Maneno msingi ya Kongamano la Kimataifa wa Wakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na wale wa Maisha ya Wakfu ni uhusiano shirikishi. Kongamano hili limeanza Oktoba 28, 2016, katika ukumbi wa Mtakatifu Clement mjini Vatican, kwa makaribisho ya Baba Mtakatifu Francisko, aliyewahimiza washiriki: Kuyapenda Maisha ya Wakfu, na hivyo kutafuta ufahamu wa kina juu yake. Zaidi ni kujenga mahusiano shirikishi kwa kuzingatia Kanuni za Kanisa kama Jumuiya, Uwepo sambamba, na kujitegemea kwa haki na uwiano.
Akiwakilisha mada yake, Gianfranco Ghirlanda, aliongelea wajibu wa Maaskofu katika kujali na kuchunga Mashirika ya Maisha ya Wakfu. Maisha ya Wakfu ni zawadi ya Roho Mtakatifu, sio tu kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, bali kwa Kanisa zima. Hivyo ni jambo la msingi kwa viongozi wa Kanisa kuhakikisha kuwa tunu Injili zinatafsiriwa vema na kuziishi inavyopaswa.
Sr. Nicla Spezzati, ambaye ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, ametazama zaidi jinsi watu wa Maisha ya Wakfu wanavyoishi na kutenda utume wao kwa kung’amua baadhi ya Nyanja msingi zinazoendana na Utume wao, wanapokuwa katika Makanisa Mahalia. Kawaalika watu wa Maisha ya Wakfu, kuendelea kukua kimisionari na kijumuiya pamoja na watu, ili kujenga mahusiano mazuri yenye kuzaa matunda, kama ambavyo Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, amesisitiza katika Barua yake ya Kitume,”Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo” Novo millennio ineunte.
Leonello Leidi, Afisa Mwandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Maisha ya Wakfu, amekazia umuhimu wa wajibu wa Maaskofu kuchanganua kwa makini karama na uhitaji wa Mashirika ya Kitawa na Maisha ya Kitume, kabla ya kuyatambua kisheria. Ni kweli kuwa karama hizi ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu, lakini ni ukweli pia kuwa ni wajibu wa Kanisa kuchanganua na kupembua vema uhalisia, uaminifu na uhitaji wake katika zama za leo; pamoja na malezi yao sahihi, ambao ni wajibu wa Maaskofu wakishirikiana katika umoja na Baba Mtakatifu.
Askofu Mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Maisha ya Kitume, amekazia Uhusiano-Shirikishi kati ya Makleri-Jimbo na Watu wa Maisha ya Wakfu. Palipo na kukutana katika kweli kati ya watu au vikundi vya watu, patakuwa na Uhusiano-Shirikishi, iwapo pia heshima na unyenyekevu katika mazungumzano vinazingatiwa, katika roho ya kidugu. Hivyo yanapopatikana mafanikio, huwa ni juhudi za pande zote mbili zinazosafiri pamoja. Vinginevyo panapotokea mafarakano na kuanguka, kawaida huwa ni makosa ya pande zote mbili.
Na Padre Celestine Nyanda
Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican
All the contents on this site are copyrighted ©. |