2016-11-10 16:07:00

Kanisa linawashukuru Watawa wa Upendo kwa huduma makini!


Wakati wa mahubiri yake, katika Misa Takatifu pamoja na wamisionari wa Upendo, mjini Lusaka, Zambia, Alhamisi, tarehe 10 Novemba 2016 Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, anawaalika wazambia kumshukuru Mungu kwa sala na sadaka, kwa ajili ya miaka 125 ya uinjilishaji nchini humo. Wakati Kanisa likiwa bado na kumbukumbu hai za kutangazwa Mtakatifu, mama Theresa wa Calcuta, ni jambo la kumshukuru Mungu kwa utume na huduma za wamisionari wa Upendo sehemu mbali mbali za dunia, hasa miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Waamini wengi leo wanapendelea imani ya maonesho zaidi, lakini Kristu anapofundisha kwamba Ufalme wa mungu upo tayari kati ya watu, anawakumbusha kuuthamini na kufaidika na matunda ya Ufalme huo ambao kweli upo,  ingawa katika hali ya ukimya, na ni ufalme unaokua taratibu ndani ya mioyo ya watu. Huu ndio utume, huu ndio umisionari wa Kanisa. Kazi ya wamisionari na waamini wote ni kuutambua Utakatifu wa Ufalme wa Mungu ulio kati ya watu, katika familia za kikristo ambapo kwa uvumilvu wanalinda maisha ya familia, wanajali watoto na wazee, na mara nyingi hufanya hivyo bila kitu mfukoni, lakini wanadumu katika sala. Ni wajibu wa kila mkristo kuonesha kwamba Ufalme wa Mungu upo hata katika mateso, katika msalaba wa kazi na familia. Palipo na msalaba, hapo Kristo yupo. Na alipo Kristo, Ufalme wa Mungu upo katika mamlaka yake. Hivyo waamini wanaalikwa kuonesha uwepo wa Ufalme huo hasa kwa wahitaji. Wakumbuke anachosema Kristo mwenyewe: mlichomtendea mmoja wa wadogo hawa, mmenitendea mimi.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.