2016-11-09 08:48:00

Uchumi unaojali na kuzingatia mafao ya wengi!


Udugu, Mshikamano, Ukarimu, na Upendo kwa jirani, ni misingi ya muhimu katika kukabiliana na changamoto za: kinzani, mafarakano na hata myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; ni hatua ya kwanza katika kujenga jamii ya haki na usawa, inayonuia kuakisi mji ule wa milele, Yerusalemu ya mbinguni ambapo hapatakuwa na kilio wala mahangaiko (Ufunuo 21). Ni maneno matamu kabisa ya ufunguzi ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican, katika kitabu chake: Mababa Watakatifu na Jubilei, kutoka Leo XIII hadi Francisko.

Kardinali Parolin anaonesha jinsi gani tangu Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIII, Rerum Novarum, Mababa Watakatifu wamekuwa na mwono wa kujenga jamii yenye kujikita katika tunu msingi  za kibinadamu na Kikristo, kwa mshikamano wa Kikatoliki unaojumuisha wote wenye mapenzi mema, ikiwa ni nyenzo ya Huruma ya Mwenyezi Mungu. Mababa Watakatifu Benedekto XVI na Francisko, wamekuwa wakisisitiza pia kuwa: jamii yenye nia ya kuheshimu utu wa mwanadamu, haiwezi kusahau umuhimu wa mshikamano, ambao ni mfano wazi wa kujenga uchumi wenye fikra za udugu na jumuiya.

Tangu wakati wa Baba Mtakatifu Leo XIII, jamii ilikuwa imegawanyika kuanzia mwisho wa karne ya kumi na nane hadi mwisho wa karne ya kumi na tisa, ambapo wachache walikuwa matajiri sana na wenye nguvu kwa  kuhozi mali na mamlaka, huku wengi wakikandamizwa na kuishi katika umaskini mkubwa na majanga. Hali hii hata leo inaonjwa katika jamii mbalimbali. Baba Mtakatifu Francisko anaonya kuwa: mahali popote pale, panapokuwepo hali ya utajiri na umaskini mkubwa kwa pamoja, ni aibu na kashifa kwa utu wa binadamu. Na sio hilo tu la utajiri kwa wachache na umaskini kwa wengi, bali pia suala la fedha za kimataifa usio na sheria makini, pamoja na myumbo wa uchumi, ni kati ya vitu vinavyopelekea kutokuwa na hali nzuri kimaisha na usawa, tangu enzi za karne ya kumi na nane mpaka leo.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanatambua umuhimu wa fedha na uchumaji kwa ujumla katika kuendesha maisha ya mwanadamu, hivyo mashirika, taasisi zote, na vyama vya wafanyakazi, vinaalikwa kuzingatia kwamba: watu wanapata kazi zenye kujali utu na heshima ya mwanadamu, mishahara ya kutosheleza mahitaji msingi, BIMA za afya na Maisha ya jamii, na hasa akiba ya kutosha kujali wanaopata ajali kazini au wanaostaafu kazi, badala ya kuwa na akiba ya kuokoa hali ya viwanda tu wakati wa myumbo wa uchumi.

Tangu wakati wa Sherehe ya Pentekoste, Kanisa limeishi hali ya kuzingatia maendeleo ya maisha ya watu na ukuaji wa Mafundisho msingi ya Kanisa. Uchumi sio uhalisia pekee wa maisha ya binadamu, bali ni sehemu tu ya maisha ya jamii. Kwa sababu hiyo ni muhimu kuepuka suala la uchumi na fedha likawa ndiyo mwongozo na pengine kulifanya kuwa ndiyo kila kitu katika maisha ya jamii. Kufanya hivyo ni kupoteza dira katika maisha, na ndipo majanga mengi yanatokea na haki kuvunjwa. Elimu juu ya uchumi isiwe nadharia tu, bali izingatie pia Taaluma zingine kama vile Falsafa na Maadili Jamii. Uchumi uzingatie pia uhalisia wa maisha na utu wa mwanadamu, kwa kujali mahitaji yake msingi, haki zake katika kazi, na maisha jamii kwa ujumla, kama anavyosisitiza Papa Francisko katika Barua yake ya Kitume Laudato si. Elimu na Uelewa juu ya jamii, mwanadamu, na kuheshimu Uumbaji, vinapasawa kuwa mwanga katika upembuzi na maisha ya uchumi.

Fedha na faida kubwa vimegeuka kuwa miungu ya wenye tamaa leo, kiasi cha kutojali Utu wa mwanadamu na haki zake. Wafanyakazi wanadhalilika na kunyimwa haki msingi katika baadhi ya sehemu, ambapo wenye tamaa wachache wanapata faida kubwa. Mababa Watakatifu wanakumbusha kuwa: akili na utashi wa mwanadamu una uwezo wa kuchanganua ubaya na wema, hivyo maendeleo ya sayansi, teknolojia na ukuaji wa uchumi, visiweke kiwingu katika akili na utashi wa mwanadamu, kiasi cha kuumizana, kunyanyasana, na kudhalilishana, amesisitiza Kardinali Pietro Parolini katika kitabu chake. Wajibu huu unawagusa sio tu mashirika, taasisi na vyama vya wafanyakazi duniani, bali pia mashirika na taasisi za uzalishaji za kimataifa, serikali mbalimbali, vikundi vya kijamii na taasisi za haki, ili kuhakikisha uchumi wa haki na ukweli unajengwa kwa mafao ya wengi.

Kardinali Parolini anasema, ni kweli kuwa tangu karne ya kumi na nane mpaka leo, mwanadamu amekumbana na vita, uonevu, na uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu, lakini pia zimekuwa karne zilizoguswa kwa Utakatifu, ambapo wamejitokeza wasamaria wengi waliosaidia wahitaji, wakiwa wanaishi Injli ya Bwana: “Amri Mpya nawapa: Mpendane; kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa mmekuwa wanafunzi wangu” (Yohane 13: 34 – 35). Ndivyo Kardinali Parolin katika kitabu chake, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuishi Amri hiyo ya upendo kama sehemu ya mchakato wa harakati za kujenga uchumi wa dunia, unaosimikwa katika tunu msingi za maisha ya kijamii!

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.