2016-10-30 13:22:00

Papa Francisko: Hija ya kiekumene inayojikita katika udugu na umoja!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili  tarehe 30 Oktoba 2016 amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumsindikiza kwa sala na sadaka zako, wakati wa hija yake ya kitume nchini Swedeni kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 1 Novemba 2016 kama sehemu ya Jubilei ya miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani. Waamini wamwombee ili hija hii ya kitume iwe ni hatua mpya katika majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika udugu, ili kuweza kufikia umoja kamili wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, hili ni tukio ambalo litawaunganisha Waluteri na Wakatoliki kuadhimisha kumbu kumbu hii kwa kusali pamoja.

Baba Mtakatifu amewakumbuka wenyeheri wanne wafiadini waliotangazwa na Mama Kanisa huko nchini Hispania, Jumamosis tarehe 29 Oktoba 2016 na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Wenyeheri wapya ni: José Antón Gómez, Antolín Pablos Villanueva, Juan Rafael Mariano Alcocer Martínez e Luis Vidaurrázaga Gonzáles. Wafiadini hawa walikuwa ni Wabenediktini ambao waliyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake bila hata ya kujibakiza. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kujiweka pia chini ya maombezi yao na kwamba, hata leo hii, bado kuna waamini wanaomwaga damu kwa ajili ya imani yao Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu ametumia muda huu pia kwa ajili ya kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu walioathirika kwa tetemeko la ardhi kati kati mwa Italia, tetemeko ambalo limejirudia tena, Jumapili tarehe 30 Oktoba 2016 na kusikika hata mjini Roma. Baba Mtakatifu anawaombea waathirika wote na watu wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi, ili Kristo Mfufuka awajalie nguvu na Bikira Maria, awakinge kwa ulinzi na tunza yake ya kimama! Amewatakia waamini na mahujaji wote waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, heri na baraka kwa Siku kuu ya Watakatifu wote, itakayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 1Novemba 2016, changamoto na mwaliko wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.