2016-11-04 09:45:00

Huruma ya Mungu inajionesha katika ufufuko wa wafu!


Kila Dominika tunapokiri imani yetu huwa tunahitimisha kwa maneno yafuatayo: “ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo, amina!” Hii ni kiri imani ambayo inatuhakikishia maisha baada ya kifo. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha hivi kuhusu maisha baada ya kifo: “Tunasadiki kwa uthabiti, na pia tunatumaini kwamba kama vile Kristo alivyofufuka kweli kutoka wafu na anaishi daima, vivyo hivyo wenye haki, baada ya kifo chao, wataishi daima katika Kristo Mfufuka, naye atawafufua siku ya mwisho” (KKK 988). Hivyo msingi wa maisha ya ufufuko ni Kristo Mfufuka. Tunaipokea zawadi hiyo ya ufufuko wa miili katika kuungana kwetu na maisha ya Kristo mfufuka. Yeye anapokuwa hai ndani mwetu ndipo nasi tunakuwa hai katika Yeye.

Tukizama zaidi tunaweza kupata mwanga zaidi na kuuelewa Ufufuo katika fumbo la uumbaji. Mungu alimuumba mtu mzima: mwili na roho. Mwanadamu katika mwili anamiminiwa uzima wa kimungu ambao unamfanya aendelee kuungana naye. Mwili wetu huu wa kibinadamu unapokufa kwa sababu ya dhambi ni haki kabisa kupatiwa ufufuko ili kwamba katika hali ya utukufu mbele ya Mungu uwe katika ukamilifu wake, yaani mwili na roho. “Kwa kifo, mtengano wa roho na mwili, mwili wa mtu huoza, pindi roho yake huenda kukutana na Mungu ikingojea kuunganika na mwili uliotukuka. Mungu kwa uwezo wake mkuu, atairudishia kwa hakika miili yetu, uzima usiharibika na kuiunganisha na roho zetu, kwa nguvu ya ufufuko wa Yesu” (KKK 997).

Wakati wa tukio la Ufufuko Kristo alitufunulia namna ambavyo miili yetu itakavyofufuka. “Mbona mnafadhaika na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo” (Lk 24: 38b – 39). Katika ufufuko tunafufuka na miili ileile. Miili hii inakuwa si sawa na miili ya kidunia bali katika hali ya utukufu, yaani miili ile ambayo inakuwa katika uhalisia wake tangu wakati wa uumbaji. Ni miili ile ambayo inaipatia roho iliyo pumzi ya Mungu maskani stahiki yasiyo na mawaa yoyote.

Masomo ya Dominika ya leo hususani somo la kwanza na Injili yanatupeleka moja kwa moja katika tafakari hiyo. Somo la kwanza linatupatia mbele yetu mfano wa wale ambao wanautambua vema uzima wa mwili tunaoutarajia baada ya kifo cha mwili huu tulionao sasa na wanaukumbatia vema bila kujali matukano, mateso, manyanyaso na makandokando mengine ya kiulimwengu yanayoweza kukatisha tamaa. Kwa ufupi wanaungana mtumishi wa Mungu Ayubu kusema: “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, na kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi lakini katika mwili wangu nitamwona Mungu” (Ay 19:25 – 26).

Huku ndiko kuichuchumilia neema ya Mungu inayofunuliwa kwetu kwa njia ya Kristo aliye Uso wa huruma yake. Maana “Mungu alimtuma Mwanae ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani ‘Baba!” (Gal 4:4 – 6). Hali hii ya kuwa waana wa Mungu, yaani pale tunapokuwa na uzima wa kimungu ndani mwetu kunatustahilisha kuupokea ufufuko wa miili. Hivyo kwa huruma yake tunafanywa kuwa watoto wake katika maisha ya ufufuko. Vijana hawa saba tunaowasikia katika somo la kwanza wanatupatia nguvu na mwanga wa namna ya kuushinda ulimwengu ambao hutuondoa katika kundi la wana wa Mungu na kuikumbatia amri ya Mungu na kuwa tayari kufa kwa ajili ya Neno lake.

Mienendo na mawazo ya kidunia hutuzuia kuonja na kuikumbatia huruma hii na mara nyingi hujikuta tunaitupilia mbali na zaidi kuwazibia wengine ambao pengine wamekwishaanza kuijongea kwa sababu wamepatwa na mwanga fulani kutoka juu wasiionje. Hili ndilo linalojitokeza katika somo la Injili. Masadukayo wanapingana na habari ya ufufuo wa miili, tukio ambalo ni zawadi tunayoipokea kwa sababu ya huruma ya Mungu, kwa sababu bado hawajakuwa tayari kutoka katika utu wao wa kale na kuiruhusu neema ya Mungu kufanya kazi ndani mwao. Swali la Masadukayo kwa Yesu halikulenga katika kupata elimu na ufafanuzi zaidi bali lilitaka kumjaribu Kristo na kuonesha jinsi elimu yake au utume wake ulivyo wa hovyo.

Kristo anawaambia waziwazi kwamba “wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na Malaika, nao ni wana wa Mungu, kama vile walivyo wana wa ufufuo”. Huruma ya Mungu ndiyo inayotustahilisha kuhesabiwa katika ulimwengu mwingine. Huruma hii inatufanya kuwa watoto wake na hivyo miili yetu inakuwa katika hali ya utukufu, hali ambayo haiendani na mawazo na namna za ulimwengu huu. Katika maisha mmoja hufanana na malaika ikimaanisha kwamba anakuwa katika maisha ya utumishi au wanakuwa wajumbe wa Mungu.

Maisha haya ya utukufu yanaweka kipao mbele tendo la kumrudishia Mungu utukufu wake anaostahili, yaani kumtambua Yeye kama Baba yetu aliyejaa wingi wa huruma na mapendo. Ufufuko huo wa miili ni zawadi ya uaminifu wetu katika maisha yetu ya kawaida hapa duniani, maisha ambayo yamefumbatwa katika imani thabiti katika Kristo anayesema: “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi. Naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele” (Yoh 11:25b – 26). Kristo anaendelea kuonesha ile iliyo hamu ya Mungu kwamba ni kuwa na wale walio hai na si walio wafu. Mababu tunaotajiwa katika somo la Injili wamewekwa kama kielelezo kwetu kwani kwa maisha yao ya imani waliendelea kuwa hai kwa Mungu na ndivyo walivyo hata leo na milele.

Unabaki kuwa ni wajibu wetu kuikimbilia huruma hiyo, yaani kuungana na Mungu daima huku tukitaraji kuungana naye katika maisha baada ya kifo. Kubaki waaminifu katika huruma ya Mungu kunaonekana katika uaminifu wetu na imani yetu thabiti kwa Mungu. Pale tunapotekeleza yote kadiri ya mapenzi yake na si mapenzi ya wanadamu. Waraka wa Mtume Paulo kwa Watesalonike unatuhamasiha katika uimara huo pamoja na kwamba tutapitia changamoto mbalimbali za kimaisha katika jamii yetu. Mtume Paulo anasema kwamba Mungu “aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema, katika neema awafariji mioyo yenu na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema”. Faraja hiyo ya Mungu ambayo inafumbwa katika tendo lake la huruma kwa wanadamu kwa njia ya Kristo ndilo linatufanya sisi kuwa watoto wake na kuungana naye milele katika utukufu.

Kutoka Studio za Radio Vaticani mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.