2016-11-05 14:57:00

Mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu!


Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni janga kubwa dhidi ya ubinadamu, linaloendelea kukua na kupanuka kila kukicha kutokana na baadhi ya watu kuendelea kujinufaisha kwa biashara hii haramu dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 30% ya waathirika wa biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo na viungo vya binadamu ni wale watu wanaotoka katika nchi ambazo hapo awali zilikuwa chini ya utawala wa Kikomunisti! Asilimia 13% ya waathirika hawa ni watu kutoka Amerika ya Kusini; asilimia 7% ni kutoka nchi za Ulaya ya Kati; asilimia 5% ni watu kutoka Barani Afrika na asilimia 3% ni wale wanaotoka Barani Asia.

Hizi ni takwimu ambazo zimetolewa na Mtandao wa Mashirika ya Kitawa Barani Ulaya dhidi ya Biashara haramu ya binadamu na unyonyaji, (RENATE) Ijumaa, tarehe 4 Novemba 2016 wakati viongozi wakuu wa mtandao huu walipokuwa wanazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican. Bi Imelda Poole, Rais wa RENATE anasema, mtandao huu utaanza mkutano wake mkuu wa pili, Jumapili tarehe 6 – 11Novemba 2016, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Hatima ya biashara haramu ya binadamu inaanza na sisi wenyewe”.

Katika mkutano huu na waandishi wa habari, wameshiriki pia Bi  Ivonne Vandekar aliyefafanua kwa kina na mapana jinsi ambavyo mtandao wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unavyoendelea kuwanyanyasa watu. Sr. Monica Chikwe afisa kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anayeshughulikia mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, amefafanua mtindo wa soko la biashara haramu ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia.

Sr. Chikwe anasema, waathirika wakubwa ni wanawake na wasichana wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo, unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Katika biashara haramu ya ngono, kuna umati mkubwa wa watu wanaojitajirisha na kufaidika kutokana na kashfa hii dhidi ya utu na heshima ya binadamu na matokeo yake, biashara inaendelea kupamba moto kila kukicha Barani Ulaya. Hii inatokana na ukweli kwamba, Ulaya kuna soko la biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Sr. Chikwe amepembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo Umoja wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Italia unavyoendelea kuivalia njuga changamoto na kashfa hii kwa kupambana kufa na kupona na wahusika wa biashara hii, sanjari na kuwasaidia waathirika waliotumbukizwa kwenye janga hili la kijamii, ili waweze kuandika tena upya ukurasa wa maisha yao, kwa imani na matumaini makubwa zaidi.

Wanawake na wasichana wengi, wanatumbukizwa katika biashara hii kutokana na umaskini, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka; ndoto ya kupata maisha bora zaidi Barani Ulaya, maisha wanayoyatazama kwenye vyombo vya habari na kuonekana kana kwamba, Ulaya hakuna tena shida, lakini wanapofikishwa Barani Ulaya, hapo wanatambua kwamba, wameingizwa mjini na kinachobaki ni kutekeleza amri ya wale waliowaleta, vinginevyo wanaweza kusuka au kunyoa! Wakakiona kile kilichomn’goa Kanga manyoya! Kwani wafanyabishara ya binadamu na utumwa mamboleo ni watu hatari, mishipa ya huruma imekwisha kukatika katika maisha yao!

Katika mazingira ya utumwa mamboleo, wanawake na wasichana wanaangaliwa kwa jicho la kengeza kwani wao ndio wale wanaoonekana kuwa watu wanaovuruga ndoa za watu, upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Wakati mwingine, wamekuwa ni chanzo cha magonjwa na vifo kwenye familia za watu. Lakini ili hawa mahakaba waweze kuonekana, lazima wawepo watu wanaowatafuta na kwa mtindo huu, utumwa mamboleo utaendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Mapambano dhidi ya utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, hayana budi kuanzia katika dhamiri ya watu wenyewe.

Waathirika wa vitendo hivi vinavyowapora wanawake utu na heshima yao, wanapaswa kusaidiwa ili kuondoka kwenye mazingira yanayowanyanyasa. Pili, kuwaponya na kuwaganga madonda haya kwa njia ya ushauri nasaha. Tatu, kuwawezesha kiuchumi na kijamii, ili kuanza tena kuandika historia ya maisha yao, huku wakihudumiwa na mtandao wa watawa dhidi ya biashara haramu ya binadamu na unyonyaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.