2016-11-02 07:50:00

Tamko la Pamoja: Waluteri na Wakatoliki katika Uekumene wa huduma!


Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani Jumatatu, tarehe 31 Oktoba 2016 huko kwenye Uwanja wa michezo wa Malmo, Swden, imekuwa pia fursa kwa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja na Shirikisho la Huduma ya Waluteri Duniani kutiliana sahihi mkataba wa makubaliano kwa ajili ya kusimama kidete kulinda na kudumisha utu wa binadamu pamoja na haki jamii! Caritas Internationalis ilianzishwa kunako mwaka 1951 ni muungano wa Mashirika 165 ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa yanayotekeleza dhamana katika nchi 200 duniani. Lengo ni kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu; umoja na mshikamano wa upendo.

Kwa upande mwingine, Shirikisho la Huduma ya Waluteri Duniani ni chombo cha huduma kilichoanzishwa na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri kunako mwaka 1947, ili kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji pamoja na kutoa huduma za kibinadamu kwa wahitaji pamoja na kusimama kidete, kulinda na kutetea haki msingi za binadamu! Mashirika haya mawili kwa miaka ya hivi karibuni, yamekuwa yakishirikiana katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi kwa njia ya huduma makini kwa wahitaji.

Maadhimisho ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani imekuwa ni fursa nyingine tena ya kuanza mchakato wa upatanisho katika Uekumene wa huduma unaofumbatwa katika ushuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia ya kutangaza Injili inayojikita katika huduma, ili walimwengu waweze kuamini! Ushirikiano huu unalenga pamoja na mambo mengine kusaidia mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu kimataifa kufikia mwaka 2030, kwa kupambana na umaskini duniani.

Haya ni mashirika ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika hutoaji wa huduma kwa watu walioathirika kwa majanga asilia, huku wakiwa wanasukumwa na Imani, ujasiri, udumifu na uthabiti wa moyo katika kukabiliana na changamoto za ulimwengu mamboleo, ili kudumisha Injili ya uhai duniani; kwa kusimama kidete kutetea utu na heshima ya binadamu sanjari na kudumisha haki jamii, ili kuwapatia watu matumaini ya maisha katika ngazi mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Mashirika haya mawili katika tamko lao la pamoja, wanaahidi kushirikiana kwa karibu zaidi kadiri inavyowezekana: kwa kushirikishana taarifa, malengo, changamoto na fursa zilizopo; kwa kukazia amani na utulivu. Watashirikiana katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano; kwa kujibu kilio cha walimwengu pamoja na kusaidia utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo ifikapo Mwaka 2030. Dhamana hii itawashirikisha wataalam na wadau mbali mbali kwa kuwa na sera na mikakati ya pamoja katika huduma kwa ngazi mbali mbali. Wajumbe wa ushirikiano huu watakuwa wanakutana walau kila mwaka kupanga sera, mikakati na utekelezaji wake.

Tamko la ushirikiano kati ya Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja na Shirikisho la Huduma ya Waluteri Duniani limetiwa sahihi na Bwana Michael Roy, Katibu mkuu wa Caritas Internationalis pamoja na Bi Maria Immonem, Mkurugenzi mkuu Shirikisho la Huduma ya Waluteri Duniani, tarehe 31 Oktoba 2016. Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.