2016-11-06 07:50:00

Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani: Uwajibikaji wa Makanisa!


Uwajibikaji wa kila mmoja ni suala ambalo Wakristo wote wanapaswa kulizingatia kwa makini wakati huu Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani linapoadhimisha Jubilei ya miaka 500 tangu mageuzi ya Kiluteri yalipofanyika. Hii ni nafasi nyingine ya kutumainia na kuonja matunda ya kiekumene, sambamba na tukio kubwa la kiekumene lililofanikishwa Lund, Sweden, kuanzia tarehe 30-31 Novemba 2016. Huu ni uchambuzi wa Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, akiwasilisha mada yake katika Chuo Kikuu cha Heidelberg, Ujerumani.

Katika dunia ya leo ya mgawanyiko wa Makanisa, ni jambo la msingi ule utendaji wa pamoja katika jitihada za kiekumene. Mageuzi ya Kiluteri  Dunianiyalianza mwaka 1517 na uchapishwaji wa maoni 95 ya Luther, ambayo yameigusa kwa kina historia ya ulaya na dunia nzima, na kuleta mgawanyiko mkubwa wa Wakristo. Maadhimisho ya miaka 500 ya mageuzi hayo yanapaswa kuwa fursa nyingine ya kuweka katikati uwajibikaji wa pamoja, kwa kutilia maanani uvumbuzi wa karama ambazo makanisa yameshirikishana kwa kipindi hicho chote, badala ya kujikita kwenye majivuno na tabia ya kupenda madaraka.

Dr. Tveit anasema, Wakristo wanapaswa watazame historia ya nyuma na uhalisia wa hali ya leo, wakijiakisi mbele ya Uso wa Mungu kwa kutambua kuwa wameumbwa kwa sura na mfano wake, na hivyo kuvumbua tena wajibu wao kwa viumbe vyote duniani. Hivyo kunahitajika mwenendo wa unyenyekevu, thabiti, uwazi na ukweli. Mazungumzano kati ya makanisa yamekuwa kiini cha safari ya pamoja ya Wakristo katika kuishuhudia Injili. Kama vile makanisa ya Ireland ya kaskazini na Afrika kusini yalivyofanya, kawaalika Wakristo wote kujifunza kuponya kumbukumbu za kale zenye maumivu, ili kuachana na tofauti zinazotenga na kuzingatia mazuri yanayojenga umoja wao. Kwa namna hii matunda ya kiekumene yataonjwa zaidi kati ya wakristo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.