2016-11-06 11:46:00

Andikeni historia yenu kwa neema na baraka na uwajibikaji binafsi


Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka mtakatifu wa huruma ya Mungu kwa ajili ya wafungwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili, tarehe 6 Novemba 2016, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican yamepambwa kwa shuhuda mbali mbali za jinsi watu walivyoguswa na huruma ya Mungu katika maisha yao. Umekuwa ni muda wa sala na tafakari na hatimaye, Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko alikita mahubiri yake katika fadhila ya matumaini yanayobubujika kutoka katika Liturujia ya Neno la Mungu. Ni matumaini yaliyooneshwa na wafiadini kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya matumaini ya maisha ya uzima wa milele!

Yesu katika Injili anajibu kwa ufasaha juu ya matumaini ya maisha ya uzima wa milele kwa kusema kwamba, Mungu si wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake! Kwa maneno haya, Yesu anaufunua Uso wa huruma na Mungu anayetamani maisha ya watoto wake na matumaini katika maisha ya uzima wa milele, mwaliko wa kuwa waaminifu kwa mafundisho ya Yesu. Ikumbukwe kwamba, fadhila ya matumaini ni zawadi kutoka kwa Mungu inayokita mizizi yake katika sakafu ya moyo wa mwanadamu, ili kupata mwanga unaofukuzia mbali giza la mahangaiko na mateso ya mwanadamu.

Matumaini yanapaswa kuwa thabiti ili kweli yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwanza kabisa kwa kutambua na kukiri uwepo endelevu wa upendo wa Mungu licha ya mateso na mahangaiko yanayomsibu mwanadamu. Pale ambapo mwanadamu ametenda dhambi na kukengeuka katika maisha yake, Mungu anaweza kumfikia kwa njia ya huruma yake kwa kuamsha toba na wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho. Baba Mtakatifu anakaza kusema, maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wafungwa ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaopaswa kufumbatwa katika maisha ya mwanadamu. Pale makosa yanapotendeka, sheria haina budi kuchukua mkondo wake, lakini udhibiti wa uhuru wa mtu ni adhabu kubwa ambayo mtu anaweza kuitekeleza kwani inagusa kiini cha maisha yake, lakini hata katika mazingira kama haya, bado matumaini yanapaswa kuendelea kuchanua kama Mwerezi wa Lebanon.

Mwanadamu anaadhibiwa kwa makosa anayotenda, lakini daima anaendelea kuwa na matumaini ambayo kamwe hayawezi kuzimishwa kama moto wa kibatari! Moyo wa mwanadamu, daima unatamani yaliyo mema, kumbe, matumaini ni mchakato unaomwezesha Mwenyezi Mungu kukutana na mwanadamu pasi ya kumtelekeza! Hii inatokana na ukweli kwamba, Mungu ni kiini na chemchemi ya matumaini, kiasi kwamba, huruma kwa waja wake, inaendelea kumtendea, hadi pale atakapomwona mwanadamu aliyetenda dhambi na kukengeuka, anatubu na kumwongokea, tayari kukimbilia na kuambata huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka! Matumaini ni fadhila ambayo ni haki ya kila mtu na nguvu ya kusonga mbele pasi na kukata wala kukatishwa tamaa, ili kukumbatia upendo wa Mungu licha ya dhambi za binadamu. Hapa mwanadamu anakumbushwa kwamba, daima yuko katika hija ya matumaini kielelezo cha nguvu ya huruma ya Mungu inayotenda kazi ndani mwake, tayari kusonga mbele ili kushinda kwa nguvu ya imani badala ya kumkimbia Mungu kwa njia ya ubaya na dhambi.

Maadhimisho ya Jubilei ya Wafungwa Duniani yamewasha tena moto wa matumaini ya kuwa na uhuru wa kweli, dhamana inayotekelezwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Wafungwa katika hali zao, wanayo nafasi ya kuweza kubadilika na kuwa watu wema zaidi, kwani hapa duniani wote wametenda dhambi na kutindikiwa anasema Baba Mtakatifu na pengine wana bahati tu kwamba, hawajakamatwa na kutiwa gerezani. Kuna watu ambao ni wafungwa wa maamuzi mbele; watu waliomezwa mno na malimwengu kwa kupenda fedha na mali na matokeo yake ni watu wanaopenda kutunga sera na sheria zinazoendelea kumkandamiza mwanadamu na kumsukumizia kwenye kuta za ubinafsi, hali ya kujiamini na kukosa ukweli unaoibua uhuru. Hakuna sababu ya kumwanyooshea wenginge kidole kwa kuwa wamekosa na kuanguka dhambini, kwani hakuna mtu mwenye haki mbele ya Mungu, lakini pia kuna uhakika wa kupata msamaha, kama yule mwizi aliyetubu pale Kalvari akabahatika kupata maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini kutofungwa na historia ya maisha yao yaliyopita, kwani hawawezi kuiandika tena, bali kwa neema na baraka kutoka kwa Mungu pamoja na uwajibikaji wa mtu binafsi, waanze kuandika historia ya maisha mapya. Wajifunze kutokana na makosa yaliyopita, waambate na kukumbatia msamaha na huruma ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake katika maadhimisho ya Jubilei ya wafungwa duniani kwa kusema kwamba, nguvu ya imani, iwawezeshe kutoa na kupokea msamaha kwani ni nguvu na huruma ya Mungu peke yake inayoweza kuganga na kuponya madonda ya mwanadamu kwa kuendelea kujikita katika msamaha na upendo, ili hatimaye, wote waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na mapendo. Bikira Maria, awe ni chemchemi ya matumaini ya maisha mapya yanayomwilishwa katika uhuru na huduma kwa jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.