2016-11-02 07:03:00

Papa Francisko: Uekumene wa umoja, huduma na mapendo!


Ushuhuda wa kiekumene unaotolewa na Waluteri na Wakatoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwa ni awamu ya pili ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, yaliyofanyika Jumatatu, tarehe 31 Oktoba 2016 kwenye Uwanja wa michezo wa Malmo, nchini Sweden wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko. Hapa alipata baahati ya kukutana na kuzungumza na wawakilisi wa Makanisa ya Kiekumene kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa kutambua kwamba, majadilialino ya kiekumene ni kati ya vipaumbele vya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, kwani kuna mambo mengi zaidi yanayowaunganisha Wakristo ikilinganishwa na mambo yale yanayowatenganisha. Waluteri na Wakatoliki wameungana kwa sala ili kuinua uso wao kwa Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake anasema, majadiliano ya kiekumene yamesaidia kujenga imani na kuimarisha ile kiu ya kutembea kwa pamoja ili kufikia umoja kamili wa Kanisa, matunda ya ushirikiano kati ya Kanisa Katoliki na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani. Kutokana na mazingira haya, Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja na Shirikisho la Huduma ya Waluteri Duniani wameweka sahihi makubaliano ya pamoja ili kujenga na kuimarisha utamaduni wa kushirikiana kwa ajili ya kuinua utu wa binadamu sanjari na kusimamia haki jamii. Baba Mtakatifu anawapongeza wajumbe wa Mashirika haya kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa ajili ya huduma kwa watu wanaoishi katika maeneo ya vita, kinzani na migogoro. Anawataka kuendelea kujikita katika njia ya ushirikiano.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, amesikiliza kwa umakini mkubwa shuhuda zilizotolewa na watu mbali mbali, changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kutunza mazingira nyumba ya wote, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa binadamu na fursa kwa binadamu kuweza kuutafakari kwa njia ya kazi ya Uumbaji. Uchafuzi wa mazingira unaendelea kusababisha madhara makubwa duniani, lakini waathirika wakuu ni maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi! Watu wote wanahimizwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, kwa kuwa na mwelekeo mpya wa mtindo wa maisha pamoja na kujikita katika misingi ya imani. Watu wajenge amani na utulivu miongoni mwao na mbele ya Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anapongeza juhudi zinazofanywa kwa ushirikiano kati ya Waluteri na  Wakatoliki nchini Colombia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana naye kwa ajili ya kuombea amani na maridhiano nchini Colombia. Sala hii, iwafikie na kuwaambata watu wote wanaoteseka kutokana na vita na kinzani za kijamii. Amani iwafikie hata watoto wanaoteseka kutokana na nyanyaso mbali mbali, watu ambao hawana tena sauti, ili watoto hawa waweze kupata mazingira yatakowawezesha kwenda shule, kukua pamoja na kupata afya njema.

Watu wengi zaidi waweze kujitokeza ili kuwa ni vyombo vya imani, matumaini na mapendo kwa wale waliokata tamaa. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kutumia vyema karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Vijana watambue kwamba,  wao ni watoto wapendwa wa Mungu. Sala na maombi yao yawawezeshe watoto wengi zaidi kupata fursa ya kusoma, amani na utulivu hasa huko Kusini mwa Sudan ambako hali yake bado ni tete sana!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru viongozi wa nchi mbali mbali ambao wamekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao, kielelezo cha mshikamano na utambuzi wa utu wao. Wakristo wanahamasishwa kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha, kielelezo makini cha upendo na huruma ya Mungu unaowakumbatia wote pasi na ubaguzi.

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka kwa namna ya pekee, Wakristo na wananchi wote wanaoishi huko Mashariki ya Kati, hususan Syria ambako wanaendelea kukabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na vita ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka mitano. Anawaombea viongozi wenye dhamana na hatima ya maisha ya wananchi wa Syria, kuongoka, ili kuweza kuokoa maisha ya watu wengi wanaoendelea kuteseka kwa vita. Shuhuda mbali mbali zilizotolewa ni changamoto na mwaliko kwa kushikamana na kushirikiana kwa pamoja kama sehemu ya mchakato wa kutafuta na kudumisha haki, amani na upatanisho, ushuhuda na matumaini ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.