2016-11-02 14:37:00

Papa Francisko achonga na waandishi wa habari!


Wakimbizi na wahamiaji; Daraja Takatifu ya Upadre kwa wanawake na msimamo wa Kanisa Katoliki; Majadiliano ya kiekumene na Kanisa la Kiorthodox, Kanisa Anglikani na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani; Amani, upatanisho na umoja wa kitaifa nchini Venezuela; Changamoto ya ukanimungu Barani Ulaya; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni kati ya tema msingi zilizogusiwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na Waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake nchini Swedeni, Jumanne, tarehe 1 Novemba 2016.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwa kazi nyeti waliyoifanya wakati wa Sala na ushuhuda wa kiekumene kati ya Waluteri na Wakatoliki. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru wananchi wa Swedeni ambao wamekuwa na utamaduni wa upendo na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji, kiasi kwamba, takwimu zinaonesha kwamba. Nchini humo kuna wakimbizi na wahamiaji wapatao millioni 9 na wengi wao wanatarajiwa kupewa uraia wa Sweden.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kutofautisha kati ya wakimbizi na wahamiaji. Wakimbizi ni watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kwa sababu mbali mbali na wanayo haki ya kimataifa inayowalinda na kuwasimamia ili waweze kupata hifadhi na usalama wa maisha yao. Ni watu wanaokimbia vita, dhuluma na nyanyaso; baa la njaa na majanga asilia yanayotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Wakimbizi wanahitaji msaada, huduma na fursa za ajira. Nchini Sweden, wakimbizi wamepewa kipaumbele cha pekee na Serikali katika kuwasaidia kujifunza, utamaduni na mapokeo ya wananchi wa Sweden.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Bara la Ulaya limejengeka kutokana na watu kutoka katika makabila, lugha na tamaduni mbali mbali. Anasikitika kuona kwamba, kuna baadhi ya nchi za Ulaya zinazojikita katika sera ya uchoyo kwa kutaka kufunga mipaka ya nchi zao, badala ya kuwa wazi na wakarimu kwa kubainisha sera na miakati ya kuwapokea na kuwapatia hifadhi bora ya maisha. Kila nchi iwajibike kadiri ya uwezo na rasilimali iliyopo. Wakimbizi na wahamiaji wasipopata hifadhi, wanatumbukizwa katika utumwa mamboleo na matokeo yake hata utamaduni unadumaa kutokana na woga na hofu isiyokuwa na mashiko!

Hapa Baba Mtakatifu anawataka wakuu wa nchi kujivika fadhila ya busara, ili kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanapata fursa ya watoto wao kwenda shule, kupata matibabu msingi, makazi bora na salama pamoja na fursa ya kazi. Sweden ni mfano bora wa kuigwa katika kuwapokea, kuwahifadhi na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji.

Baba Mtakatifu anasema, msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu Daraja Takatifu ya Upadre kwa wanawake, ulikwisha kutolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II na hapa hakuna mabadiliko. Kuhusu uwezo wa wanawake katika kutekeleza dhamana na wajibu wao kama Mapadre na Maaskofu, anasema, hana uhakika na mchuano mkali kati ya wanawake mapadre na wanaume mapadre! Wanawake wana karama na mapaji ambayo wakiyatumia vyema na kwa uaminifu wanaweza kufanya vyema zaidi hata kuliko wanaume. Haya ni mambo ambayo yanaweza kupembuliwa katika nyaraka mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.

Mtakatifu Petro ni mkuu wa kikosi kizima cha Mitume waliokabidhiwa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Mwelekeo wa Bikira Maria ni ushuhuda wa dhamana na utume wa wanawake katika ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Wakati wa Pentekoste, Bikira Maria alikuwa pamoja na Mitume wa Yesu. Kanisa ni Mama na mwalimu na hakuna Kanisa bila ya kuwa na mwelekeo huu wa Kimama!

Baba Mtakatifu anasema, Mwaka 2016 umefunikwa na matukio mengi ya majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiorthodox, Kanisa la Kianglikani pamoja na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani. Ni matumaini yake kwamba, ataendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika uhalisia wa maisha ya waamini kama alivyofanya alipowatembelea waamini wa Kanisa la Kipentekosti mjini Caserta, nchini Italia. Kanisa Katoliki kwa miaka mingi halikuwatendea haki waamini wa Makanisa ya Kipentekosti, kumbe, hapa kuna haja ya kuomba msamaha na kuanza mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya utengano, chuki na uhasama kati ya waamini. Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwani ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake. Majadiliano katika maisha ni chachu muhimu sana inayoweza kudumisha majadiliano katika ngazi mbali mbali ili kujenga utamaduni wa kufahamiana, kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja katika Kristo Yesu.

Chama cha Kikatoliki cha Uhamsho wa Roho Mtakatifu kwa kushirikiana na Chama cha Wakarisimatiki Wakatoliki kunako Mwaka 2017 wanaadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya uwepo na utume wao ndani ya Kanisa; matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Vyama hivi wakati wa Mkesha wa Pentekosti vitafanya kongamano la kimataifa naye anatarajiwa kushiriki kikamilifu. Baba Mtakatifu anawataka waandishi wa habari kuwa makini na matumizi ya Neno “Pentekosti” kwani linaweza kuleta utata kidogo!

Baba Mtakatifu anasema, Chama cha Wakarisimatiki Wakatoliki kilipoanzishwa nchini Argentina, alikuwa wa kwanza kukipinga kwamba, alitamani kuona Liturujia ikiheshimiwa na wala si kugeuka kuwa ni shule na mahali ambapo waamini walikuwa wanasakata Samba, hadi viatu kuchanika! Lakini leo hii, anamang’amuzi na mwelekeo na mtazamo tofauti kabisa, kwani taratibu aliweza kugundua tunu bora zilizokuwa zinafumbatwa katika maisha na utume wa Wakarisimatiki Wakatoliki; kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko kuhusu mkutano wake wa faragha na Rais Nicolàs Maduro wa Venezuela anasema, kumekuwepo na utashi wa kutaka kuonana na Rais Maduro tangu mwaka 2013 lakini kutokana na sababu mbali mbali mkutano huu haukuweza kufanyika. Akiwa njiani kutoka Mashariki ya Kati, Qatar na Falme za Kiarabu, Rais Maduro alisimama kidogo mjini Roma akiwa njiani kuelekea Venezuela na hivyo kupata nafasi ya kuzungumza na Baba Mtakatifu kwa muda wa nusu saa. Amemsikiliza kwa makini na kumuuliza maswali kadhaa.

Anasema, amekazia umuhimu wa Venezuela kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, kama njia ya kupata ufumbuzi wa kudumu kwenye mgogoro wa kisiasa unaoendelea kusababisha madhara makubwa kwa wananchi wa Venezuela. Hispania na Vatican ni kati ya nchi ambazo zimeombwa kushiriki katika mchakato wa majadiliano ya kisiasa nchini Venezuela anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Kuhusu changamoto ya ukanimungu inayoendelea kuzisakama nchi za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hapa kila mtu anawajibika kuilinda, kuitunza na kuishuhudia Imani yake kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alikazia umuhimu wa majiundo awali na endelevu; Katekesi makini na utamadunisho, ili kweli imani iweze kuingia katika maisha na vipaumbele vya watu, ili kusafisha na kuganga pale ambapo utamaduni unasigana na tunu msingi za Kiinjili. Kutokana na changamoto hizi za kiimani, Kanisa likaamua kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Ukanimungu ni dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu inayotaka kumwondoa Mungu katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu na matokeo yake ni kukosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha. Ukanimungu ni matokeo ya udhaifu wa mchakato wa Uinjilishaji wa watu na matokeo yake ni watu kumezwa mno na malimwengu na huko wanakiona cha mtema kuni! Kardinali De Lubac anasema, Kanisa linapomezwa mno na malimwengu hapa linakabiliwa na hatari kubwa katika maisha na utume wake. Waamini watambue kwamba, wako ulimwenguni lakini wao si wa ulimwengu huu, bali hapa ulimwenguni ni wapita njia tu!

Baba Mtakatifu anasema, ratiba ya hija zake za kitume bado haijakamilika lakini ana uhakika kwamba, atatembelea India na Bangaladesh. Anasikitika kusema kwamba, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Hii ndiyo maana Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Matha, kinaendelea kulivalia njuga janga ili hatimaye, kulipatia ufumbuzi wa kudumu. Baba Mtakatifu anayapongeza Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, Vyama vya kujitolea pamoja na wadau mbali mbali wanaoendelea kujifunga kibwebwe ili kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.