2016-11-05 15:34:00

Wakimbizi wa Palestina wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha!


Katika mkutano wa Umoja wa Mataifa unaoendelea Jijini New York, Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja huo, amechambua hali mbaya ya wakimbizi wa Kipalestina, inayotokana na kutojitosheleza kwa misaada inayotolewa ikilinganishwa na wingi wao. Zipo taasisi na baadhi ya kikatoliki yanayotoa huduma na misaada pia katika maeneo hayo ya mashariki ya kati, katika sekta ya elimu, afya na huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na nyumba za wenye changamoto za kimwili na kiakili, kutokana na mishtuko ya vita na ulipuaji holela wa mabomu.

Kanisa Katoliki linatambua mji wa Yerusalemu kuwa ni hazina ya waamini wa dini tatu waishio katika eneo hilo takatifu, ambao ni Wakristo, Wayahudi na Waislamu. Waamini hawa wanapata changamotio kubwa kushiriki ibada na kufika katika maeneo yao ya ibada na hija, kutokana na machafuko na uharibifu wa sehemu nyingi. Askofu Mkuu Bernadirto Auza, anawaalika Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba wakazi wa eneo hilo wanapata uhuru wa kutosha wa kuabudu na uhuru wa dhamiri.

Ametoa shukrani za dhati kwa nchi za Lebanon na Yordani, kwa ushirikiano wao wa kupokea na kusaidia wakimbizi kutoka Iraq na Siria, pamoja na wale wa Palestina. Hata hivyo kasisitiza kilio cha nchi ya Lebanon, inayoonekana kulemewa na changamoto ya wakimbizi, hivyo wanahitaji msaada wa Jumuiya ya Kimataifa. Pamoja na machafuko na ukatili unaotendeka mpaka sasa maeneo hayo, Askofu mkuu Auza anawaalika Jumuiya ya Kimataifa kutokata tamaa katika utafutaji wa amani maeneo hayo na kwa dunia  nzima, amani ambayo inatamaniwa na inahitajika sana, hivyo wadumu katika matumaini kwamba ipo siku, amani hiyo itachomoza kama jua la asubuhi na kuangaza kheri na furaha.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.