2016-11-04 15:15:00

Huduma ya kichungaji kiroho kwa wafungwa magerezani!


Kuwatembelea wafungwa ni kati ya matendo saba ya huruma kimwili ambayo yanapewa kipaumbe cha pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wafungwa na mahabusu wataadhimisha mwaka wa huruma ya Mungu kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 6 Novemba 2016, ili kuonesha upendo na mshikamano wa Kanisa kwa wafungwa na mahabusu. Ni nafasi kwa Mama Kanisa kuamsha tena ari na moyo wa huduma kwa wafungwa gerezani, ili kuwajengea matumaini mapya, ili pale wanapomaliza adhabu yao waweze kurejea tena katika maisha ya kawaida wakiwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia gerezani!

Hivi karibuni, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE kwa kushirikiana na Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafungwa, (Iccpc) waliendesha kongamano  juu ya huduma kwa wafungwa gerezani kwa kukazia kwa namna ya pekee: umuhimu wa kuheshimu na kuthamini utu wa binadamu; uhuru wa kuabudu pamoja na kuepuka vitendo vya ukatili na unyanyasaji wanavyoweza kutendewa wafungwa gerezani.

Kwa upande mwingine, wafungwa wanatakiwa pia kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani ambayo imekuwa wakati mwingine chanzo kikuu cha mateso na mahangiko yao gerezani. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi, ili kusaidia mchakato wa mabadiliko katika maisha ya wafungwa magerezani. Kongamano hili liliwashirikisha wadau kutoka katika Makanisa na dini ya Kiislam wanaojihusisha katika huduma kwa wafungwa na mahabusu Barani Ulaya.

Kwa pamoja wamepembua kwa kina na mapana mambo yanayopelekea uwepo wa misimamo mikali ya kidini na kiimani magerezani hususan Barani Ulaya. Katika mkutano huu, kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko aliwataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya wafungwa magerezani. Hali ngumu  ya maisha gerezani kisiwe ni kisingizio cha kuwanyanyasa na kuwatesa wafungwa au kudhalilisha utu na heshima yao kama binadamu. Hawa ni watu wenye haki zao msingi zinazopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa bila kigugumizi.

Wajumbe wa kongamano hili wamepongeza juhudi zilizowezesha kuchapishwa kwa Mwongozo kwa ajili ya huduma kwa wafungwa na udhibiti wa uhuru kwa wafungwa wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani; mwongozo ulioidhinishwa na Baraza la Ulaya hapo tarehe 2 Marchi 2016. Uhuru wa kidini na uhuru wa kujieleza ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa na kuheshimiwa na wadau mbali mbali kwa ajili ya wafungwa magerezani. Ili wafungwa waweze kupata haki zao msingi, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kuabudu, kuna haja kwa viongozi wa dini kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma msingi kwa wafungwa gerezani. Hii pia ni sehemu muhimu katika mapambano dhidi ya misimamo mikali ya kiimani. Serikali na wadau mbali mbali wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wafungwa gerezani wanapata huduma za maisha ya kiroho, ili kuwajengea wafungwa mazingira yanayojikita katika imani na matumaini kwa wale wanaowahudumia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.