2016-10-30 13:10:00

Huruma ya Mungu inawakumbatia wote hata akina Zakayo!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana Jumapili tarehe 30 Oktoba 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alitafakari kuhusu kisa cha Zakayo mtoza ushuru aliyekuwa tajiri na kwa utajiri wake akawanyonya na kuwanyanyasa wananchi. Hata Zakayo alitamani kumwona Yesu, lakini kutokana na hali yake ya kuwa mtoza ushuru na mdhambi mkubwa alishindwa kumkaribia Yesu. Lakini mbaya zaidi anasema Baba Mtakatifu alikuwa ni mfupi wa kimo, hali iliyomlazimu kuparamia mkuyu ili aweze kumwona Yesu aliyekuwa anapitia katika njia ile!

Yesu alipofika eneo lile na kumwona, Zakayo mtoza ushuru, akamwamuru kushuka mtini, kwani alitamani kushinda nyumbani mwake. Hapo Zakayo akashuka kwa haraka huku akiwa amepigwa bumbuwazi. Yesu anamwambia Zakayo kwamba alikuwa na wajibu wa kutekeleza mpango wa Mungu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Hiki ni kielelezo cha mpango wa huruma na ukombozi kwa mwanadamu unaowakumbatia hata akina Zakayo mtoza ushuru, mdhambi na mtu ambaye hakuwa mwaminifu, kiasi hata cha kudharauliwa na watu.

Baba Mtakatifu anasema, lakini Zakayo alikuwa ni mtu aliyehitaji kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kuanza ukurasa mpya wa maisha, licha kwamba alijitajirisha kwa kutumia mgongo wa jirani zake! Lakini Yesu akiwa anaongozwa na kusukumwa na huruma ya Mungu alikuwa anamtafuta mtu kama Zakayo, ili kumshirikisha wokovu wa Mungu ambao ni zawadi kwa watu wote pasi na ubaguzi.

Yesu anangalia kwa huruma na wala dhambi na wala maamuzi mbele si kikwazo kwake, kwani anamwangalia mtu kwa jicho la kimungu ambaye habaki kwenye historia ya kale, bali anaangalia mafao ya mbeleni; hakatishwi tamaa kwa ubinafsi, bali anafungua fursa mpya za maisha; haangalii yale mambo ya nje, bali anaangalia moyo wa binadamu!

Baba Mtakatifu anasema, mdhambi anaweza kurekebishwa kwa kumwonesha  tunu msingi za maisha zinazoangaliwa na Mungu licha ya mapungufu yake ya kibinadamu. Mwelekeo huu wa maisha ni changamoto kubwa inayomwezesha mdhambi kufungua kutoka katika undani wake utu na wema uliofichika kutoka katika sakafu ya moyo wake. Mdhambi athaminiwe na kujengewa imani, ili hatimaye, aweze kukua na kubadilika.

Hivi ndivyo anavyotenda Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Kamwe hakwamishwi kwa dhambi za binadamu, bali anavuka vizingiti vyote hivi kwa njia ya upendo unaomwezesha kung’amua wema na uzuri uliomo ndani mwao. Bikira Maria awawezeshe waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuona wema na uzuri uliomo ndani ya watu wanaokutana nao kila siku ya maisha yao, ili kuiona ile sura na mfano wa Mungu uliochapwa katika mioyo yao. Kwa njia hii, waamini wataweza kushangazwa na huruma ya Mungu inayoendelea kutenda miujiza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.