2016-11-05 11:40:00

Mshikamano wa upendo na wakimbizi pamoja na wahamiaji!


Baba Mtakatifu Francisko katika nia yake ya jumla kwa mwezi Novemba, 2016 anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kushikamana katika mchakato wa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha. Jambo hili linawezekana ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itaweza kuunganisha nguvu na rasilimali fedha ili kutoa huduma makini kwa watu wanaoteseka kutokana na vita, njaa, umaskini, nyanyaso, dhuluma na majanga asilia.

Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu ambao umetolewa kwa njia ya video na mtandao wa Utume wa Sala Duniani, anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na hofu, wasi wasi na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji na badala yake, wajenge na kudumisha utamaduni wa ukarimu, upendo na ushirikiano. Hapa duniani hakuna mtu ambaye anauhakika wa hatima ya maisha yake kwa leo na kesho ijayo!

Leo ni zamu ya wakimbizi wanaoangaliwa kwa jicho la kengeza, lakini kesho na kesho kutwa anasema Baba Mtakatifu anaweza kuwa ni mtu yoyote kati yetu! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye katika sala, ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali mbali mbali katika mchakato wa kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi na wahamiaji, ambao kwa sasa wamekuwa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Anawapongeza na kuwaomba viongozi wa nchi hizi, kuendeleza mshikamano wa huruma na upendo kwa watu wanaohitaji msaada zaidi. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Kati yao ni vijana wanaojitolea, madaktari wanaoendelea kuokoa maisha, waandishi wa habari wanaoendelea kuhabarisha, askari wa vikosi vya ulinzi na usalama, wanaoendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha amani na utulivu; mambo yanayojenga na kuimarisha utamaduni wa upendo, mshikamano na ukarimu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao, ili utu na heshima yao viweze kulindwa na kudumishwa na wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.