2016-11-10 07:36:00

Mwaka wa huruma ya Mungu: Toba, Wongofu wa ndani; Maadili na Utu wema


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa familia ya Mungu nchini Ukraine iwe ni fursa ya mwendelezo wa toba na wongofu wa ndani ili kuambata huruma na upendo wa Mungu kwa kupambana kufa na kuponya na vitendo vya rushwa na ufisadi; ukosefu wa haki katika mfumo wa sheria na mahakama; ukosefu wa uaminifu na uwajibikaji katika maeneo ya kazi; ulevi wa kupindukia pamoja na kushamiri kwa utumwa mamboleo, mambo yanayonyanyasa utu na heshima ya binadamu, kiasi hata cha kuhatarisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Armenia katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema matukio yote haya yanayoonesha saratani ya dhambi jamii nchini Ukraine inayopaswa kufanyiwa kazi kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kufanya mageuzi makubwa katika maisha ya watu: kiroho na kimwili. Mchakato huu ni muhimu sana ili kuimarisha imani, matumaini na mapendo ya familia ya Mungu nchini Ukraine kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho!

Toba na wongofu wa ndani ni changamoto na mwaliko kwa familia ya Mungu nchini Ukraine inayohitaji kujikita katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani na utakaso wa kitaifa, ili kukimbilia toba, msamaha na huruma ya Mungu kwa ajili ya wananchi wa Ukraine. Toba ni mwaliko wa kuacha dhambi na makando kando yake, tayari kufanya malipizi kwa dhambi zilizotendwa. Hii ni changamoto na wajibu wa raia na viongozi wao katika medani mbali mbali za maisha.

Jamii inapaswa kulinda, kuheshimu na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai, huruma na upendo wa Mungu, kwa kulinda na kutetea maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Jamii isimame kidete kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili ya familia; utu na heshima ya kila binadamu aliyembwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Taifa halina budi kuanza mchakato wa mageuzi katika vyombo vya sheria na mahakama, ili kweli haki iweze kutendeka. Wananchi wajikite katika kudumisha tasaufi ya maisha yao ya kiroho sanjari na kutunza mazingira nyumba ya wote! Wananchi waoneshe ari na ujasiri wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira sanjari na ujenzi wa Jumuiya ya Ulaya kwa kutekeleza dhamana na wajibu wake badala ya kutaka kuwafurahisha wakuu wa mataifa. Wananchi waongozwe na Neno la Mungu, Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na utu wema.

Hapa waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanatakiwa kusimama kidete kupinga sera zinazotaka kumong’onyoa tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili kwa kupandikiza sera zinazokinzana na sheria asilia, kanuni maadili na utu wema. Mambo haya yakiendekezwa na kushabikiwa na baadhi ya wanasiasa matokeo yake ni uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu na wasichana na watoto wengi kugeuzwa na kutumbukizwa katika wimbi la utumwa mamboleo na nyanyaso za kijinsia. Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk  anahitimisha kwa kusema, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, atawasamehe waja wake dhambi zao, ikiwa kama watamrudia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani tayari kuambata utakatifu wa maisha. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ukoleze chachu ya toba na wongofu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.