2016-11-09 07:36:00

Kilio cha watu wenye magonjwa adimu na yanayoweza kuponyeka!


Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafanyakazi wa Sekta ya afya, kuanzia tarehe 10 – 12 Novemba 2016 linaadhimisha mkutano wa XXXI wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu “Utamaduni wa ukarimu na mshikamano kwa ajili ya huduma kwa watu wenye magonjwa adimu na yanayoweza kuponyeka”. Shirika la Afya Duniani linakadiria kwamba, kuna watu wanaoathirika kutokana na magonjwa adimu na wengi wao ni magonjwa ambayo wamerithi kutoka kwa wazazi wao, hali inayohatarisha maisha.

Wagonjwa hawa wanakadiriwa kuwa ni zaidi ya millioni 400 na wengine wanateseka kwa magonjwa ambayo yanaweza kuponyeka, ikiwa kama yatapewa tiba muafaka. Waathirika wengi ni wale wanaotoka katika nchi za Ukanda wa Joto, wanaoishi katika mazingira machafu; wanakosa huduma ya maji safi na salama; huduma bora za afya pamoja na baa la umaskini! Hii ni changamoto inayomwandama mwanadamu katika medani mbali mbali za maisha yake. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika hutoaji wa huduma kwa wagonjwa kama sehemu ya dhamana na utume wake.

Haya yamesemwa na Monsinyo Jean-Marie Musivi Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafanyakazi wa Sekta ya afya, Jumatatu, tarehe 7 Novemba 2016 wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican. Anasema, Kanisa linataka kusikiliza kilio cha wagonjwa hawa kwa kukipatia majibu yanayojielekeza zaidi katika misingi ya elimu, utamaduni na shughuli za kichungaji, ili kuweza kukabiliana na changamoto hii.

Hii ni sehemu ya utekelezaji wa matendo ya huruma kimwili, mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Mkutano huu wa kimataifa utajikita zaidi katika mambo makuu matatu: Mageuzi yatakayowawezesha washiriki kuwa na ufahamu mpana zaidi kisayansi na kitabibu. Pili ni tiba inayofumbatwa katika ukarimu na mshikamano katika maisha ya mgonjwa. Tatu ni kulinda na kudumisha mazingira bora anamoishi mgonjwa. Lengo ni kumwangalia mgonjwa katika utimilifu wake: kiroho na kimwili, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu!

Kwa upande wake, Padre Augusto Chendi, Katibu mkuu msaidizi Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafanyakazi wa Sekta ya afya amegusia kuhusu magonjwa haya adimu na yanayoweza kuponyeka, lakini yanaendelea kusababisha mateso, mahangiko na vifo kutokana na tabia ya uzembe na kutoyapatia magonjwa haya uzito unaostahili. Hapa kuna haja ya kujikita katika haki afya itakayowapatia wagonjwa haki ya kupata dawa wanazostahili. Kuna magonjwa anayowatesa watu wanaoishi katika Ukanda wa Joto duniani, lakini hayajapewa uzito mkubwa katika vyombo vya habari kitaifa na kimataifa kutokana na kuwa na ushawishi mdogo katika masuala ya kiuchumi ikilinganishwa na magonjwa kama Ukimwi na Ebola yanayoendelea kutikisa maisha ya watu wengi duniani.

Hapa, Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kwa ajili ya kulinda na kudumisha mafao ya wengi na haki msingi katika huduma ya afya; kusimama kidete kutetea utu na heshima ya binadamu hata katika hali yake ya ugonjwa. Kanisa linataka kuwa kweli ni sauti ya kinabii katika shughuli na mikakati yake katika sekta ya afya kwa kujikita katika mshikamano unaongozwa na kanuni auni, ili kuwasaidia watu wanaoteseka kutokana na magonjwa adimu na yanayoweza kutibika. Hii ni changamoto ya watu kuwa ni Wasamaria wema kwa kuguswa na mahangiko ya jirani zao ambao ni wagonjwa kwa kushiriki na kujisadaka bila ya kujibakiza.

Padre Augusto Chendi anakaza kusema, huu ni mkutano wa mwisho kuandaliwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafanyakazi wa Sekta ya afya kwani, kutokana na utashi wa Baba Mtakatifu Francisko, Baraza hili litakuwa ni sehemu ya Baraza jipya la kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu, linalotarajiwa kuundwa hivi karibuni.

Kwa upande wake, Dr. Claudio Giustozzi anasema kwamba, magonjwa adimu yanachangia kwa kiasi kikubwa mateso na mahangiko ya familia nyingi kiuchumi. Hii inatokana na ukweli kwamba, magonjwa haya hayafahamiki na wengi na wala hakuna jitihada za makusudi za kuweza kuyafanyia utafiti wa kina na kuyapatia tiba muafaka. Ni vigumu sana kwa watafiti kuwekeza katika kile kinachoitwa “Dawa Yatima” kwa vile hakuna wagonjwa wengi wanaohitaji dawa hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.