2016-11-02 14:59:00

Papa Francisko: Majadiliano ya kiekumene na huduma ya Kiinjili!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 1 Novemba 2016 amehitimisha hija yake ya kitume nchini Sweden ambako alikwenda kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani pamoja na kukutana na kusali na Jumuiya ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Sweden, kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa Uekumene unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Malmo, nchini Sweden, Bi Alice Bah-Kuhnke, Waziri wa Utamaduni na Demokrasia kwa niaba ya Serikali ya Sweden alimsindikiza na hatimaye, kumuaga Baba Mtakatifu Francisko aliyerejea mjini Vatican majira ya mchana. Akiwa njiani, Baba Mtakatifu ametuma salam na matashi mema kwa Mfalme Carl Gustaf  XVI wa Sweden, kwa kumshukuru kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Sweden kwa wema, upendo na ukarimu ambao wameoneshwa wakati wa hija yake ya kitume nchini mwao. Amewahakikishia uwepo wake wa daima kwa njia ya sala na sadaka yake.

Baba Mtakatifu Francisko alipoingia kwenye anga la Ujerumani alimtumia salam na matashi mema, Rais Joachim Gauck wa Ujerumani, kwa kumhakikishia sala zake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Ujerumani. Kwa mara nyingine tena,  Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa familia ya Mungu nchini Austria aliomwandikia Bwana Doris Bures, ameitakia mafanikio mema.

Baba Mtakatifu Francisko amemwambia Rais Sergio Mattarella wa Italia kwamba, wakati wa hija yake ya kitume nchini Sweden amepata fursa ya kuwahamasisha Wakristo kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene sanjari na udumifu katika huduma ya Kiinjili. Baba Mtakatifu amewahakikishia wananchi wa Italia ustawi na maendeleo endelevu, huku akiwaombea baraka kutoka mbinguni. Mara tu baada ya kuwasili mjini Roma, Baba Mtakatifu alikwenda moja kwa moja kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, mjini Roma, ili kumshukuru Bikira Maria, afya ya Warumi, kwa kumwezesha kufanikisha hija hii ya kitume nchini Sweden.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.