2016-10-29 11:10:00

Kutana na Zakayo aliyeparamia mkuyu ili kukutana na Uso wa huruma!


Hii ya leo ni kali! Usingoje kusimliwa na jirani ataongeza chumvi bure, jipatie nakala yako mwenyewe! Jumapili iliyopita tulisikia Yesu anasafiri kutoka Galilea kuelekea Yerusalemu. Leo Yesu yuko mjini Yeriko. Yeriko ulijengwa bondeni wakati mji wa Yerusalemu ilikuwa mlimani. Watu walienda Yerusalemu ili kusali hekaluni, tofauti na Yeriko mji wa kiuchumi. Wakazi wake walifanya biashara na matajiri wa Misri na wale waliozunguka bahari ya kati (Mediteraneani). Matajiri na watu wakubwa walikuwa na majumba ya kupumzika huko Yeriko.

Huu ndiyo mji kulikotokea kituko cha leo. Lakini kabla yake, tunasimulia uponyi wa kipofu. “Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia akiomba sadaka.” Kipofu huyo aliketi kwa sababu alishindwa kutembea akichelea kupotea au kujikwaa. Yesu anamponya na akaweza kuona tena njia. Uponyaji  huu ni maingilio ya kituko kifuatacho. Baada ya uponyaji wa kipofu: “Naye Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake,” maana yake kujipitisha hadharani ili aonekane.

Yesu anapita katika mitaa ya miji na vijiji vyetu kwa sababu yeye ni Mungu aliyefika kujionesha kwetu (Epifania). Katika kukata mitaa ya Yeriko kulikuwa na mtu mmoja tena Mtoza ushuru aliyewania sana kumwona Yesu. Kwa kawaida watoza ushuru au kodi walihesabiwa kuwa na sifa ya wizi na dhuluma ya mali ya watu. Walinufaika sana kutokana na mwanya wa kutoza kodi zaidi hivi walikuwa matajiri, waliishi maisha mazuri na walikula vizuri na walitegemewa wawe wamelitulia na kuridhika. Kutokana na mwelekeo huu, waliangalia pia kwa jicho la kengeza na jamii iliyowazunguka!

Mtoza ushuru huyo aliitwa Zakayo kutoka neno la kiebrania Zakai maana yake safi. Jina hilo Zakai linatajwa mara tatu kuonesha ukamilifu wa usafi wa mtu huyo. Huyu Zakayo alikuwa Mkubwa wa watozaushuru kwa kigiriki ni Architeiones, sifa iliyotumika na mwinjili Luka peke yake kwani siyo msamiati wa kawaida katika lugha ya kigiriki.  “Zakayo alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani.” yaonekana alikuwa anakereketwa na jambo lililomnyima raha, na alisikia mambo ya Yesu, hivi akahaha kutaka kumwona Yesu laivu, anayeweza kuelewa matatizo yake na kumpa faraja na amani. Kwa bahati mbaya umati wa watu ulimzuia kumwona Yesu kwa sababu alikuwa mfupi wa kimo. Umati huo ni ule wa watu waliomzunguka Yesu waliowania kutaka kumwangalia lakini hawakumwona sawasawa. Kwa vyovyote baada ya kuona umati ule uliomzunguka Yesu, Zakayo angeweza kushiti na kurudi nyumbani kuendelea na maisha yake.

Hali ya Zakayo ya kutambua udogo wake inawakilisha wale wote wanaojiona wadogo na wanataka kumwona Yesu. Kumbe anayejiona kuwa ni mrefu haoni sababu ya kujitaabisha kutaka kumwona Yesu. Hata kwetu sisi, kama tunajiona tunafahamu tayari Biblia, Maandiko Matakatifu, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii ya Kanisa tunajisikia tumemzunguka Yesu, tunaenda Kanisani kila jumapili kusali, na hatuna mahangaiko yoyote ya ndani hapo hatuoni sababu ya kujihangaisha na Yesu. Kwa vile Zakayo amewania kumwona Yesu licha ya ufupi wake, hapo anaamua kujiongeza. “Zakayo akatangulia mbio akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.” Zakayo anakwea mkuyu na kutafuta pahala anapoweza kumwona Yesu vizuri lakini yeye mwenyewe bila kuonekana, yaani anataka kuficha mahangaiko yake ya ndani.

Kumbe, tukitaka kuuona Uso wa Kristo, ufunuo wa huruma ya Baba wa milele, yatubidi kukwea Mkuyu. Huo mkuyu waweza kuwa Maandiko Matakatifu (Biblia) au hata neno jema toka kwa jirani. Zakayo akiwa juu ya mkuyu anafanikiwa kumwona Yesu. Lengo la Zakayo ni kuuona uso wa Mungu jinsi ulivyojiakisi au kijionesha katika Yesu. Yaani huyu Yesu yupoyupoje! Hebu sasa tuione tabia ya uso wa Mungu iliyojifunua katika Yesu ambayo Zakayo anahaha kutaka kuiona. Tutaorodhesha tabia kadhaa za uso wa Mungu katika Yesu anazoziona Zakayo:

Mosi, “Yesu alipofika mahala pale, alitazama juu” Tabia ya kwanza ya uso wa Mungu iliyojiakisi katika Mwana wake ni kuinua macho na kutazama juu. Katika Injili tunamkuta Yesu daima amekaa chini au hata akipiga magoti na kuinuka kutazama juu. Mathalani kwa mama yule mzinifu: “Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke.” Huyu ndiye Mungu katika Kristu anayemtumikia binadamu daima anatuangalia sisi. Kinyume na fikra zetu tunapodhani kwamba binadamu ndiyo walio chini na kuinua macho kumwangalia Mungu juu.

Pili, Yesu anamwona kwa nafasi ya kwanza yule aliyejificha kutokana na aibu. Yesu amezungukwa na wengi lakini anamwona Zakayo aliyejificha. Kumbe hata kama tunajisikia aibu kutokana na dhambi zetu, Mungu anatupenda kama tulivyo na anatuangalia. Tatu, Yesu anamwita kwa jina: Zakayo! yaani safi, mzuri. Yesu anatufahamu na kutuita kwa majina yetu tena anaona uzuri tu kutoka kwetu.

Nne, “shuka upesi.” Upendo haupotezi muda. Uso huu wa Mungu katika Kristu ni kama mtu anayependa sana na hataki kupoteza muda. Ingawaje Zakayo ni mdhambi Yesu hamwambii labda aende kwanza kuungama, la hasha bali anataka kupata furaha ya kuonana naye. Anamwita ashuke upesi. Tano, “Leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.” Yesu anajialika mwenyewe kwenda nyumbani kwa Zakayo. Yesu daima anabisha mlango wa moyo wako. Sita, “Imenipasa kukaa nyumbani” Kutokana na upendo alio nao kwa mdhambi, Yesu anaona ulazima wa kukaa na Zakayo. Yesu ni Mungu anayeomba kukaribishwa. Sisi sote tuna nyumba, tunatakiwa kumkaribisha Yesu anayetaka kukaa nasi.

Saba, Zakayo anashuka kwa haraka na kumkaribisha kwa furaha. Katika Injili ya leo tunashuhudia matukio ya mwendo kasi: “Yesu anaingia mji wa Yeriko, anapita mji wa Yeriko. Halafu Zakeo anakimbia kutangulia mbele; anapanda mkuyu; na sasa Zakayo anashuka kwa haraka.” Lakini baada ya kushuka kutoka kwenye mkuyu kuna hali ya utulivu. Kwani sasa Yesu anajisikia nyumbani, hivi ametulia na anapiga mazungumzo na Zakeo. Nane, Zakayo akafurahi. Kwa vyovyote kumkaribisha Yesu nyumbani kunaleta furaha. “Mgeni afike mwenyewe apone.” Tisa, baada ya kuona hayo yote, watu walianza kunung’unika. Kwa sababu Yesu aliingia katika nyumba ya mdhambi. Watu hawakutegemea kuuona uso wa Mungu anayeshirikiana na wadhambi. Mbaya zaidi kiasi cha kuingia hata majumbani kwao.

Kwa hiyo wenye haki wale waliomzunguka Yesu wamekwazwa. Karibu mara tatu Yesu anakosolewa na kunung’unikiwa katika Injili ya Luka kutokana na kushirikiana na wakosefu: Mosi, alipoingia katika nyumba ya Mlawi. Pili, Yesu anaposimulia mfano wa mwana mpotevu kwamba anakaa na wakosefu na kula nao. Tatu, ni katika nafasi hii anapoingia kwenye nyumba ya mkosefu Zakayo. Yawezekana hata sisi tunaojiona tuko karibu na tumemzunguka Yesu tukapata shida kumpokea Mungu mwenye Uso wa huruma na wa kushirikiana na wadhambi. Kumbe Yesu ni Mungu anayewakwaza wenye haki.

Kumi, Yesu ameingia nyumbani kwa mkosefu kwa vile amependa, hivi hajali maneno ya wengine. Yafuatayo ni mambo ya uso wa Mungu yanayotokea baada ya kupokewa na Zakayo yumbani mwake. Kumi na moja, Zakayo akasimama, kwa kigiriki ni statheis maana halisi ya neno hilo ni akajisimamia (akiwa wima) ni sawa na mtu mpya aliyezaliwa baada ya kugundua uso wa Yesu. Kwa hiyo anayeigundua Injili (kama yule kipofu aliyeona) anaweza kusimama na kutembea akijua kinachotakiwa katika maisha, yaani ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Zakayo amegundua kwamba Mungu amemwona na kumpenda jinsi alivyo. Wale watu waliokuwa nje, wakabaki wanamkosoa Yesu wakidai kwamba Mungu hawezi akafanya kama alivyofanya Yesu kuchangamana na wadhambi. Kumbe, Zakayo alitambua  kwamba, Yesu amempenda na ametulia na kufurahi kuwa naye. Kumi na mbili Zakayo akasema: “Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang’anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.” Kabla yake Zakayo alikuwa kipofu hakuweza kuwaona maskini. Mali ambayo aliona yangempa maana katika maisha, kumbe sasa anaona ni mali ya kuwagawia wahitaji. Kumbe tukiwania kumwona Yesu, yeye atatuponya upofu wetu na tutaweza kuwaona wahitaji, maskini na kuwagawia haki yao.

Kumi na tatu, Yesu hagombi, hatishi, halaani, haadhibu mkosefu. Huo ndiyo uso wa Mungu. Simulizi letu linaishia hapa, hatusikii chochote zaidi juu ya Zakayo hata kama sisi tungetamani kujua kinachofuata baada ya hapo. Kumbe huyu Zakayo ni kila mmoja wetu. Leo tunaambiwa kuutafuta uso kweli wa Yesu kwani katika kuonana naye tutaweza kutatua mahangaiko yetu ya ndani ndiye atakayetupa furaha na amani.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.