pale inapowezekana wa kufanya tendo la huruma kila Ijumaa.

Katika kutekeleza azma hii, Ijumaa, tarehe 11 Novemba 2016, Baba Mtakatifu aliwatembelea Mapadre walioacha wito na utume wao na kuamua njia nyingine ya maisha, ambao kwa sasa wanaishi mjini Roma wakiwa na familia zao. Kundi hili la familia saba za Mapadre wa zamani zilikutana na Baba Mtakatifu Francisko aliyependa kuwaonesha uwepo wake wa karibu, ili kuwapatia faraja ya kibaba baada ya Mapadre hawa kutoa huduma ya Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma, wakajikuta wanaingia katika upweke, kiasi cha kugundua kwamba, walikosea katika kuchagua wito wa maisha wao!

Hawa ni Mapadre vijana anasema Baba Mtakatifu walioteseka katika maisha na utume wao, lakini kwa sasa wanaonekana kuwa huru. Baba Mtakatifu alipoingia kwenye nyumba iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya tukio hili, alilakiwa na kundi la watoto na wazazi wao walionesha furaha kwa kutembelewa na Baba Mtakatifu kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwani hata wao wameonja ndani mwao huruma ya Mungu inayoponya na kumkomboa mwamini. Baba Mtakatifu alitumia muda huu kusikiliza historia ya maisha, wito, ushauri waliopata na hatima ya kesi zao. Wote hawa wamehakikishiwa uwepo wa Baba Mtakatifu kwa njia ya sala katika mahangaiko yao, kielelezo cha upendo na mshikamano.

Kwa tukio hili, Baba Mtakatifu Francisko amekunja jamvi la Ijumaa ya huruma ya Mungu kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Itakumbukwa kwamba, katika kipindi cha mwaka mzima, Baba Mtakatifu amewatembelea wazee, wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji; Mapadre wazee na wagonjwa. Amesali kwenye kambi za mateso nchini Poland; akatembelea hospitali ya watoto wagonjwa pamoja na kushiriki Tafakari ya Njia ya Msalaba wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Jimbo kuu la Cracovia, Poland. Baba Mtakatifu pia alitembelea Jumuiya ya Papa Yohane XXIII inayojihusisha na huduma ya upendo na ukarimu kwa wanawake na wasichana wanaotumbukizwa kwenye utumwa mamboleo. Ametembelea pia kituo cha wagonjwa walioko kufani mjini Roma, ili kuwafariji na mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko mwezi Oktoba, 2016 ametembelea “Kijiji cha SOS” kituo kinachotoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na familia zinazokabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.