2016-10-30 07:32:00

Miaka 50 ya uwepo na utume wa Wafokolari Kaskazini mwa Afrika


Nchini Algeria Jumuiya ya Wafokolari inaadhimisha miaka hamsini ya Uwepo na ya Maisha ya Utume wa Wafokolari katika Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati. Katika kituo cha Wafokolari kiitwacho Dar es Salaam, mjini Tlemcen Algeria, kunaadhimishwa tukio hilo tangu tarehe 1-2 Novemba, 2016 likienda sambamba na tukio lingine muhimu linalotangulia, la Kongamano la pili la Kimataifa la Waislamu Wafokolari, kutoka nchi za Lebanon, Misri, Yordan, Italia, Ufaransa, Sweden na Canada. Rais Mwambata wa Wafokolari Jesùs Moràn, anashiriki pia tukio hilo muhimu.

Wafokolari walipoingia Algeria, wengi hawakuelewa nini wanapaswa kufanya katika utume huo wanapojiunga, lakini pole pole walibadilishwa na kujifunza kutokana na nyimbo na utendaji mbali mbali, vilivyogusia nyanja nyingi za maisha na hasa wito wa kuishi upendo kati ya watu. Ndivyo anavyoeleza Daktari Mourad, aliyejiunga Fokolari akiwa kijana wa miaka kumi na saba, na sasa ametimiza miaka sitini na saba ya umri, akiendeleza utume wa Kifokolari.

Fokolari imegusa maisha ya watu wengi katika maeneo ya Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati, imewatia hamasa, ikawapa ujasiri wa kuwa wa kwanza kuanzisha utamaduni wa kukutana, kujenga madaraja kati ya watu, kushirikishana tunu za utu na maadili, kujithamini na kuthamini wengine, na kujenga urafiki na udugu kwa upendo. Ndivyo wanavyoshuhudia baadhi ya Wafokolari nchini Aljeria.

Kwa upande wake, Henri Teissier, Askofu Mkuu Mstaafu wa Algeri anasema: kanisa nchini Algeria kupitia Wafokolari, limeweza kukazia juu ya mahusiano na mazungumzano kati ya watu wa dini na itifaki mbali mbali. Wameweza kutafsiri hayo katika utamaduni wa watu wa Aljeria, na kuwa Jumuiya ya waamini wanaotafuta wengine ili kujitambua kwa pamoja. Wafokolari wa kwanza walifika Algeria tarehe 16 Oktoba 1966, nao ni waitaliano wawili: Salvatore Strippoli na Ulisse Caglioni; pamoja na mwenzao Mfaransa, Pierre Le Vaslot. Kazi waliyoianzisha, imezaa matunda mema katika nchi za Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati, kiasi cha kusherehekea sasa kwa furaha kubwa na mbwembwe nyingi, miaka hamsini ya utume huo maeneo hayo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.