2016-11-02 08:20:00

Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri: Wakristo wameonja upendo wa Papa!


Kwa moyo wa dhati kabisa, washiriki wa tukio la kiekumene huko Malmo, Sweden, wamemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo wake wa kibaba katika tukio hilo. Shukrani hizo zimewakilishwa na Anders Arborelius, Askofu wa jimbo la Stocholm, Sweden, wakati wa adhimisho takatifu la Misa katika uwanja wa Malmo, Jumanne, tarehe 1 Novemba, 2016, Siku kuu ya Watakatifu Wote!

Siku hizo mbili za tukio la Sala ya kiekumene, zimekuwa siku za furaha katika imani, upyaisho wa Ukarimu na matumaini. Washiriki wamejisikia kuwa vijana tena, wenye furaha na waliojawa na Roho Mtakatifu, amefafanua Askofu Arborelius. Kwa Wakatoliki waishio imani yao katika nchi za pembezoni, ambapo hawana nafasi za kutosha kukutana na Baba Mtakatifu, imekuwa ni zawadi kubwa kukutana naye katika tukio hilo, ambapo wameonja upendo wake wa kibaba, na macho yake ya furaha na unyenyekevu, na hivyo kuwatia nguvu washiriki kushuhudia ufuasi wa Kristo hasa katika umoja, ili kuwaonjesha upendo huo watu wengine pia.

Ni furaha kubwa kuona jinsi Baba Mtakatifu Francisko, alivyowakumbusha washiriki wote na kuwahimiza juu ya wajibu wa kutenda kazi kwa pamoja, umoja na mshikamano, na kuwaonesha jinsi Mungu alivyo kati ya watu wake, na hasa maskini, wakimbizi, wahamiaji na waliosahauliwa. Wameshukuru kwa namna alivyoweza kuwasaidia kuivumbua Huruma ya Mungu na nguvu ya Injili katika dunia ya leo, ambayo mara nyingi imepoteza imani kwa Mungu. Askofu Arborelius kawaalika wote kuungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kutenda kazi kwa pamoja wakiwa wameshikama katika upendo wa Kristo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.