2016-11-06 10:19:00

Papa Francisko: Ni kashfa kuokoa taasisi za fedha wakati watu wanakufa maji!


Mkutano mkuu wa tatu wa Shirikisho la Vyama vya Kijamii Kimataifa imekuwa ni fursa nyingine tena ya kuweza kupembua kwa kina na mapana mchakato mabadiliko unaowahusisha watu wa kawaida katika jamii, ili kushikamana kama binadamu, tayari kukabiliana na changamoto za maisha zinazosababishwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Uchumi hauna budi kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu; ujenzi wa haki na amani, unapaswa kupewa msukumo wa pekee sanjari na kujizatiti katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Jamii inahitaji kuona mabadiliko yatakayowawezesha watu kupata fursa za ajira; wananchi kuweza kumiliki ardhi kwa ajili ya kujipatia chakula na mahitaji yao msingi; watu wanahitaji kuwa na makazi bora na salama. Ubaguzi, nyanyaso, vita na kinzani za kijamii ni mambo ambayo yanadumaza, ustawi na maendeleo ya wengi; Injili ya uhai kwa kukuza na kuendeleza utamaduni wa kifo. Kuna haja sasa ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mshikamano na upendo, ili kuboresha maisha ya watu wengi zaidi pamoja na kuendelea kuwapatia utambulisho wao. Ukoloni mamboleo na utandawazi tenge ni hatari sana kwa maendeleo ya watu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 5 Novemba 2016 alipokuwa anazungumza na wajumbe wa Mkutano mkuu wa tatu wa Shirikisho la Vyama vya Kijamii Kimataifa. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu katika hotuba yake amejikita katika vitendo vya hatari na kuta zinazowatenga watu; umuhimu wa kujenga mshikamano wa upendo na madaraja ya watu kukutana; huduma kwa utu na heshima ya binadamu, badala ya kuwekeza katika kuokoa taasisi za fedha zinazoendelea kufilisika kwa kujikita zaidi na zaidi katika kanuni maadili na utu wema.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu katika maisha na utume wake, alitoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu! Akajitahidi kumpatia mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili, kiasi cha kujitambulisha kuwa ni kiongozi aliyekuwa huru kuishi, kupenda na kuhudumia jirani. Aliwalisha watu, akawaganga na kuwaponya magonjwa yao na mwishoni aliwaondolea dhambi na kuwaweka huru kabisa. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na vyama vya kijamii kwa kuunda mfumo wa uchumi na kijamii unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi bila ya kuogopa kusadaka maisha kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi!

Lengo ni kuendeleza mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu yanayofumbata utu, heshima, umoja, upendo na udugu pamoja na kujikita katika utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote. Inasikitisha kuona kwamba, kuna wakimbizi na wahamiaji wanakufa maji, lakini viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanajadili namna ya kuokoa taasisi za fedha zinazoendelea kufilisika kutokana na ukosefu wa kanuni maadili na sheria makini. Vita inaendelea kurindima sehemu mbali mbali za dunia kutokana na kushamiri kwa biashara haramu ya silaha inayopandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo.

Umefika wakati wa kuokoa maisha ya watu badala ya Bahari ya Mediterrania kugeuka kuwa ni kaburi la wazi kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Lakini, ikumbukwe kwamba, wahamiaji na wakimbizi si tatizo bali ni changamoto kubwa ya dunia nzima. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika utekelezaji wa haki jamii, kwa kuokoa maisha ya wakimbizi na wahamiaji pamoja na kudhibiti mambo yote yanayosababisha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji.

Vyama vya kijamii vinahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kuhakikisha kwamba, vinashiriki kikamilifu katika majadiliano tete na nyeti kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwani siasa kimsingi ni huduma ya kijamii inayofumbatwa katika upendo na mshikamano wa dhati. Vyama vya ushirika viendelezwe na kudumishwa ili kuwajengea maskini uwezo wa kiuchumi, ili kuboresha hali ya maisha yao.

Demokrasia itoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini, mafao na ustawi wa wengi, tayari kupambana na umaskini, ili kujenga usawa unaofumbatwa katika kanuni maadili, utu wema, imani na sayansi jamii. Kamwe viongozi wa vyama vya kijamii wasikubali kutumbukia na kutumbukizwa katika kashfa ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma unaoweza kufanywa katika masuala ya uchumi, kisiasa na kijamii. Kanuni maadili, imani na utu wema viwe ni msingi na dira katika utekelezaji wa shughuli zao.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, watu wanapomezwa sana na malimwengu kwa kupenda fedha, mali na vyeo wanahatarisha mustakabali wa jamii nzima na matokeo yake wanakosa furaha, amani na utulivu wa ndani. Kanuni maadili na imani ni mambo yatakayowasaidia kuwa na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao! Viongozi wa vyama vya kijamii washinde woga usiokuwa na mashiko wala mvuto kwa kujikita katika utamaduni wa maisha ya huduma, mshikamano, unyenyekevu na upendo unaoponya na kuganga familia yote ya binadamu. Hata katika dhuluma na nyanyaso kama ilivyokuwa kwa Martin Luther King aliweza kukuza na kudumisha upendo wa kidugu kwa kupinga kwa nguvu zote chuki, uhasama na hali ya kulipizana kisasi. Jamii iwe na ujasiri wa kuvunjilia mbali mnyororo wa vita, chuki na uhasama kwa kujikita katika nguvu ya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.