2016-11-10 15:52:00

Papa Francisko: Msijihangaishe kutafuta miujiza!


Waamini wanapaswa kushinda vishawishi vya dini ya maigizo, dini inayotafuta kila siku ufunuo mpya kana kwamba ni baruti za kupiga wakati wa kusherehekea matukio fulani Fulani, badala yake wanapaswa kulinda matumaini waliyo nayo katika maisha ya kila siku. Katika Misa Takatifu kwenye kikanisa kidogo cha Mt. Martha, mjini Vatican, ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anawalisha waamini Neno la Mungu, siku ya Alhamisi, tarehe 10 Novemba 2016. Mafarisayo wanapomuuliza Yesu: Ufalme wa Mungu utakuja lini. Yeye anawajibu: Ufalme wa Mungu ulishakuja hapa duniani, Ufalme wa Mungu upo kati yenu. Ufalme wa Mungu ni kama mbegu ndogo iliyopandwa na inakua yenyewe kadiri ya muda. Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuifanya ikue.

Mungu kaongea na mwanadamu kwa kupitia Neno wake Yesu Kristo, na huo ni ufunuo wa mwisho. Mwanadamu anapopata vishawishi vya kupata ufunuo mpya au ujumbe kutoka mbinguni kila siku, anaanguka katika hatari ya imani rejareja, imani ya mpito. Ufalme wa Mungu ni kama mbegu inayokua, kama mwanamke anayekanda unga wa ngano na kuandaa mkate, uvumilivu na matumaini vinahitajika, matumaini yanayokua. Baruti za sikukuu sio nuru, ni maigizo yanayopita. Kumbe ni muhimu muumini kukumbatia nuru ya kweli kwa matumaini, kukua siku hadi siku, badala ya kuhangaikia ufunuo mpya, ambao haupo.

Mbegu hiyo ya Ufalme wa Mungu inapaswa kutunzwa vizuri na kwa matumaini ili ikue. Kila mkristo anaye Roho wa Mungu ndani yake, mbegu ya Ufalme wa Mungu imeshapandwa, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuitunza na kuilinda dhidi ya magugu ili ikue vema. Ufalme wa Mungu unajengeka imara katika matumaini. Ni muhimu kuishi imani kwa kuchambua kila siku kwa tafakari, mbegu ni ipi na magugu ni yapi, anafafanua Baba Mtakatifu Francisko. Anawaalika wakristo wote, wajitafakari na kujitathimini kuona ni namna gani kila mmoja anailinda na kuifanya ikue kwa matumaini, mbegu ya Ufalme wa Mungu iliyopo  ndani yake.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.