2016-11-11 16:46:00

Maadhimisho ya Siku ya shukrani nchini Italia kwa Mwaka 2016


Siku ya 66 ya Kitaifa ya Shukrani nchini Italia, itaadhimishwa tarehe 13 Novemba 2016. Baraza la Maaskofu Italia, katika kushiriki wito wa Umoja wa Mataifa kujikita katika kutatua matatizo ya kijamii na kazi, haki na amani, wanatoa ujumbe wao kwa maadhimisho ya Siku ya Shukrani nchini kwao, ujumbe unaojikita katika wimbo wa Mzaburi: “Wewe waotesha nyasi kwa ajili ya mifugo, na mimea kwa matumizi ya binadamu, ili naye ajipatie chakula chake ardhini.” (Rej., Zaburi 104: 14).

Mtazamo wa Maaskofu katoliki nchini Italia unaalika kuchochoea shughuli halisi na dhahiri zinazojikita katika namna mbali mbali za uzalishaji na matumizi ya chakula, kama vile kuthamini tena masoko mahalia, kushirikisha watu dhaifu na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii au wasiofadika sana na kilimo jamii, na juhudi za kisheria za kurudisha ardhi za wakulima zilizotekwa na waonevu wachache, na zaidi sana juhudi za uwazi na ukweli katika utoaji taarifa kwa watumiaji wa mazao. Ni muhimu sana kuhangaikia malezi na elimu ya Lishe na Chakula Bora, na kutoa kipaumbele katika Uzalishaji Mahalia na hasa kwa wakulima wadogo wadogo. Hili litakuwa jibu tosha katika kutatua uharibifu wa mazingira, myumbo wa uchumi kitaifa, mzunguko hafifu wa bidhaa na hudumapamoja na udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kazi za mwanadamu zinapotendeka katika mshikimano na kuheshimu utu na hali ya ardhi na viumbe vyote, kadiri ya mpango wa Mungu Muumbaji, ndipo Familia ya binadamu itashamiri katika ubora wake, na kukomaza udugu kati yao. Maisha ya mbeleni ya binadamu yanategemea sana chakula safi na cha kutosha. Kwa sababu hiyo, Maaskofu nchini Italia, wanasisitiza umuhimu wa kilimo duniani katika kupambana na baa la njaa na utapia mlo, ili kulinda afya bora za watu. Ukweli huu unaonekana kusahauliwa na wengi. Ikumbukwe kuwa Umoja wa Mataifa umeutangaza mwaka huu, 2016, kuwa mwaka wa Mboga za jamii ya Kunde. Lengo ni kutumia vyakula hivi vyenye protini na virutubisho bora zaidi, kwa afya bora ya mwanadamu.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.   








All the contents on this site are copyrighted ©.