2016-11-03 08:40:00

Mshikamano wa Papa Francisko kwa wananchi wa Italia!


Matetemeko ya ardhi yaliyotokea hivi karibuni nchini Italia yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Zaidi ya watu 22, 000 wamekuwa wakipewa msaada wa dharura tangu tetemeko lililotokea tarehe 24 Agosti na lile la tarehe 26 Oktoba, 2016. Kuna zaidi ya wananchi 15, 400 wanaohudumiwa kwenye miji yao na wengine 6, 700 wanahudumiwa kwenye hoteli baada ya nyumba zao kutangazwa kwamba hazifai tena kwa matumizi ya binadamu. Waziri mkuu wa Italia, Matteo Renzi ameonesha matumaini kwamba, Serikali yake itaivalia njuga changamoto hii ili kuipatia ufumbuzi kwa kuwajengea tena wananchi uwezo wa kusimama na kuendelea tena na shughuli zao.

Baba Mtakatifu Francisko  kwa kuguswa na mahangaiko ya wananchi wa Italia, hususan kwenye Jimbo kuu la Spoleto- Norcia ambako tetemeko hili limesababisha maafa makubwa, amempigia simu Askofu mkuu Renato Boccardo, akimwomba awafikishie sala, baraka na kuwaonjesha uwepo wake wa karibu wale wote walioguswa na kutikiswa na tetemeko la ardhi nchini Italia. Rais Sergio Mattarella wa Italia aliyekuwa nchini Israeli, amelazimika kurejea nchini Italia, ili kujionea mwenyewe madhara yaliyosababishwa na tetemeko hili la ardhi ambalo linaendelea kutishia usalama, maisha na maendeleo ya wananchi wengi wa Italia.

Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na taarifa kwamba, nyumba nyingi za Ibada na majengo ya kumbu kumbu za kale zimeharibiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na tetemeko hili. Huu ni utambulisho wa imani na utamaduni wa watu mahalia. Askofu mkuu Renato Boccardo amemshukuru Baba Mtakatifu kwa uwepo wake wa karibu na faraja kwa familia ya Mungu nchini Italia ambayo kwa sasa inateseka sana kutokana na majanga asilia.

Askofu mkuu Renato Boccardo ameunda Kikosi kazi cha Matumaini kwa ajili ya kuwasaidia, kuwafariji na kuwatia moyo waathirika wa tetemeko la ardhi, ili waweze kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo; kwa kushikamana na kusaidiana kwa hali na mali. Kanisa Katoliki nchini Italia linaendelea kuonesha ukaribu wake na wale wote walioathirika kwa kuwasaidia kiroho, kimwili na kisaikolojia. Katika mazingira kama haya ya mchoko na hali ya kukata tamaa anasema Askofu mkuu Boccardo, Kanisa halina budi kuwa mstari wa mbele ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu wanaoendelea kukata tamaa kutokana na majanga asilia. Ni muda muafaka wa kuwapangusa machozi kwa mafuta ya Injili ya huduma na mapendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.