2016-11-04 14:50:00

Mashuhuda wa imani 38 kutoka Albania


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi tarehe 5 Novemba 2016 anamwakilisha Baba Mtakatifu Francisko huko Scutari, Albania kwa ajili ya kuwatangaza watumishi wa Mungu 38 kuwa ni Wenyeheri. Hili ni kundi ambalo linawaunganisha Maaskofu 2, Mapadre wa Jimbo 25, Wafranciskani 7, Wayesuit 3, Mseminari 1 na Waamini walei 4 kati yao, kuna mkandidati aliyekuwa anawania kusadaka maisha yake kama mtawa, lakini akakumbana na kifodinia hata kabla ya wakati!

Hawa ni waamini waliouwa kikatili nchini Albania Karne iliyopita kutokana na utawala wa Kidekiteta wa Kikomunisti, ambao haukuta kuona uhuru wa kidini unatekelezwa na kushuhudiwa nchini Albania. Hapa waamini wa dini zote walionyanyaswa na kuteswa bila ubaguzi, lakini kwa namna ya pekee, dhuluma hizi zilielekezwa kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini Albania. Hii inatokana na ukweli kwamba, imani yao kwa Kristo Yesu, ulikuwa ni ushuhuda wa imani na utambulisho wa kitamaduni.

Kardinali Angelo Amato anasema, Mashahidi wa imani kutoka Albania, walionesha kwa namna ya pekee fadhila ya: Msamaha, ukweli, nguvu, udugu, huruma na upendo wa Mungu uliokuwa unawaambata na kuwasindikiza ili kukabiliana na madhulumu haya katika maisha yao. Hawa ni watu ambao walioosha mavazi na utu wao kwa Damu ya Mwanakondoo wa Mungu, wakauvua utu wa kale na kujivika utu mpya kwa kukataa katu katu: mbegu ya ya chuki na kinzani iliyokuwa inapandikizwa kwa misingi ya kisiasa; wakaambata na kutangaza: amani, furaha, udugu na umoja wa kitaifa; watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wakakombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo!

Ni katika mazingira kama haya, watesi wao waliwataka kuwaonesha Mungu wao, ambaye kwa wakati huo alionekana kuwa hana nguvu tena! Kardinali Angelo Amato anasema, huu ulikuwa ni wakati wa kimya kikuu cha Mungu katika maisha na utume wa Kanisa nchini Albania, lakini aliendelea kuwasindikiza, wakati wa njia yao ya Msalaba kuelekea Kalvari, ili kuweza kuunganisha mateso yao na mateso ya Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Kwa namna ya pekee, Kanisa linawakumbuka Wafiadinidi: Padre Lazer Shantoia na Padre Ndre Zadeia, waliouwawa kikatili hapo tarehe 5 Machi 1945. Wengine waliopata faraja ya pekee, kiasi cha kuyasadaka maisha yao kwa ajili ya imani kwa Kristo na Kanisa lake kunako mwaka 1956 walikuwa ni Giovanni Fausti na Daniel Deian; Wayesuiti; Padre Gion Shllaku, Mfranciskani.

Katika orodha hii, yumo Jandokasisi Mark Cuni na kijana Gjelosh Lulashi aliyekuwa kijana mbichi kabisa wa miaka 21 tu, lakini akawa tayari kumshuhudia Kristo pasi na woga wala makunyanzi. Orodha hii anasema Kardinali Angelo Amato inakamilishwa na Mzee Qerim Sadiku, Baba wa familia, aliyeyamimina maisha yake ili kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika kanuni maadili na utu wema. Maaskofu waliuwawa kikatili sana, kwani wao ndio waliokuwa wamepewa dhamana ya kufanya majadiliano na Serikali, lakini matokeo yake wakakamatwa na kutiwa mbaroni kama “chuma chakavu”, wakashindishwa njaa na kiu hadi mauti ilipowafika! Kielelezo cha ukatili mkubwa wa binadamu! Wengine walitandikwa na kucharazwa viboko hadharani, kiasi cha kutumbukizwa katika dimbwi la matope na huko wakafa katika mateso makali

Pamoja na patashika yote hii nguo kuchanika, lakini Mti wa Msalaba, kielelezo cha hekima, huruma na upendo wa Mungu, ukaendelea kusimama dede! Hii ikawa ni nguvu na mwanzo mpya wa Kanisa nchini Albania, lililosimika imani, matumaini na mapendo yake kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Damu ya mashuhuda hawa wa imani, imekuwa ni chachu ya Ukristo wenye mvuto na mashiko nchini Albania. Pale ambapo Mapadre walikosekana, wazazi na walezi, wakachukua dhamana ya kurithisha moyo wa sala; imani, matumaini na mapendo kwa watoto wao; familia ikawa ni shule ya kwanza ya tunu msingi za Kiinjili, Imani na Utu wema.

Wakristo wakaadhimisha Mafumbo ya Kanisa ufichoni; Biblia, ukawa ni mkate wao wa njiani katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Kunako mwaka 1990, Jua la haki likachomoza, huo ukawa ni mwanzo wa maadhimisho ya Pasaka ya Bwana, kusherehekea ushindi wa imani. Tarehe 4 Novemba 1990 kwa mara ya kwanza Ibada ya Misa Takatifu ikaadhimishwa kwenye Makaburi Scutari na kuhudhuriwa na bahari ya waamini.

Tarehe 25 Aprili 1993, Mtakatifu Yohane Paulo II akabariki Jiwe la msingi la madhabahu ya Bikira Maria, Mama wa Shauri Jema, Msimamizi na mlinzi wa Nchi ya Albania. Kwa maombezi na tunza ya Mama huyu, Kanisa Katoliki nchini Albania, likabaki imara na thabiti, licha dhoruba na mateso walioyokumbana nayo Wakristo nchini humo. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kutosahau makovu ya mateso na mahangaiko yao, lakini bila kulipiza kisasi, kwani hawana vipimo sahihi vya huruma na upendo wa Mungu. Anawataka waamini kusonga mbele kwa imani na matumaini, kwani mbele yao kuna mambo mazuri zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.