2016-11-06 08:07:00

Jubilei ya miaka 25 ya huduma kwa familia ya Mungu!


Umoja wa Kanisa la Kiorthodox, mazungumzano ya kitaalimungu na wakristo wengine, na yale ya dini tofauti, mlipuko wa vita na ugaidi, changamoto za wakimbizi na wahamiaji, myumbo wa uchumi na wakijamii na utunzaji wa mazingira ni masuala makuu ambayo Askofu Mkuu wa Konstantinopoli, Patriaki Bartolomeo wa kwanza, anayazungumzia na kuyakabili kwa matumaini kwa siku za usoni, anapoadhimisha miaka 25 ya kuchaguliwa kwake katika utumishi huo ndani ya Kanisa la Kiorthodox.

Patriaki Bartolomeo ameeleza kwamba, mafanikio yaliyopatikana katika utendaji wa Makanisa ya kiorthodoksi ni matunda ya mshikamano na juhudi za kujituma za wasaidizi wake, maaksofu na mapadri wanaotenda utume wao katika maeneo yote kuanzia nchi za Afrika, nchi za Mashariki na Magharibi. Amegusia pia umuhimu wa Sinodi ya kiorthodox iliyofanyika mwezi Juni, katika kisiwa cha Creta, Ugiriki. Ni wajibu wa wote kuyapokea na kuyafanyia kazi maamuzi ya sinodi hiyo.

Kawaalika kuombea amani duniani na kuwakumbuka ndugu wakristo wanaoteswa na kudharirishwa sababu ya imani yao. Amekazia kusema kwamba, hakuna vita takatifu, bali ni amani peke yake ambayo ni takatifu, na lengo la mwisho la pamoja la binadamu wote. Kaalika pia kuwaombea wahamiaji  kwa hofu na maumivu, wakizingatia yale wanayopitia wahamiaji hao, na kwamba siasa safi na uchumi unaojali wote viwe haswa ndiyo kipaumbele cha mwanadamu mahali kote duniani.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.