2016-10-31 15:23:00

Tafakari ya Papa Francisko kwenye Ibada ya Kiekumene na Waluteri


Yesu Kristo kabla ya kujisadaka bila ya kujibakiza pale juu Msalabani, aliwaombea wafuasi wake kukaa ndani mwake naye ndani mwao, kielelezo makini cha upendo na umoja kwa wale wote wanaomwamini, changamoto kwao wote kubaki wakiwa wameungana, kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Maadhimisho ya Sala ya kiekuemene kwenye Kanisa kuu la Lund ni ushuhuda kwa Wakristo wa kutaka kuwa wamebaki huku wameungana na Kristo Yesu ili kuwa na maisha tele, tayari kushuhudia imani, matumaini na mapendo. Hiki ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwa jitihada mbali mbali ambazo zimefanywa na waamini katika kukuza na kudumisha mchakato wa kiekumene bila kukatishwa tamaa na utengano, bali wakaendelea kuwa na matumaini hai ya upatanisho kwa wale wote wanao mwamini Kristo Yesu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 31 Oktoba 2016, kwenye Kanisa kuu la Lund, nchini Sweden wakati wa Ibada ya Kiekumene kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Wakatoliki na Waluteri wamekwisha anzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika njia ya upatanisho. Maadhisho ya Mageuzi ya Mwaka 1517 iwe ni fursa ya kutembea kwa pamoja kama mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene yaliyoanzishwa na Makanisa haya mawili, takribani miaka 50 iliyopita.

Hakuna sababu ya kukata tamaa anasema Baba Mtakatifu Francisko, kutokana na utengano uliosababishwa na Wakristo. Umefika wakati wa kujenga umoja wa Kanisa kwa kurekebisha kinzani na mipasuko ya Kanisa iliyowasababishia Wakristo kushindwa kuelewana. Mwenyezi Mungu ndiye anayeendelea kuitunza bustani yake kwa kurekebisha mahusiano yao na Kristo Yesu ikiwa kama yanajikita katika umoja na upendo kwa kuendelea kuwatia shime ili kujitakasa kutokana na mapungufu yao ya kihistoria, ili kujikita katika mchakato wa kutekeleza kiu ya umoja wa Kanisa.

Wakristo wanapaswa kuangalia historia yao iliyopita kwa upendo na ukweli, ili kutambua makosa yaliyofanyika, tayari kuomba msamaha: kwani Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Hakimu mwenye haki, kwani utengano wa Wakristo unakwenda kinyume kabisa na mpango asili wa watu wa Mungu kuendelea kushikamana; umoja uliovurugwa na watu wenye nguvu duniani, lakini bado kuna haja kuongozwa kwa usalama na upendo wa Mchungaji mwema. Kwa pamoja, Wakristo wanataka kuungama na kutetea imani, ili waweze kuwa ni wajumbe wa ukweli unaolindwa na kutunzwa na Mwenyezi Mungu, anayewaangalia waja wake kwa jicho la upendo anayetaka kuwaona wakiwa wameungana na Mwanaye mpendwa, Yesu Kristo kwa kutambua ukweli wa tukio hili la kihistoria na kulipatia maana mpya zaidi, tayari kuzaa matunda yanayokusudiwa!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, utengano ndani ya Kanisa umekuwa ni chanzo cha mahangaiko na hali ya kutoelewana, lakini umekuwa pia ni wakati muhimu wa kutambua kwamba, bila Kristo Yesu hakuna lolote wanaloweza kufanya! Imekuwa ni nafasi ya kutambua kwa kina na mapana imani ya Kanisa; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa umuhimu wa Biblia katika maisha na utume wa Kanisa. Yameonesha umuhimu wa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu pamoja na kuendeleza majadiliano kati ya Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Duniani na Kanisa Katoliki, majadiliano ambayo sasa yanatimiza takribani miaka 50.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie kuwaunganisha kwa njia ya Neno lake, chakula cha maisha bila Neno la Mungu, Wakristo hawawezi kufanya lolote. Martin Luther anawaalika waamini kumtafuta Mungu mwenye huruma, kwa njia ya Neno wake aliyefanyika mwili, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kwa njia ya neema ya Mungu, anaweza kutenda kadiri ya utashi wake na kwamba, mafundisho juu ya kuhesababiwa haki ndani ya Kanisa yanaonesha umuhimu wa binadamu mbele ya Mungu.

Yesu anaendelea kuwaombea umoja wafuasi wake, ili kweli ulimwengu upate kuamini kwa njia ya huruma yake. Huu ndio ushuhuda ambao walimwengu wanasubiri kuuona kutoka kwa Wakristo. Wanaweza kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, ikiwa kama wataonesha msamaha, upyaisho wa maisha na upatanisho vitakuwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku. Kwa pamoja wanaweza kushuhudia huruma ya Mungu, kwa kulinda na kudumisha utu wa binadamu sanjari na kutoa huduma makini, kielelezo cha imani yao ya Kikristo. Waluteri na Wakatoliki wanasali pamoja kwa kutambua kuwa, bila Mungu juhudi zao zote ni bure. Waendelee kumwomba ili awajalie kuwa na umoja, kwa kuambata neema ili kwa pamoja waweze kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu, upendo na huruma yake kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.