2016-11-02 07:22:00

Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri: Tamko la Viongozi wa Makanisa


Katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, kwenye Kanisa kuu la Lund, nchini Sweden, Jumatatu, tarehe 31 Oktoba 2016, Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya Kanisa Katoliki na Askofu Mounib Younan, Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, walitia sahihi ya makubaliano kwa Makanisa haya mawili kama sehemu ya maadhimisho haya.

Utangulizi wa makubaliano haya umesomwa na Askofu Helga Byfuglien, Makamu wa Rais, Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, ambaye amemshukuru Mungu kwa kuwawezesha viongozi wa Makanisa haya mawili kukutana na kusali pamoja katika Sala ya kiekumene kama sehemu ya uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani na miaka 50 ya Majadiliano ya kiekumene na Kanisa Katoliki. Katika kipindi hiki, tofauti nyingi zimeweza kupatiwa ufumbuzi, kiasi hata cha kujenga hali ya kuelewana na kuaminiana kati ya waamini wa Makanisa haya mawili.

Kumekuwepo na ushirikiano wa kiekumene katika huduma kwa watu wanaoteseka na kudhulumiwa, kielelezo cha Uekumene wa huduma unaojikita katika majadiliano na ushuhuda wenye mvuto na mashiko miongoni mwa watu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna mambo mengi yanayowaunganisha kuliko yale yanayowatenganisha. Viongozi hawa wanasema, wataendeleza mchakato wa majadiliano ili kuweza kutoa ufumbuzi wa kudumu kwenye vikwazo ambavyo vinaendelea kukwamisha majadiliamo ya kiekumene, ili kuweza kwa na umoja kamili.

Viongozi hawa wanasema, wataendeleza mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano ili kujibu kilio na kiu ya kiroho ya maisha ya waamini wao, yaani kuweza kuadhimisha wote Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hili ndilo lengo kuu la majadiliano ya kiekumene! Waamini wa Makanisa haya pamoja na wadau mbali mbali wanahamasishwa kujikita katika ugunduzi, furaha na matumaini, wanapoanza safari hii iliyoko mbele yao.

Katika tamko lao la pamoja, viongozi wa Kanisa Katoliki na Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani wanakazia mambo makuu yafuatayo: Mosi ni mchakato wa kutoka kwenye kinzani na kuanza kuelekea kwenye umoja unaonekana wa Kanisa. Wanatambua kwamba, tofauti za kitaalimungu zilimezwa na maamuzi mbele pamoja na kinzani, kiasi kwamba dini ikatumika kwa ajili ya mafao ya kisiasa.

Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inawadai toba na wongofu wa ndani, ili kuvuka matukio ya kihistoria na kinzani yaliyokwamisha huduma ya upatanisho. Ni wakati wa kufanya mabadiliko katika historia iliyopita, kuponya madonda na kumbu kumbu za kale; kwa kuondokana na chuki pamoja na kinzani kwa kisingizio cha udini. Waamini hawa wanatambua kwamba wamewekwa huru kwa njia ya neema ya Mungu na sasa wanataka kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja wa Kanisa, changamoto ambayo inatolewa na Mwenyezi Mungu mbele yao.

Pili, Waamini wa Makanisa haya wanataka kushirikiana na kushikamana katika kushuhudia neema na huruma ya Mungu iliyofunuliwa kwa njia ya Kristo Mfufuka, kwa njia ya Ubatizo ambao ni kifungo muhimu kinachowaunganisha, wakati huu wanapoendelea na mchakato wa kuondoa vizingiti vinavyokwamisha umoja kamili wa Kanisa, ili waweze kuwa wamoja ndani ya Kristo. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi ni kiini cha mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Kumbe, Makanisa haya mawili yataendeleza majadiliano ya kitaalimungu pamoja na kutafuta mbinu ya kuweza kuganga na kuponya donda hili ambalo bado linaendelea kulitesa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.

Lengo ni kuwawezesha Waluteri na Wakatoliki kwa pamoja kushuhudia Injili ya Kristo kwa kusimama kidete katika Uekumene wa huduma; kwa kulinda na kutetea: utu na heshima ya binadamu hasa miongoni mwa maskini, ili kuchuchumilia haki kwa kukataa vitendo vinavyosababisha kinzani; sanjari na kuendelea kushikamana na wale wote wanaotafuta utu na heshima yao; haki, amani na upatanisho.

Viongozi wa Makanisa haya mawili wanapenda kupaaza sauti yao dhidi vita na dhuluma zinazosababishwa na misimamo mikali ya kidini na kiimani, kwa namna ya pekee, dhidi ya Wakristo. Wanataka kushikamana ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaokimbia nchi zao kutokana na vita na madhulumu sanjari na kutetea haki za wakimbizi na watu wanaoomba hifadhi ya kisiasa, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Tatu, viongozi hawa katika tamko lao, wanawashuruku waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema ambao wamehudhuria na kushiriki katika Ibada ya Sala ya Kiekumene, wakati huu Makanisa haya mawili yanapoanza safari kutoka kwenye kinzani kuelekea kwenye umoja wa Kanisa, kwa kutambua msingi wa umoja huu ni Ubatizo. Waamini hawa wawakumbushe, wawaunge mkono na kuwakosoa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Waendelee kusali na kuambatana nao, katika utekelezaji wa malengo haya.

Mwishoni, Waluteri na Wakatoliki wanahamasishwa kujikita katika kipaji cha ugunduzi, kwa kuambata umoja ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowaongoza katika ushirikiano na mshikamano. Ni kipindi cha kusikilizana kwa kuishi na kumwilisha uhusiano kati ya Wakatoliki na Waluteri pamoja na kujiweka wazi mbele nguvu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa kujisimika na kumshuhudia Kristo Yesu, viongozi wa Makanisa haya wanataka kuwa warithi waaminifu wa upendo wa Mungu kwa watu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.