2016-11-07 07:10:00

ICC na changamoto kutoka Barani Afrika


Mahusiano kati ya mahakama kuu ya kimataifa ya makosa ya uhaini, alimaarufu kama ICC au The Hague, na nchi baadhi za kiafrika, yamekuwa na changamoto nyingi sana kwa muda sasa. Utendaji wa mahakama hii umekuwa gumzo hivi karibuni, kufuatia utangazaji dhahiri wa nchi tatu wanachama kujiengua kutoka katika umoja wa mahakama hiyo. Nchi hizi ni pamoja na Afrika ya kusini, Burundi na Gambia.

Pamoja na ukweli kwamba, bado zipo nchi za Afrika wanachama wa mahakama hii, wanaosimamia kidete umuhimu na utendaji wake, ule uchangamkiaji wa awali wa nchi za Afrika kwa mahakama hii, unaonekana kupoa sana kwa ujumla, kiasi kwamba kuna hatari ya ongezeko la nchi zinazonuia kujiengua kutoka katika ushirika huo, zikiwemo Kenya, Uganda na Namibia. Vugu vugu kubwa lilianza  mwezi Juni 2015, katika kikao cha kidiplomasia kilichohusisha Afrika kusini, Jijini Johanesburg, ambapo Rais wa Sudan Bwana Omar Al Bashir pia alishiriki, akiwa ni mmoja wa watuhumiwa kufuatia mauaji ya Darfur ya mwaka 2009 na 2010. Tangu kikao hicho, Pretoria ilianza kutishia kujitoa. Oktoba 21 mwaka huu 2016, waziri wa mambo ya nje wa Afrika ya kusini, ndugu Maite Nkoana-Mashabane aliutaarifu Umoja wa Mataifa, nia yao ya kujiengua, kwa madai kwamba: shughuli za Mahakama kuu ya kimataifa ya makosa ya uhaini, zinapingana na kinga ya kidiplomasia wanayokuwa nayo viongozi wakuu wa mataifa.

Tarehe 28 Oktoba 2016, nchi ya Burundi imefuata njia ya Afrika ya kusini kuomba kujiengua, kupitia waziri wao wa sheria, ndugu Aimèe Laurentine, kwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-moon. Wakati huo, siku tatu kabla mnamo tarehe 25 Oktoba 2016, Gambia ilikuwa imewasilisha nia yake ya kujitoa. Ukweli ni kwamba, kinzani kati ya mahakama ya The Hague na nchi za Afrika, zina historia ya nyuma kidogo, tangu Juni 2011 huko Malabo, Equatorio Guinea, ambapo nchi hizo zilianza kukubaliana kutia mgomo wa kushiriki katika kuwatia nguvuni, watuhumiwa wakuu wa mataifa baadhi ya Afrika, kuanzia na Rais wa wakati huo wa Libya, Bwana Ghaddafi.

Januari 2016, Umoja wa Afrika uliunda kamati ya kuandaa taratibu za nchi zote za Afrika kujiengua katika umoja wa mahakama hiyo, kufuatia kushtakiwa kwa Rais Uhuru Kenyata na msaidizi wake Bwana William Ruto, kwa tuhuma za makosa dhidi ya haki msingi za binadamu, kwa kuruhusu machafuko yaliyopelekea vifo, baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya, tarehe 4 Marchi 2014. Mwaka 2015, kwa kukosa ushahidi wa kutosha, Rais Kenyatta aliachiliwa huru, lakini kesi dhidi ya Bwana William Ruto bado inaendelea.

Nchi za Afrika zinapambana dhidi ya mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhaini kwa jambo moja kubwa, ambalo ni haki ya kinga ya kidiplomasia ya wakuu wa nchi, kutoshtakiwa wakiwa katika uongozi, hivi kwamba mahakama hiyo haiwezi kujiamulia nini cha kufanya na kwa namna inavyotaka. Msimamizi mkuu wa mahakama hiyo, Bwana Fatou Bensouda anasema: ni lazima kusimama imara kutoruhusu ama kufumbia macho hata kidogo, kwa yeyote anayetenda, anayetoa amri, anayeshawishi, anayeshabikia au anayechangia kwa namna yeyote makosa dhidi ya haki msingi za binadamu. Bwana Ban Ki-moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, anasisitiza kwamba, ni muhimu viongozi wa Afrika watambue kwamba, kinga ya kidiplomasia ya viongozi wa mataifa, haiwezi kukandamiza haki msingi za binadamu. Hata hivyo, katika nyanja za kidiplomasia, kunaaminika kwamba, kutapatikana namna ya kutafuta suruhu juu ya suala hilo.

Mahakama ya The hague, ilianzishwa 1998 Jijini Roma, na kuanza kazi zake rasmi 2002 huko Hague, Uholanzi, ikiwa na wanachama 125, ambao kati yao ni nchi 24 za kiafrika. Mahakama hii inahusika na makosa ya uhaini dhidi ya binadamu ikiwa ni pamoja na mauji, makosa ya kivita na makosa dhidi ya haki msingi za binadamu. Ushiriki katika umoja wa mahakama hii ni uhuru wa nchi. Umuhimu wa mahakama ni dhahiri katika kulinda haki na utu wa binadamu kisheria. Jambo la kujiuliza: iwapo machafuko, ugaidi na uvunjwaji wa haki unaendelea namna hii sehemu mbali mbali duniani, halafu kuna mlolongo wa nchi wanaonuia kujiengua, Je haki za binadamu na utu wake zitaheshimiwa na kulindwa kwa uzito gani! Ieleweke kwamba, utawala wa sheria na haki ndio utawala bora, na hakuna aliye juu ya sheria. Haki msingi za binadamu na utu wake, havifai kuzimwa na kupotezewa kwa kushabikia manufaa ya wachache.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya kiswahili, Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.