2016-11-11 11:41:00

Dumisheni utamaduni wa ukarimu na upendo kwa wagonjwa


Utamaduni wa ukarimu na mshikamano kwa ajili ya huduma kwa watu wenye magonjwa adimu na yanayoweza kuponyeka ni kati ya tema ambazo Baraza la Kipapa  la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya limekuwa likizifanyia kazi kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Magonjwa adimu na yale yanayoweza kutibiwa bado yanaendelea kusababisha maafa mateso na mahangaiko kwa wagonjwa.

Yote haya ni matokeo ya huduma hafifu za afya. Shirika la Afya Duniani linakadiria kwamba, kati ya watu millioni 350 – 400 wanasumbuliwa na magonjwa adimu na yale ya Ukanda wa Joto ambayo yanaweza kutibiwa. Kumbe, hapa kuna haja ya kujenga mshikamano wa upendo ili kuhakikisha kwamba, wagonjwa hawa wanapata tiba muafaka na kamwe wasitelekezwe kana kwamba, ni magari mabovu! Ili kufanikisha azma hii kuna haja ya kuwa na tafiti makini na endelevu, ili kubainisha chanzo na hatimaye kutoa tiba muafaka kwa magonjwa haya.

Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, makampuni makubwa ya dawa hayapendi kuwekeza katika magonjwa haya kwani yanafahamika kuwa ni magonjwa yatima! Hata pale tafiti zinapofanywa na dawa kupatikana, mara nyingi uzalishaji wake unasitishwa kutokana na ukosefu wa faida kubwa ikilinganishwa na magonjwa makubwa makubwa duniani. Haya yamesemwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican Ijumaa, tarehe 11 Novemba 2016 alipokuwa anazungumza na wajumbe wa mkutano wa XXXI wa Kimataifa kuhusu magonjwa adimu na yanayoweza kupatia tiba muafaka.

Hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na Serikali mbali mbali duniani, lakini ukweli wa mambo unaonesha kwamba, Serikali nyingi zimeanza kupunguza bajeti katika masuala ya afya. Matokeo yake anasema Kardinali Parolin, dhamana hii inatekelezwa na vyama vya wanafamilia wenye magonjwa adimu, vyama na mashirika ya kiraia pamoja na taasisi za afya za Kanisa Katoliki. Hata hivyo bado kuna haja ya kuwekeza zaidi katika suala hili.

Magonjwa ya Ukanda wa Joto yanayoweza kutibiwa yanawaathiri watu wengi wanaoishi katika nchi maskini zaidi duniani. Magonjwa haya kadiri ya taarifa za Shirika la Afya Duniani yanaweza kutibiwa na watu kupona kabisa kwa gharama nafuu, lakini kutokana na uzembe na hali ya kutojali, watu wengi wanaendelea kuteseka kwa magonjwa haya duniani. Shirika la Afya Duniani, hivi karibuni lilizindua kampeni ya kupambana na magonjwa haya kwa kushirikiana pia na taasisi za afya zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki katika maeneo husika.

Hata hapa bado kuna haja ya kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba watu wengi zaidi wanafaidika kwa huduma hii inayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa. Mkazo ni kujenga mtandao wa huduma za kuzuia, uchunguzi wa kina na hatimaye tiba makini kwa wale watakaogundulika kuwa wameathirika na magonja haya. Kardinali Parolin anakaza kusema, kuendelea kushamiri kwa magonjwa haya ni kutokana pia na umaskini. Kumbe, huduma ya makini ya afya haina budi kwenda sanjari na mapambano dhidi ya umaskini duniani kama sehemu ya haki msingi za binadamu. Mapambano haya pia yanapaswa kuungwa mkono na upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya mahitaji ya binadamu. Elimu makini na unyanyapaa dhidi ya waathirika utaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya magonjwa adimu na yale yanayoweza kupatiwa tiba

Kardinali Parolin anahitimisha hotuba yake kwa kusema, kuna haja kwa wadau mbali mbali kushirikiana na serikali husika ili kuhakikisha kwamba, lengo hili linafanikiwa pamoja na kuwahusisha wafanyakazi katika sekta ya afya. Vyombo vya mawasiliano ya jamii, vinaweza kusaidia kuhabarisha jamii kuhusu mapambano haya, ili watu wengi zaidi waweze kutambua madhara na hatimaye kushiriki vyema katika kutafuta suluhu ya kudumu dhidi ya magonjwa adimu na yale yanayoweza kutibika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.