2016-11-09 07:10:00

Huduma kwa Mungu na jirani inajikita katika unyenyekevu!


Anayetaka kumtumikia Mungu vyema, anapaswa kujitazama kwanza jinsi gani alivyo geugeu na mwenye tamaa. Sababu haiwezekani kumtumikia Mungu na mali. Baba Mtakatifu Francisko anaalika kutafakari ujumbe huo wakati wa mahubiri, katika Misa Takatifu kwenye Kikanisa kidogo cha Mt. Martha, mjini Vatican, siku ya Jumanne, tarehe 8 Novemba 2016. Katika kumtumikia Mungu kuna vikwazo vingi. Kimojawapo ni tamaa ya madaraka, tamaa inayoonekana kila mahali hata katika familia, kujisikia mkubwa kwa kusema wazi wazi au kwa kuonesha kwa vitendo. Lakini Kristo anawaalika wafuasi wake kuwa watumishi wa wote, iwapo wanajisikia hamu ya kuwa wakubwa.

Tamaa ya fedha ni kikwazo kingine katika kumtumikia Mungu. Tamaa ya fedha ni kuwa geugeu, jambo ambalo sio tu dhambi, bali ni tabia ya kufanya maigizo, kucheza na Mungu na kucheza na fedha, na hii ni mbaya zaidi, kwani hakuna uhalisia wa maisha katika hilo. Kwa namna hii mwanadamu anajiondolea amani nafsini mwake, na kujikuta akiishi kwa wasi wasi muda wote.

Katika kumtumikia Mungu, mwanadamu ni mtu huru, ni mwana wa Mungu na sio mtumwa. Kwa sababu hiyo, anapswa kumtukia Mungu kwa uhuru, furaha na wema. Hivyo ni muhimu kumuomba Mungu awaondolee vikwazo hivyo, wakati huo huo wanadamu wenyewe wanafanya bidii kujiepusha na tamaa hizo za madaraka na fedha. Mwanadamu ni mtumishi asiye na faida, amruhusu Roho Mtakatifu atende kazi ndani yake ili aweze kumtumikia Mungu kwa uaminifu na utulivu wa ndani, na amani ya kweli.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.