2016-11-10 01:00:00

Utunzaji bora wa mazingira: Changamoto na matumaini!


Ekolojia timilifu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa kama yaliyofafanuliwa na Mwenyeheri Paulo VI, Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na sasa Papa Francisko ni mada ambayo imepembuliwa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, Jumatano, tarehe 9 Novemba 2016 kwenye Makao Makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, mjini Paris, nchini Ufaransa.

Majadiliano haya yamehudhuriwa na ujumbe wa UNESCO chini ya uongozi wa Bi Irina Bokova, Mkurugenzi mkuu wa UNESCO kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa changamoto ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, uliotiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika na baadaye kukaziwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi COP21 uliofanyika mjini Paris, Ufaransa, 2015.

Majadiliano haya pamoja na mambo mengine yametoa kipaumbele cha pekee katika misingi ya mshikamano, haki, usawa na ushiriki mkalimifu kama sehemu ya mchakato wa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na mapambano dhidi ya umaskini ili kuendeleza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, mambo msingi katika Mafundisho Jamii ya Kanisa. Itakumbukwa majadiliano haya yamefanyika wakati huu, Mama Kanisa anapofanya kumbu kumbu ya miezi 18 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochapisha Waraka wake wa kitume “Sifa kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”” Laudato si”.

Kardinali Peter Turkson anasema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto inayofumbata matumaini kwani mazingira ni tema inayogusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu ili hatuimaye kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani; usawa, maendeleo, utu na heshima ya binadamu. Huu ni mwaliko pia wa kujikita katika majadiliano yatakodumisha maridhiano na mafungamano ya kijamii kati ya watu. Kanisa katika Mafundisho Jamii kuanzia kwa Papa Leo XIII hadi Papa Francisko, limeonesha uhusiano kati mazingira na ekolojia ya binadamu.

Papa Francisko kwa namna ya pekee kabisa anayatajirisha Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kujikita katika utimilifu wa ekolojia inayomwambata mwanadamu na mazingira yake. Papa Paulo VI alikazia maendeleo kama jina jipya la amani duniani pamoja na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mwelekeo chanya wa matumizi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kudumisha haki duniani sanjari na kusikiliza kilio cha maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi! Mtakatifu Yohane Paulo II akafafanua kuhusu maendeleo ya binadamu yanayojikita katika kanuni maadili na utu wema; matumizi sahihi ya rasilimali ya dunia pamoja na kuepuka uchafuzi mkubwa wa mazingira unaohatarisha maisha ya wengi. Hapa alikazia kuhusu mazingira asilia, ekolojia ya binadamu kwa kukazia umuhimu wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akajikita katika masuala ya ekolojia ya kijamii na ekolojia ya amani, ili kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu, asili ya amani, upendo na mshikamano wa kweli. Ikumbukwe kwamba, maendeleo ya binadamu ni shirikishi na yanajikita katika kanuni maadili mhimili mkuu wa mafungamano ya kijamii. Papa Francisko katika kipindi cha maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameendelea kukazia kuhusu utunzaji bora wa mazingira na ekolojia ya binadamu; maendeleo endelevu, utu na heshima ya binadamu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, mazingira ni zawadi ya Mungu kwa binadamu inayohitaji kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa kwa ajili ya mafao ya wengi dhamana inayopaswa kusimikwa katika mshikamano unaoongozwa na kanuni auni.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi; kwa kuonesha mshikamano na maskini; kwa njia ya toba na wongofu wa kimazingira; elimu makini ya utunzaji bora wa mazingira, kanuni maadili na utu wema. Yote haya yanapania kukuza na kudumisha ekolojia  timilifu ya binadamu. Binadamu anapaswa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya kizazi hiki cha sasa na kile kijacho kwa ari kuu na moyo wa shukrani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.