2016-11-05 12:13:00

Mh. Pd. Philip Davou Dung ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Shendam!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Philip Davou Dung, Paroko na mshauri wa mchumi wa Jimbo kuu la Jos, Nigeria kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Shendam, nchini Nigeria. Askofu mteule Philip Davou Dun alizaliwa tarehe 19 Agosti 1958, Jimbo kuu la Jos, Nigeria. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 24 Novemba 1984 kwa ajili ya Jimbo kuu la Jos, Nigeria.

Tangu kunako mwaka 1984 amewahi kuwa Paroko usu na hatimaye Paroko katika Parokia mbali mbali hadi mwaka 1991 alipoteuliwa kuwa mkurugenzi wa miito Jimbo kuu la Jos, Nigeria. Tangu mwaka 1992 hadi mwaka 1994 alipelekwa mjini Roma, ili kuendelea na masomo zaidi kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Alfonsiani na aliporejea Jimboni mwake, akapangiwa kuwa Paroko usu. Tangu mwaka 1999 – 2002 alikuwa ni Mwalimu wa Taaluma, Seminari kuu ya Mt. Agostino huko Jos. Baadaye aliteuliwa kuwa Paroko, Makamu wa Rais, Baraza la Wakleri Jimbo kuu la Jos; Paroko; mjumbe wa Baraza la Washauri wa Jimbo kuu la Jos; Mchumi mkuu wa Jimbo na hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yosefu, huko Du, Jimbo kuu la Jos, Nigeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.