2016-10-31 10:16:00

Watawa wa kike ni alama ya matumaini kwa walimwengu!


Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, kuanzia tarehe 28 Oktoba  hadi 29 Oktoba, 2016 limeadhimisha Kongamano la Kimataifa kwa ajili ya wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Kongamano hili katika siku yake ya tatu, lilijikita kwa namna ya pekee katika maisha ya tafakuri kwa kuwaangalia watawa wa kike kama alama ya matumaini kwa watu katika ulimwengu mamboleo.

Padre Sebastiani Paciolla, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume anasema matumaini yanayofumbatwa katika Katiba ya Kitume “Kuutafuta uso wa Mungu” “Vultum Dei Quaerere” ni kuendeleza kwa ari na mwamko mpya maisha ya taamuli katika maeneo ya Uinjilishaji mpya, daima wakionesha ushirikiano wa dhati na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, ili kuwa na mikakati makini ya shughuli za kichungaji. Huu ni mwelekeo unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Sheria za Kanisa!

Watawa kutoka Mashirika mbali mbali ya Wamonaki wa ndani, lakini kwa kwa namna ya pekee Sr. Elena Beccaria na Sr. Stefania Costarelli wamepembua kwa kina na mapana mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba ya kitume “Kuutafuta uso wa Mungu”. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anapenda kukazia majiundo makini na endelevu kwa watawa wa ndani; umuhimu wa kujenga na kudumisha maisha ya umoja na udugu; maisha ya kiasi; ukimya na matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili kuwawezesha watawa kukaza macho yao kwa Uso wa Yesu.

Watawa waoneshe bidii, juhudi na mwamko wa kutaka kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Watawa wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kilio cha walimwengu, ili kuwajibu kwa wakati muafaka, vinginevyo, wanaweza kujikuta wakiwa wamepoteza mwelekeo na utambulisho wao wa Kikristo!

Sr. Stefania Costarelli amepembua kwa kina na mapana Kanuni ya Mtakatifu Benedikto : Sala na Kazi “Ora et Labora”. Huu ni mwongozo unaowasaidia Wabenediktini katika maisha na utume wao kuwa ni watu wanaofanya kazi kwa juhudi na maarifa ili waweze kujipatia mahitaji yao msingi pamoja na kuendelea kumwilisha matunda ya kazi hizi katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa njia ya kazi za mikono na akili zao wanamtukuza Mwenyezi Mungu, aliye asili ya wema na ukarimu wote. Wabenediktini ni watawa wanaojipatia chakula chao cha kila siku kwa kutokwa na jasho kama ilivyo kwa wakulima na wafanyakazi wengi duniani.

Monsinyo Orazio Pepe, Afisa mwandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume amechambua mambo ya Kisheria yanayotajwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Katiba ya kitume“Kuutafuta uso wa Mungu” “Vultum Dei Quaerere”. Amehitimisha kwa kusema, maisha ya taamuli yameendelea kupyaishwa ndani ya Kanisa kutokana na uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya watu wake, hata pale ambapo kumekuwepo na changamoto kubwa na hali ya kutaka kukata tamaa. Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, maisha ya taamuli yataendelea kupyaishwa ndani pamoja na Kanisa, ili kwa kuutafuta Uso wa Mungu, waweze kuona na kuguswa na mahangaiko ya binadamu katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.